Kama umewahi kupanda gari na kukaa karibu na dereva utakuwa umeshaona dereva anavyoendesha gari anakuwa katika hali gani. Na kama umewahi kuendesha gari unajua ni jinsi gani unajisikia ukiwa unaendesha mwenyewe tofauti na unapokuwa unaendeshwa.
Kama umepanda gari inayoendeshwa na mtu mwingine na gari ikawa inakwenda kwa mwendo wa kasi sana lazima utakuwa na wasiwasi mkubwa. Ila wakati wewe una wasiwasi huo dereva anayeendesha gari anakuwa hana wasiwasi wowote.
Gari inapokuwa inaendeshwa kwa mwendo kasi wewe uliyepanda unakuwa na mawazo na wasi wasi kwamba kama chochote kikitokea inaweza kuwa ajali kubwa na ikaleta madhara kwenye maisha yako au hata kifo. Ila dereva anayeendesha gari hilo kwa mwendo kasi anakuwa hana wasiwasi mkubwa kwa sababu ana uhakika kila kitu kipo chini yake na anakijua chombo chake vizuri.
Mfano huu wa gari unafanana sana na maisha yetu ya kila siku.
Kama wewe ndio kiongozi mkuu wa maisha yako na ndio unayasimamia maisha yako huwezi kuwa na wasi wasi mkubwa kwenye maisha.
Kama huna umiliki wa maisha yako na umewaachia wengine ndio waongoze maisha yako kila siku utakuwa na wasiwasi kwa kuwa hujui anayeongoza maisha yako anaweza kufanya maamuzi gani na yakaathiri maisha yako.
Kama kweli unataka kuwa na furaha kwenye maisha na kufanikiwa kufikia malengo yako ni lazima uwe kiongozi wa maisha yako. Ni lazima uweze kuyapangilia maisha yako na kuweka malengo na mipango ya kufikia malengo hayo. Ni lazima katika wakati wowote kwenye maisha yako ujue unafanya nini na kwa sababu gani.
Unaporuhusu mtu mwingine afanye maamuzi juu ya maisha yako unakosa uhuru mkubwa wa maisha yako. Kila siku utakuwa na hofu juu ya maisha yako kwa kuwa hujui anayefanya maamuzi hayo kesho anaweza kufanya maamuzi gani.
Unapomtegemea mtu mwingine moja kwa moja maisha yako yanakuwa ya kitumwa. Kwa kuwa yule unayemtegemea ndiye atayekuwa na maamuzi juu ya maisha yako.
Kwa chochote unachofanya kwenye maisha, iwe umejiajiri, umeajiriwa ama unafanya biashara hakikisha maamuzi muhimu juu ya maisha yako unayafanya wewe mwenyewe. Hakikisha kwa kiasi kikubwa maisha yako hayawezi kutetereka kwa maamuzi ya mtu mwingine hata awe mwajiri wako.
Ndege anatua kwenye mti na kukaa kwa starehe sio kwa sababu analiamini sana tawi la mti ila kwa sababu anaziamini mbawa zake. Popote ulipo na chochote unachofanya usiweke imani yako juu ya mtu ama kitu chochote ila kwako mwenyewe. Jua kwamba una uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo makubwa. Kuona kwamba mtu mwingine ndiye anayeweza kukuendeshea maisha ni kuudhalilisha uwezo mkubwa ulioko ndani yako.
Kama ulishapoteza uhuru wa maisha yako anza sasa kuchukua hatua za kushikilia usukani wa maisha yako.
Maisha yako yatakuwa ya maana na furaha sana kama wewe ndiye utayekuwa dereva. Unapokuwa dereva unaamua mwendo gani uendeshe na pia unakijua chombo chako vizuri hivyo unaweza kuendesha unavyotaka mwenyewe kama hutovunja sheria zilizowekwa.
Chukua hatua dhidi ya maisha yako sasa.
Kwel kabisa timiza ndoto zako mwenyew usitegemee mtu akufanikishie mambo yako!
LikeLike
NDIO HIVYO MKUU
LikeLike