Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Unanijua mimi rafiki yako jinsi ambavyo huwa napinga kabisa uchezaji wa kamari na michezo ya kubahatisha. Hivyo ni vitu ambavyo vimekuwa vinasukumwa sana kwa watu, na kuonekana kama ndiyo njia ya mkato ya kufanikiwa.

Kamari na michezo ya kubahatisha vinafanya safari ya mafanikio ionekane nyepesi sana. Kwamba hakuna haja ya kuweka juhudi kubwa, ni kubashiri tu na kupata matokeo makubwa.

Uongo huo wa kamari kuwa njia ya mafanikio umekuwa unasukumwa kwa nguvu kubwa sana. Kwa wachache wanaobahatisha kutumiwa kama ushuhuda kwa wengine kuendelea kucheza, ili nao wapate ushindi.

Pamoja na kelele zote zinazopigwa, bado kamari na michezo ya kubahatisha siyo njia ya mtu kutegemea kwenye kupata mafanikio makubwa kwenye maisha. Haipaswi hata kufikiriwa kama njia inayowezekana, lakini wengi wamekuwa hawapendi kusikia ukweli huo.

Pamoja na ukweli huo ulio wazi kwamba wanaoshinda kamari na michezo ya kubahatisha ni wachache sana, bado watu wamekuwa wanaendelea kupoteza kiasi kikubwa cha fedha kwenye michezo hiyo.

Hii inafanya tulazimike kuangalia upande mwingine wa hii michezo, ina kitu gani hasa mpaka watu wawe tayari kupoteza fedha? Na je hicho ambacho michezo hiyo inatoa, hakiwezi kutumika kusaidia watu kupata mafanikio makubwa?

Hilo ndiyo tunakwenda kulipata kwenye #BaruaYaKocha, ambapo utajifunza kamari moja ya kucheza ambayo unahitaji kushinda mara moja tu na uwe umetoboa kabisa kimaisha. Karibu ujifunze ili uweze kuyabadili maisha yako na kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

1. Kamari Inatoa Matumaini Ya Ushindi.

Pamoja na watu kupoteza fedha nyingi kwenye kamari na michezo ya kubahatisha, bado wamekuwa wanaendelea kucheza. Haiwezekani watu wakawa wajinga au wazembe kiasi cha kupoteza tu pesa. Lazima kuna kitu wanapata, hata kama siyo ushindi wa pesa wanaokuwa wanategemea.

Na hilo ni kweli, kwani tafiti nyingi ambazo zimefanywa kwa watu wanaocheza kamari na michezo ya kubahatisha, zinaonyesha watu wanavutiwa zaidi na matumaini ya ushindi kuliko ushindi wenyewe.

Iko hivi rafiki, watu wengi wana maisha duni na hakuna ushindi wowote wanaopata kwenye maisha yao. Wanapocheza kamari na michezo ya kubahatisha, wanakuwa na matumaini huenda wakashinda. Ni hayo matumaini ndiyo yanawasukuma waendelee kucheza hata kama wanapoteza. Kwa kipindi kifupi wanachokuwa na matumaini ya kuweza kushinda, wanajisikia vizuri sana.

Hayo matumaini ya ushindi kwenye kamari ndiyo tunakwenda kuyageuza na kuyatumia kwenye kupata mafanikio makubwa tunayoyataka.

2. Kamari Pekee Unayohitaji Kucheza.

Kwa sababu manufaa ya kamari ni yale matumaini ya kushinda, tunaweza kuyatumia hayo kupata mafanikio makubwa tunayoyataka. Tunachohitaji ni kuchagua kamari sahihi ya kucheza, ili tuwe na hayo matumaini yatakayotusukuma kuendelea hata kama tunakutana na magumu na kupoteza.

Kamari pekee unayopaswa kucheza ni kwako wewe mwenyewe, kwenye maisha yako. Kamari hiyo ni kujiahidi na hata kuwaahidi watu wengine kwamba utapata mafanikio makubwa unayoyataka kwenye maisha yako. Na usiseme tu mafanikio kwa ujumla, badala yake eleza kwa hakika ni mafanikio gani hasa unayoyataka.

Ukishachagua kile unachotaka kwenye maisha yako, kazi yako inabaki ni kucheza tu. Kama ambavyo wacheza kamari wanaendelea kucheza licha ya kupoteza, wewe pia ndivyo unapaswa kuendelea kufanyia kazi mchakato wako bila kuacha.

Haijalishi ni matokeo gani unayapata, endelea kubaki na tumaini la ushindi unakuja. Hilo tumaini ndiyo litakalokuvusha kwenye nyakati zote ngumu utakazopitia kwenye hiyo safari.

Watu wengi wanayataka mafanikio makubwa, lakini yamebaki kwa wachache kwa sababu wanapokutana na magumu wanaacha. Na wanaacha kwa sababu wanakosa kabisa matumaini. Wewe kuwa na tumaini kubwa la kamari ya maisha yako na hakikisha unaendelea bila kujali unakutana na nini.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK114; Cheza Hii Kamari Ambayo Unahitaji Kushinda Mara Moja Tu ‘Utoboe’ Milele