Pamoja na kwamba mambo yamebadilika sana hasa kwenye zama hizi za sayansi na teknolojia, kuna wafanyabiashara wengi sana ambao bado wameshikilia imani za kishirikina au uchawi katika biashara. Moja ya imani hizo ni kitu kinaitwa CHUMA ULETE.
Kama hujui CHUMA ULETE, maana yake ni kwamba wewe unachuma halafu unampelekea mwenzako bila ya wewe mwenyewe kujua. Yaani kuna wafanya biashara wanaamini kwamba hawapati faida kwenye biashara zao kwa sababu kila wanapochuma kuna mtu wanampelekea bila kujijua. Hivyo fedha zinatoka kwao na kwenda kwa mtu mwingine kwa njia ya uchawi.
Imani hii ni kali sana kwa baadhi ya watu kiasi kwamba wanaweza kuepuka kufanya biashara na mtu anayehisiwa kuwa chuma ulete. Kwenye mtaa ninaoishi kuna mzee mmoja akienda maduka ya hapa mtaani hawamuuzii kabisa. Ukiwauliza wanakwambia huyo mzee ni chuma ulete.
Kuna wafanyabiashara wengine wana imani kali sana kuhusu chuma ulete kiasi kwamba ukienda na fedha kubwa asubuhi inayohitaji kurudishiwa chenchi yuko radhi asikuuzie unachotaka. Wanaamini kwamba wanapokurudishia fedha asubuhi hiyo hasa kama ni mteja wa kwanza basi mauzo yote ya siku hiyo yatakwenda kwako. Hii imewahi kunitokea nilienda dukani asubuhi na shilingi elfu kumi kutaka mahitaji, muuzaji akaniambia hana chenchi, nikamwambia nipe mahitaji halafu chenchi nitafuata baadae, alichokifanya alipokea fedha yangu na kuiweka pembeni kabisa, hakuichanganya na fedha nyingine.
Tabia na imani hizi zimenifanya nifikiri sana juu ya hii CHUMA ULETE na kwa nini watu wanateseka kiasi hiki. Swali kubwa nililojiuliza ni je chuma ulete wapo? Kwa kuwa mimi naamini katika sayansi jibu la moja kwa moja lilikuja kwamba hakuna chuma ulete ila ni imani tu za watu. Na kama ilivyo kwenye kila imani, wanaoamini wanaona matokeo ya imani zao.
Baada ya kuja kufikiri kwa kina niligundua sikuwa sahihi kusema chuma ulete hayupo. Ukweli ni kwamba kwenye kila biashara CHUMA ULETE wapo/yupo na kwa bahati mbaya ni vigumu sana kumjua na kumzuia. Ugumu huu unatokana na ukweli kwamba chuma ulete wa biashara yako ni wewe mwenyewe. Unaweza kuhangaika sana kuzuia chuma ulete lakini hujui wewe mwenyewe ndio chuma ulete mkubwa wa biashara yako.
Mahesabu na matumizi yako mabovu ya fedha kwenye biashara ndio yanakufanya uwe chuma ulete wa biashara yako mwenyewe.
Unawezaje kumdhibiti chuma ulete huyu mbaya(wewe mwenyewe) kwenye biashara yako?
Uzuri ni kwamba unaweza kumdhibiti chuma ulete huyu ambae ni wewe mwenyewe kama utafuata misingi muhimu ya mipango na matumizi ya fedha za biashata. Hapa nitaeleza vitu vitano muhimu unavyotakiwa kuvifanya au kuacha kuvifanya ili kumdhibiti chuma ulete na biashara yako iweze kustawi.
1. Tenganisha matumizi ya biashara na matumizi yako binafsi.
Moja ya kosa kubwa linalofanywa na wafanyabiashara wengi na linawaletea upotevu wa hela kwenye biashara zao ni kuchanganya matumizi binafsi na matumizi ya biashara. Ni vigumu sana kuona faida na ukuaji wa biashara kama fedha ya matumizi yako binafsi inatoka moja kwa moja kwenye fedha ya biashara. Utaona unauza sana lakini fedha huzioni, hii ni kwa sababu chuma ulete wewe, unaendelea kutoa fedha za mauzo na kutumia kwenye matumizi yako binafsi. Ili uweze kuona ukuaji halisi wa biashara yako tenga fedha za biashara na fedha za matumizi binafsi.
