Umeweka malengo yako na mipango ya kuyafikia ila muda unakwenda na hufiki kule unakotarajia! Unafanya kila unachoweza lakini bado majibu sio mazuri. Je unajua tatizo linaweza kuwa nini? Kuna tatizo kubwa ambalo sio rahisi kulijua kwa sababu limejificha kwenye vitu unavyofanya. Unaweza kuwa unafanya vitu vingi lakini hujui vipi vinakupatia majibu mazuri na vipi havikupatii majibu mazuri ama vinatumia muda na nguvu nyingi lakini majibu yake ni finyu.

  Kaa chini na utafakari kwa makini uandike vitu vyote ambavyo ukivifanya vitakufikisha kwenye malengo yako. Angalia vitu ama tabia ambazo ukiwa nazo miaka kumi ijayo utakuwa umepiga hatua kubwa kwenye maisha yako. Anza kutekeleza moja baada ya nyingine ila anza na ile unayoona ni ya muhimu zaidi ama itakupatia majibu mazuri zaidi. Ukishachagua cha kufanya ni lazima kujifunza kustahimili na kutokata tamaa ama kuishia njiani. Kwa mfano unaweza kuamua kutenga saa moja kila siku kujisomea na kujiendeleza kwenye jambo unalofanya, ukiweza kuifanya hii kila siku ndani ya muda mchache utaanza kuona mafanikio.

business planner 

  Pia kaa na utafakari na uandike mambo ambayo unayafanya sasa ila hayana mchango wowote kwenye malengo yako. Andika mambo yote ambayo yanachukua muda wako mwingi na nguvu zako ambayo kila siku unayafanya. Anza mpango wa kuacha kufanya mambo hayo na anza na yale ambayo yanakuchukua muda na nguvu nyingi zaidi. Weka mpango wa kuondoa kabisa hayo mambo ama tabia ili uweze kufikia malengo yako. Kwa mfano unaweza ukawa unatumia muda wako mwingi kwenye mitandao ya kijamii(facebook, twitter n.k), kama ukiweza kupunguza muda huo na kuuweka kwenye mambo yaliyo kwenye malengo yako utayafikia haraka.

  Kwa kufanya mambo hayo mawili, kuongeza nguvu na muda kwenye mambo yanayokuletea majibu unayotaka na kupunguza mambo yanayokupotezea nguvu na muda kutakuhakikishia kuyafikia malengo yako ndani ya muda uliojiwekea.