Sikiliza hapa; 

Rafiki yangu Mpendwa,

Nimekuwa nakuambia na kukukumbusha kwamba mambo mengi tunayohangaika nayo, ni kwa sababu tunataka kupata vitu vikubwa viwili; uhuru na furaha. Hayo ndiyo mahitaji makubwa kwetu binadamu na yanayotusukuma kufanya yote tunayoyafanya.

Lakini sasa, kwa bahati mbaya, tumekuwa tunachukua hatua ambazo matokeo yake ni kutunyima hayo mawili. Kwenye uhuru hilo liko wazi sana, kuna mambo tunayafanya tukidhani yatatupa uhuru, ila ndiyo yanauondoa zaidi.

Chukua mfano wa mtu anayepata kazi au biashara ambayo inamlipa zaidi, anaifanya kwa matarajio ya kipato kikubwa kumweka huru. Lakini matokeo yake ni kazi au biashara hiyo kumbana sana kiasi cha kukosa kabisa uhuru.

Upande wa furaha nao una changamoto hiyo hiyo, mambo tunayohangaika nayo, tukidhani yanatupa furaha, yamekuwa yanaishia kutunyima zaidi furaha.

Na kubwa kabisa ni kukazana kuipata furaha yenyewe. Furaha huwa ni kama kipepeo, kila unapokazana kuikamata ndivyo inavyozidi kukukimbia.

Kuna wajibu umekuwa unajipa, wajibu ambao huwa nauita ni ukiranja wa dunia na umekuwa unakukwamisha sana kupata furaha. Hilo ndiyo tunakwenda kulijadili hapa kwenye #BaruaYaKocha ili uweze kujenga maisha ya kupambania mafanikio bila kukwamishwa na furaha.

1. Ijue Kanuni Ya Furaha.

Eh, na furaha nayo ina kanuni? Ndiyo, kila kitu kwenye maisha huwa kina kanuni. Na ukiona unapambana sana na kitu bila kupata matokeo, kwa sehemu kubwa hujui kanuni au kama unaijua basi huitumii.

Kanuni ya furaha ni kama ifuatavyo;

FURAHA = UHALISIA/MATARAJIO

Kwa maneno, furaha ni sawa na uhalisia gawanya kwa matarajio. Hivyo furaha inategemea vitu viwili, matarajio unayokuwa nayo na uhalisia unaopatikana.

Sasa basi, na hapa nisikilize kwa umakini na taratibu, pale kunapokuwa na kugawanya namba mbili, namba ya chini ndiyo huwa inaamua zaidi majibu. Namba ya chini ikiwa kubwa, majibu yanakuwa madogo na namba ya chini ikiwa ndogo, majibu yanakuwa makubwa.

Kwa mfano, nane gawa kwa mbili ni nne (8/2 = 4), wakati nane gawa kwa nne ni mbili (8/4 = 2). Kama namba ya juu inabaki ile ile, namba ya chini ikiongezeka majibu yanapungua.

Hivyo basi, furaha yako imekuwa inaathiriwa na matarajio yako. Kadiri matarajio yako yanavyokuwa makubwa, ndivyo furaha yako inakuwa kidogo. Kwa sababu mara nyingi uhalisia huwa ni tofauti kabisa na matarajio unayokuwa nayo.

Njia ya uhakika ya kuwa na furaha mara zote ni kuwa na matarajio madogo sana, kiasi kwamba uhalisia wowote unaokutana nao unakushangaza. Kama kila matokeo unayopata yanakuwa ambayo hukuyatarajia, lazima utayafurahia.

Ni kama unapokuwa na uhitaji mkubwa wa fedha, halafu kukawa na mtu anayekudai. Akakupa ahadi kwamba siku inayofuata anakulipa. Ukienda kulala na matarajio kwamba unalipwa, halafu ikatokea hajakulipa, utaumia sana. Lakini ukienda kulala ukijua hutalipwa, na hivyo kuweka mipango mingine, usipolipwa haitakuumiza sana, maana ulitarajia hivyo. Na ikitokea ukalipwa, utafurahia sana, maana siyo kitu ulichotegemea.

Niseme jambo muhimu hapa, huku siyo kufikiri hasi, bali ni kuenda na uhalisia jinsi ulivyo. Mambo huwa hayatokei kwa sababu tunataka yatokee, hivyo kuwa chanya hakutabadili uhalisia wa mambo. Unapaswa kuwa chanya kwenye yote unayofanya, hasa yaliyo ndani ya uwezo wako. Lakini inapokuja kwenye matokeo, ambayo huyadhibiti moja kwa moja, nenda zaidi na uhalisia kuliko matarajio yako.

2. Huidai Dunia Chochote.

Ukipata ajali kwenye njia ya treni, wewe ndiye unahesabika umeigonga treni na siyo treni kukugonga wewe. Hiyo ni kwa sababu treni ina njia yake, wewe ndiye unakuwa umeifuata kwenye njia yake.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye dunia. Ukiwasikia watu wakiwa wanailalamikia dunia, unaweza kudhani wao ndiyo waliiumba dunia. Kumbe wamekuja hapa duniani na kuikuta dunia tayari ipo.

Yaani dunia ipo, inajiendea na mambo yake, haijui hata kama mtu upo. Halafu mtu huyo huyo anakuwa anailaumu dunia kwa mambo yanayokuwa yanaendelea. Hapo ndipo watu wengi wamekuwa wanajinyima furaha wao wenyewe.

Haijalishi utalalamika na kulaumu kiasi gani, dunia haitaacha mambo yake kwa sababu yako wewe. Dunia haitabadilika kufuata matakwa yako wewe. Ni wewe ndiye unayetakiwa kubadilika ili uendane na dunia, kwa sababu huidai chochote.

Ukiweza kutambua huidai dunia chochote na ukashukuru kwa kila unachopata, utakuwa na furaha wakati wote. Hii haimaanishi utapokea kila unachopata, bali utapambana ili upate unachotaka, bila kulalamika au kulaumu chochote.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK115; Kiherehere Chako Cha Kutaka Kuwa Kiranja Wa Dunia Ndiyo Kinakukwamisha Kuyafurahia Maisha