Kwa mfano nikikupigia simu sasa hivi na kukuambia kwamba nahitaji kukaa na wewe kwa saa moja na unielekeze kuhusu jambo fuani linalohusiana na unachofanya utaniambia nikupe shilingi ngapi? Je unajua saa yako moja ina gharama ya shilingi ngapi? Kwa wengi ni ngumu sana kujibu hilo swali. Unaweza kujitetea kwamba kwa kazi unayofanya huwezi kujua gharama ya saa yako moja, ila sio kweli. Kwa kazi yoyote unayofanya hata kama ni kilimo kila saa, dakika na hata sekunde yako ina gharama.

timemoney

  Kama mpaka sasa hujui gharama ya saa yako moja ni vyema ukajifunza hapa ili uweze kujua kwa sababu ni muhimu sana kwa wewe kufikia malengo yako. Ni lazima ujue gharama ya muda wako ili usiutumie tu hovyo.

  Sote tunajua kwamba ni lazima kuwa na malengo kwenye maisha na kwamba malengo yamegawanyika kwenye makundi mbalimbali. Kundi mojawapo la malengo ni malengo ya kifedha.

  Ili kuweza kujua gharama ya muda wako kwanza ni lazima uwe na maengo ya kifedha. Kwa mfano kama lengo lako ni kupata shilingi milioni ishirini(tsh 20,000,000/=) ndani ya mwaka mmoja ujao ni rahisi kujua saa yako moja itagharimu shiingi ngapi.

wekundu

Mwaka mmoja una wiki hamsini na mbili(52), tukindoa wiki nne za kupumzika ama likizo zinabaki wiki 48 za kufanya kazi. Wiki moja ina siku tano za kufanya kazi(hiki ni kiwango cha chini kuna wengine wana siku 6 au 7) kwa kutumia siku tano za wiki kwa wiki 48 utakuwa na siku 240 za kufanya kazi kwa mwaka.

  Siku moja ina masaa nane(8) ya kufanya kazi, hichi pia ni kiwango kidogo ila kuna wenye mpaka masaa 12 ya kufanya kazi kwa siku. kwenye siku 240 za kazi kwa mwaka utakuwa na masaa 1920 ya kufanya kazi kwa mwaka.

  Ukigawanya milioni 20 unazotaka kupata kwa mwaka kwa masaa 1920 ya kufanya kazi unapata shilingi 10, 416/=. Kwa hiyo kwa hesabu za karibu ni shilingi  elfu kumi kwa saa.

  Hivyo kama unataka kutengeneza shilingi milioni ishirini(20,000,000/=) kwa mwaka inabidi kila saa (katika masaa nane ya kufanya kazi kwa siku) uitengeneze shilingi elfu kumi(10,000/=).

PESA TZ

Hayo ni mahesabu kwa kiwango hich cha hela ila unaweza kufanya kulingana na kiwango unachotaka wewe inaweza kuwa pungufu ya hapo ama zaidi ya hapo.

  Pia katika hesabu zako ni vyema kutenga muda wa dharura kwa mambo yatakayojitokeza yatakayoweza kusababisha usifanye kazi, kwa mfano magonjwa ama misiba ya watu wa karibu. Sio muda mwingi sana hivyo kama unatumia zaidi ya saa nane kwa siku kufanya kazi(na ni lazima kufanya hivyo kama unataka kuleta tofauti) bado hesabu zitakuwa sawa na hizo.

  Unafanya nini pale ambapo huna kazi ya kufanya?

  Unaweza kuwa umeshafanya hesabu zako na kupata gharama za muda wako. Ila kwa sasa huna kazi unayofanya ili kuingiza kipato hicho kwa saa! Ama unaweza kusema kwa kuwa sasa huna kazi ama biashara unayofanya hivyo huna haja ya kufanya hesabu hizo!

  Hata kama kwa sasa huna kazi unayofanya, ni muhimu kufanya hesabu hizo kwa kuwa tayari una malengo ya kufikia hatua fuani. Baada ya kujua gharama zako basi hakikisha kila saa unaitumia kukuweka kwenye mazingira ya kupata kiasi ulichopanga. Kama gharama ya saa yako moja ni shilingi elfu kumi basi kila unachofanya kikuweke kwenye mazingira ya kuja kutengeneza hiyo elfu kumi ama zaidi. Inaweza kuwa kwa kuendelea kujifunza, ama kutengeneza mtandao wa watu amba ni muhimu kwa ujuzi ulionao.