Ni jambo la kawaida kwa binadamu mambo yanapokuwa magumu kutafuta wa kumpa lawama. Tunapenda sana kulaumu, kwa kuwa tunapotoa lawama zetu tunapata ahueni kwamba sio kosa letu  kwa mambo kuwa magumu, sio sisi tuliosababisha yote hayo, kuna mtu mwenye mamlaka ambae ameshindwa kutimiza tuliyotaka.  Yawezekana ni kweli kabisa kwamba kuna mtu amechangia jambo fulani kutowezekana, lakini kabla ya kumtupia hizo lawama hebu kwanza jiangalie wewe mwenyewe unahusika kwa kiasi gani kwa hilo jambo kutowezekana. Kwa tatizo lolote lile unalokutana nalo kwenye maisha asilimia 80 ni wewe umesababisha na asilimia 20 ndio zimesababishwa na unayemlaumu. Kushindikana kwa jambo lolote lile kunaanza na wewe, yaweza kuwa umekosea kwenye kuchagua, utekelezaji, kuamini, uzembe n.k. Katika baadhi ya matatizo  wengi tunashawishika sana kulaumu mazingira, serikali, taasisi, jamii n.k. Yaweza kuwa kweli kwamba mojawapo ya hiyo mifano imechangia kwenye kukukwamisha lakini kuna jinsi ambavyo ungeweza kufanya jambo kwa utofauti na ukapata matokeo tofauti na hayo yaliyokukwamisha. Katika mazingira hay ohayo ambayo wewe umeshindwa kuna mwenzako amefanikiwa, jiulize kwa nini yeye ameweza na wewe umeshindwa?
   

Unapolaumu unapata ahueni na kujiona wewe huna hatia, ni rahisi sana kulaumu na katika jambo lolote lile hakosekani wa kulaumiwa. Kupenda kulaumu kuna hasara kubwa katika maisha yako, kuna hasara kuu mbili za kulaumu; kuwa mnyonge na kutokufanikiwa kabisa.

  Unapomlaumu mtu, mazingira ama mamlaka yoyote kunakufanya wewe kuwa mnyonge. Kunakufanya ushindwe kuwa msimamizi wa maisha yako na kutegemea unayemlaumu afanye jambo ili wewe uweze kufanikiwa. Unakosa nguvu ya kusimamia maisha yako, unafanya jambo kwa utegemezi mkubwa na hivyo inakufanya uwe mtumwa. Ni sawa na kuyakabidhi maisha yako kwa mtu ama taasisi unayoilaumu iamue inachotaka kuyafanya maisha yako.
  Katika kufanya jambo na ikatokea umeshindwa kufanikiwa unapomlaumu mtu ama taasisi kunakuondoa katika mstari wa mafanikio. Lawama unayoipeleka kwa wengine inakufanya wewe ujione huna tatizo, kushindwa kwa jambo ulilokuwa unafanya ni matatizo ya wengine hivyo inakuwa ngumu kwako kujitathmini na kuona ni wapi ulipokosea. Kama ukianza kujilaumu wewe, kutakufanya ufikiri zaidi ni wapi ulipokosea na ni njia gani tofauti ambayo ungeitumia ungeweza kufanikiwa.
  Wewe ndio kiongozi wa maisha yako, amua sasa kusimamia na kuongoza maisha yako. Usikubali kumwachia nafasi mtu yeyote akukwamishe, kwa jambo lolote uliloshindwa kufanikiwa wewe ndio wa kwanza kulaumiwa, jitathmini na usirudie kosa.