2. Jilipe mshahara kutoka kwenye biashara yako.
Najua unajiuliza sasa nitaishijekama siwezi kuchanganya matumizi ya biashara na matumizi binafsi wakati biashara ndio shughuli inayoniingizia kipato cha kuendesha maisha. Ili uweze kuwa na mtemgano mzuri kati ya fedha ya matumizi binafsi na matumizi ya biashara jilipe mshahara. Unaweza kuamua kujilipa mshahara kwa siku, wiki, au mwezi. Baada ya kujilipa mshahara wako usiguse tena fedha ya biashara, hili linahitaji nidhamu ya kutosha. Njia nzuri ya kujipangia mshahara ni kujilipa kamisheni, yaani unajilipa asilimia fulani ya faida unayopata kwenye biashara. Utakapohitaji kupata mshahara mkubwa zaidi utasukumwa kufanya biashara zaidi ili upate faida kubwa na baadae kamisheni kubwa. Kama biashara unayofanya ndiyo unayotegemea kuendesha maisha yako ningependekeza ujilipe mshahara kwa wiki au mwezi, ukijilipa kwa siku unaweza usione tofauti ninayozungumzia hapa.
3. Jua tofauti ya mauzo na faida.
Hiki ni kitu rahisi sana kwenye biashara ila bado wafanyabiashara wengi wanashindwa kukifuata. Mauzo ni tofauti kabisa na faida kwenye biashara. Kwa mfano umenunua mfuko wa sukari kwa tsh elfu 40 na kuuza tsh elfu 60 umepata faida ya tsh elfu 20 si ndio? Sasa weka fedha ya kufikisha mfuko huo kwenye eneo la biashara, weka muda uliotumia kuuza mfuko huo, weka kodi ya eneo la biashara. Ukijumlisha vyote hivi unaweza kujikuta unabaki bila ya faida yoyote. Nachotaka ujifunze kwenye mfano huu ni kwamba unaweza kuona unauza fedha nyingi sana ila hupati faida kwa sababu hujapiga vizuri mahesabu yako. Badala ya kufikiri chuma ulete anakuchukulia hela hebu weka hesabu zako za biashara vizuri.
4. Epuka gharama zisizo za msingi kwenye biashara yako.
Sio kila kitu unachoona wafanya biashara wenzako wanafanya na wewe inabidi ufanye, hasa pale kitu hicho kinapokuwa ni gharama kwenye biashara yako. Tumia fedha kwenye matumizi ya msingi na baadae utaendelea kukua kidogo kidogo. Kama ndio unafungua ofisi yako mpya kuna vitu vingi unaweza kuepuka gharama kwa kufanya manunuzi yako vizuri. Vitu kama thamani, unaweza kununua zinazokidhi mahitaji yako na kwa bei ambayo ni nzuri kwako. Kama unaanza biashara mpya na unataka uwepo kwenye mtandao kuliko kwenda kutumia dola elfu moja kutengeneza tovuti nzuri na ya kisasa unaweza kuanza na tovuti ndogo ya dola mia moja, au hata ukaanza na blog ya bure. Baada ya hapo unaendelea kukua kidogo kidogo. Jambo la msingi ni kujaribu kupunguza matumizi yasiyo ya msingi ili uweze kuona ukuaji wa biashara yako.
5. Fanya mahesabu ya mara kwa mara kwenye biashara yako.
Hili ni tatizo la msingi na ndipo dhana nzima ya chuma ulete inapoanzia. Watu ni wavivu wa kukaa chini na kufanya mahesabu ya biashara zao. Wengine wanaamini kwa vile biashara wanasimamia wenyewe basi wanajua kila kitu hivyo hakuna haja ya kupiga hesabu moja moja kwa kila bidhaa aliyonunua na kuuza. Kama na wewe una mawazo haya unakosea sana na wewe ni chuma ulete mkubwa sana. Hata uwe makini kiasi gani ni lazima kuna sehemu utakosea au kupitiwa. Unapofanya mahesabu mara kwa mara kwenye biashara yako inakusaidia kujua ni wapi fedha zinapotelea na kudhibiti mianya hiyo. Pia inakujuza ni vitu gani vyenye faida kubwa na vipi ambavyo vina faida ndogo. Kwa kujua hilo utawekeza zaidi kwenye vitu vyenye faida kubwa ili kukuza biashara yako. Sheria ni hii, asilimia 80 ya faida kwenye biashara yako inatokana na asilimia 20 ya bidhaa au huduma unazouza. Jua asilimia hiyo 20 na uanze kutumia vizuri ili kupata faida kubwa.
Mafanikio kwenye biashara yanahitaji kujipanga na kujua ni kitu gani unafanya. Katika zama hizi za sayansi na teknolojia usipofanya biashara kwa mitindo ya kisasa utajikuta kila siku unapata hasara na kuanza kusingizia chuma ulete wanakuharibia biashara yako. Wewe mwenyewe ndio chuma ulete wa biashara yako, jua hilo na uanze kubadilika mara moja. Jifunze mambo mapya kila siku kuhusu biashara yako/zako ili uweze kuzikuza na kupata faida kubwa.
Nakutakia kila la kheri, TUKO PAMOJA.