Umewahi kupita njia fupi ili kufika unakokwenda haraka? Je umewahi kukwepa foleni ndefu ya magari kwa kupita vichochoroni? Je huwa ukivaa nguo unajiangalia na kuona kama umependeza ama zimekutoa vizuri? Kama jibu ni ndio kwa swali lolote hapo basi wewe ni mbunifu, tena mbunifu mzuri. Kila mtu ni mbunifu, kuishi tu mpaka hapo ulipofikia ni ubunifu umekusidia.
   Kama kila mtu ni mbunifu kwa nini hatutumii ubunifu wetu kufikia maleng yetu? Jibu ni kwamba hatuuthamini ubunifu wetu. Linapokuja swala la ubunifu wengi hufikiri ni mambo makubwa kama ubunifu wa mavazi, ugunduzi wa teknolojia na kadhalika. Ubunifu sio lazima kwa mambo makubwa hivyo, jambo lolote unalofanya kukutofautisha na wengine ama kukurahisishia kazi ni ubunifu. Tumia ubunifu wako unaoutuma katika maisha ya kila siku kukusaidia kufikia malengo yako.
   Kama ukiweza kutumia ubunifu wako na mazingira yako basi itakuwa rahisi sana kufikia malengo yako uliyojiwekea kwenye maisha. Haihitaji kuwa na elimu kubwa kuweza kugundua ubunifu wako. Kila mtu ni mbunifu na kila mtu ana kipaji fulani, tatizo kubwa ni kukitambua ama kukithamini kipaji chako.
   Dunia imefika hapa ilipo kutokana na ubunifu wa watu na ili kuiendeleza tunahitaji kutumia ubunifu wetu. Mashine mbalimbali ziligunduliwa baada ya watu kutafuta njia rahisi ya kufanya kazi. Maendeleo  makubwa ya teknolojia tunayoyaona wote ni ubunifu. Njia bora za kilimo, biashara na hata usafiri tulizo nazo sasa ni ubunifu wa watu.
    Ubunifu hauna mwisho na wala hakuna mtu anaeweza kuiba uwezo wako wa ubunifu. Kama ukiweza kutumia ubunifu wako vizuri hutakuwa na haja ya kuiga wengine wala kushindana nao. Chanzo kikubwa cha ushindani kwenye nyanja mbalimbali ni ukosefu wa ubunifu. Na katika ushindani wowote aliebuni huwa mshindi na alieiga hushindwa. Hakuna anaependa kushindwa hivyo basi tumia ubunifu wako kukuweka katika nafasi ya ushindi.