3566; Tofauti na matarajio.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Wanaoianza safari ya mafanikio huwa ni wengi.
Lakini wengi sana huishia njiani, kwa kukata tamaa na kuachana kabisa na safari hiyo.
Na hilo halitokani ni kwamba mafanikio hayawezekani.
Bali linatokana na uhalisia kuwa tofauti na matarajio.
Kila anayeianza safari ya mafanikio kwenye eneo lolote la maisha yake huwa anakuwa na matarajio fulani.
Anapoenda na safari hiyo, matokeo anayokuwa anayapata kwenye uhalisia yanakuwa tofauti kabisa na matarajio aliyokuwa nayo.
Ni tofauti hiyo ya uhalisia na matarajio ndiyo inayopelekea wengi kukata tamaa na kuishia njiani.
Kadiri matarajio yanavyokuwa makubwa na uhalisia kuwa tofauti na matarajio hayo, ndivyo ukataji tamaa unavyokuwa wa haraka.
Kuna vitu vitatu ambavyo mara zote huwa vinakuwa tofauti kwenye matarajio na uhalisia.
Moja ni UGUMU.
Uhalisia huwa ni mgumu kuliko matarajio.
Kwenye mipango yako unaona kabisa utatoka A kwenda B kisha C na kuendelea hivyo mpaka Z.
Lakini kwenye uhalisia mambo huwa ni magumu kuliko mipango na matarajio hayo.
Utaanzia kwenye A na hutaweza kufika B kwa sababu ya vikwazo unakutana navyo.
Au utavuka A na kwenda C, kisha kurudi B.
Mambo yanakuwa mvurugano sana kiasi cha kuona kama hayawezekani.
Kama uliona mafanikio yatakuwa rahisi, hutadumu pale uhalisia unapojidhihirisha.
Mbili ni MUDA.
Mafanikio kwenye jambo lolote yanachukua muda mrefu kuliko unavyokuwa unategemea.
Utaweka juhudi sana, lakini utaona kama hakuna hatua unazopiga.
Muda utaenda na utaona kama hakuna kinachoendelea.
Hapo ndipo wengi hukata tamaa na kupoteza muda na juhudi wanazokuwa wameshaweka.
Matokeo hayajawahi kuja kwenye muda ambao mtu anatarajia, uvumilivu ni muhimu sana ili mtu kufanikiwa.
Tatu ni GHARAMA.
Mafanikio yana gharama kubwa kuliko ambavyo mtu alitarajia.
Kwa gharama zozote unazokuwa umetarajia kulipa, uhalisia unakuwa ni tofauti, kwa sababu gharama zinakuwa ni kubwa zaidi.
Kwa sababu ya ugumu utakaokutana nao, ambao hukutarajia na muda kuwa mrefu kuliko matarajio, gharama zinakuwa kubwa pia.
Na hii ndiyo hatua inayowalazimisha watu kuachana na safari ya mafanikio.
Kwa sababu pale fedha zinapowaishia huku gharama bado zipo, hawawezi kuendelea na safari.
Hili ndiyo eneo la kuzingatia sana, kuhakikisha fedha ulizonazo ni nyingi kuliko mipango na matarajio yako.
Rafiki, ni mara ngapi umeishia njiani kwenye yale uliyopanga kwa sababu ya ugumu, muda kuwa mrefu na gharama kuwa kubwa kuliko ulivyotegemea?
Kwa chochote unachopanga, jua kitakuwa kigumu sana, kitachukua muda mrefu na gharama kubwa kuliko matarajio yako.
Ukijiandaa vyema kwenye hayo, utaweza kudumu kwenye safari ya mafanikio na kufanikiwa kama ulivyopanga.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe