Dunia ya sasa michezo imechukua sehemu kubwa sana ya burudani zetu. Katika kipindi hiki ni vigumu kukuta mtu hana mchezo wowote anaoshabikia. Kama hushabikii mpira wa miguu, basi utashabikia mpira wa kikapu, pete ama mpira wa mikono. Kama haupo kwenye mpira basi utakuwa unashabikia ngumi, mieleka au riadha. Kwa vyovyote vile kuna mchezo ambao ukiwa unafanyika basi lazima ufuatilie na kujua nini kinaendelea.

  Pamoja na ushabiki wako mzuri kwenye mchezo unaoupenda kuna siri moja kubwa hujawahi kuifikiria kuhusu mchezo unaoupenda. Siri hii inahusisha mafanikio ya kwenye maisha na kufikia malengo yako na mchezo unaoupenda. Baada ya kuijua siri hii leo kila mara utakapokuwa unautizama mchezo unaoupenda itakufanya pia ufikirie malengo yako na jinsi ya kufanikiwa.

   Mchezo wa mpira wa miguu ndio mchezo ambao kwa sasa una mashabiki wengi sana. Watu wako radhi kukesha kuangalia mchezo na wengine wako radhi kupoteza kiasi kikubwa cha fedha kwa kutabiri matokeo ya timu zao pendwa. Je unapouwatazama wachezaji pale uwanjani unajifunza nini kuhusiana na mafanikio?

  Mchezo wa ngumi na mieleka nayo imekuwa na mashabiki wengi mno. Hebu fikiria, kwenye ngumi mtu anapigwa na wewe unashangilia!! Unajifunza nini hapa kuhusu maendeleo na kufikia malengo?

  Somo kuu tunaloweza kujifunza na unalotakiwa kujifunza kila unapotizama mchezo unaoupenda ni kwamba ili ufanikiwe kwenye maisha ni lazima uumie, baasi, hakuna la ziada.

  Kama livyo wachezaji wa mpira wanakimbia uwanjani dakika tisini(na mara nyingine zaidi ya hapo), wanachoka sana na wengine wanaumia, lengo kuu ni wewe kufurahi. Mtu anajitoa kuchoka, kuumia na hata saa nyingine kufa ili tu wewe ufurahi na yeye aweze kufikia malengo yake. Hii inamaana bila ya wewe kuchoka na wakati mwingine kuumia sana huwezi kufanikiwa kwenye maisha.

kuumia2kuumia3

  Kama ilivyo kwa mabondia, mtu anakwenda kupigana, akijua kabisa atapigwa na ataumia. Na wewe shabiki unakaa pale ukifurahia kuona binadamu mwenzako anashushiwa makonde ya nguvu kama mbwa mwizi. Kuumia kwake ndio furaha yako, na furaha yako ndio mafanikio yake.

kuumia

  Ni dhahiri hakuna mafanikio yanayokuja bila ya kuchoka na kuumia. Hivyo unapochoka na kuumia jua ndivyo njia ya mafanikio ilivyo ngumu.

   Kuanzia sasa unaposhabikia mchezo unaoupenda, kuumia kwa wale wachezaji kukutie moyo kwamba ndivyo safari ya mafanikio ilivyo. Tusikate tamaa, tuendelee na mapambano na siku moja tutakuwa washindi kwenye michezo yetu wenyewe. Mchezo wako mkuu ambao utachoka, utaumia ila mwisho wa siku utashinda ni maisha.