Linapokuja swala la kuuza wengi wetu hufikiri wafanya biashara pekee ndio wanaouza, hivyo wao ndio wenye wajibu wa kujifunza jinsi ya kuuza zaidi. Tunakosea sana, sio kweli kwamba wafanyabiashara pekee ndio wauzaji bali kila mtu ni muuzaji tofauti yetu ni vitu tunavyouza. Maisha ni kuuza kama huuzi basi huishi. Unaweza kuwa unauza bidhaa ama huduma ama unauza muda. Wafanya biashara na walijiajiri wanauza bidhaa ama huduma. Kama umeajiriwa basi unauza muda wako na taaluma yako kwa mwajiri wako. Viongozi na wanasiasa nao pia wanauza, wanauza sera ili waweze kukubalika. Hata katika maswala ya mahusiano mtu mmoja anapomwomba mwingine wawe wapenzi ama wanandoa anakwenda kuuza, anauza tabia, mwonekano, ahadi nzuri n.k.
   Duniani kuna watu waliofanikiwa sana kufikia malengo yao na wengi sana wameshindwa kufikia malengo yao. Ukiangalia hakuna tofauti kubwa ya kimaisha, kielimu ama kimazingira kati ya waliofanikiwa na walioshindwa. Tofauti kubwa ni namna wanavyouza. Watu wote waliofanikiwa kwenye nyanja yoyote kimaisha wanajua jinsi ya kuuza kile walichokuwa nacho. Viongozi wakubwa na matajiri wakubwa ni wauzaji wazuri, wameuza bidhaa, huduma, mawazo, ama vipaji walivyonavyo.
  Ni vyema kila mtu akajitafakari anauza nini kisha atafute njia bora zaidi ya kuuza ili kuweza kufanikiwa. Ni muhimu kila mtu kujifunza kuuza, soma mambo yanayohusiana na kuuza ili kupata mawazo na kujua ni jinsi gani wengine wanauza. Maisha ni kuuza, jitahidi uweze kuuza vizuri ili uweze kufanikiwa.