Moja ya vitu ambavyo mfumo wa elimu umetufunza vizuri ni kutofanya makosa. Mfumo wa elimu unamfundisha mtu kutofanya makosa na kuogpa kabisa kufanya makosa. Ndio maana adhabu nyingi za shuleni zinatokana na makosa mbali mbali. Jamii nayo imechukua mfumo huo huo wa kufundisha watu kugopa kufanya makosa. Nguvu nyingi imetumika kukufundisha wewe kugopa kushindwa, kwa kuwa kufanya makosa ndio kunaleta kushindwa.

avoid mistakes

  Unaweza ukawa umelielewa vizuri somo la kutofanya makosa na unaishi maisha yako kuhakikisha hufanyi kosa lolote. Unaishi maisha ambayo unahofia sana kushindwa kuliko  kitu kingine chochote.

  Unaweza kuona ni kitu kizuri kwa wewe kuogopa kushindwa ama kufanya makosa, ila kuogopa huko ndiko kushindwa kwenyewe. Ukishakuwa na woga wa kushindwa huwezi kujaribu jambo lolote jipya ambalo linaweza kukupatia manufaa makubwa. Kwa kuwa umeshatengeneza kuogopa kukosea unafanya yale tu unayoyajua na kuona usiyoyajua sio sahihi kufanya. Hiki ni kifungo kikubwa kwenye maisha yako.

  Ili uweze kuleta mabadiliko kwako na kwa wanaokuzunguka huna budi kujaribu vitu usivyovijua kabisa. Ni lazima ushindwe hapa na pale, ni lazima ufanye makosa kadhaa ili kujua njia bora na ndipo utakapoleta mabadiliko ya kweli.

  Sio lazima kila mara ufate sheria zilizowekwa, inabidi uvunje baadhi ya sheria ili kuweza kuleta kitu kipya. Naposema uvunje sheria simaanishi ufanye uhaifu, namaanisha uvunje taratibu zilizowekwa kitaaluma ama kijamii, ila usiende kinyume na sheria za asili(laws of nature) na pia usisababishe madhara kwenye maisha ya mtu ama kiumbe mwingine.

  Jaribu mambo mapya, kosea hapa na pale kisha jifunze kutokana na makosa. Hakuna somo zuri kama tunalojifunza kutokana na makosa. Ni somo ambalo kama utajifunza hutolisahau kamwe. Na somo ambalo huwezi kulisahau ndilo linalokuletea mafanikio kwenye maisha.

  Wanasema uoga wako ndio umasikini wako.