Duniani kuna watu wengi na wengi wamepita vizazi na vizazi. Katika watu hao wengi wachache sana wanajua ni nini waliletwa kufanya duniani. Wengi wamepita na wachache sana waliweza ama wameweza kukamilisha sehemu kidogo ya maisha yao hapa duniani.
Kuna uwezekano mkubwa sana hata wewe hujui umekuja kufanya nini duniani, kama hujui sio kosa lako ila ukimaliza kusoma hapa na bado ukashindwa kutimiza lengo lako hapa duniani basi utakuwa na tatizo kubwa. Usiseme umeletwa duniani kuishi, hata chura anaishi, je thamani yako wewe ni sawa na chura? Kuna sababu kubwa ya wewe kuwa hapa duniani na kwa bahati nzuri leo inaweza kuwa siku muhimu sana kwenye maisha yako kwa kujua sababu hiyo.
Tumeletwa duniani kufanya mabadiliko baasi, hakuna la ziada. Tofauti kubwa na uwezo ulionao wewe mwanadamu tofauti na wanyama wengine wanaoishi kama wewe ni wewe kuweza kuleta mabadiliko. Kama huleti mabadiliko yoyote utakuwa na tofauti gani na wanyama wengine?
Ili kuweza kuleta mabadiliko cha kwanza ni kubadili hali iliypo, sheria, uelewa, ujuzi, na mitazamo ya watu. Huwezi kufanya mabadiliko kwa kufuata sheria zilizowekwa ama mitazamo iliyopo. Ni lazima uende mbele zaidi ya viwang vilivyowekwa ili kuweza kuwaonesha watu vitu ambavyo wamezuiwa kuviona, kwa kutokujua kama vipo ama vinawezekana. Naposema uvunje sheria simaanishi uende ukaibe ama ufanye uhalifu, hapana, namaanisha uende zaidi ya pale watu walipokubaliana ni kikomo.
Ugunduzi wote unaotokea duniani unatokana na watu kuenda zaidi ya kipimo. Kama watu wangeridhika na kiwango kilochokuwepo enzi hizo mpaka sasa tungekuwa tunatumia zana za mawe, kusingekuwa na kompyuta, vyombo vya usafiri na vingine vingi ambavyo vimegunduliwa miaka ya hivi karibuni.
Karne ya kumi na saba(wakati huo utawala wa Roma ukiwa na nguvu) mwanafalsafa na mnajimu Galileo Galilei alikwenda kinyume na utawala wa Roma. Roma iliweka sheria kwamba Dunia imesimama katikati na jua ndio linazunguka dunia. Kwa hiyo jua linachomoza asubuhi na linatua jioni(ndivyo inavyoonekana hivyo kwa mawazo rahisi kila mtu atakubali). Galileo baada ya kufanya majaribio mbali mbali aligundua kwamba jua ndio limesimama kati kati na dunia inalizunguka jua. Utawala wa Roma ulipopata habari zake alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kwenda kinyume na sheria(nadhani unajua nguvu ya utawala wa roma kipindi hiko). Galileo hakukubali kubadili ugunduzi wake kwa sababu ya sheria hivyo alifungwa mpaka alipofia jela. Baadae sana ilikuja kugundulika ni kweli aliyoyasema Galileo.
Kwa mfano huo wa Galileo (ipo mingine mingi sana) inaonesha ni jinsi gani watu wanaweza kuwa wagunduzi kwa kutkubaliana na hali iliyopo. Na pia hali iliyopo inawalemaza wengi kutofikiri kubadili hali.
Hakikisha unaanza leo safari ya kuleta mabadiliko duniani. Usikubali kupita tu hivihivi bila kuacha alama yoyote. Kwa uwezo na kipaji cha pekee ulichonacho unaweza kufanya makubwa sana yatakayoweza kuisaidia dunia. AMKA NA UFANYE MABADILIKO.