Kutokana na ugumu wa ajira kwenye zama hizi watu wengi wanaona kujiajiri au kuwa mjasiriamali ndio njia mbadala ya kuyakomboa maisha yao. Hivyo kumekuwa na wimbi kubwa la watu kuondoka kwenye kazi na kwenda kujiajiri au kuanzisha biashara zao. Ni kitu kizuri sana kwa sababu angalau watu wanaweza kuwa na mamlaka na maisha yao na wanaeza wakaajiri na wengine pia. Ila kwa upande wa pili sio wote wanaokwenda njia hiyo wanafanikiwa kufikia malengo waliyojiwekea. Wengi sana wanashindwa na kujikuta wako kwenye mazingira magumu kuliko hata yale waliyokuwa nayo kwenye ajira.

Leo tutazungumzia mambo kumi unayotakiwa kuyajua au kuyafanya kabla hujaacha kazi na kuingia kwenye ujasiriamali au biashara. Sisemi mambo haya ili kukukatisha tamaa na uendelee kuwa mtumwa, ila nayasema ili kukupatia mwanga wa kule unakokwenda ili usije kushangazwa na mambo haya baadae. Mambo hayo kumi ni kama ifuatavyo;

1. Kujiajiri au ujasiriamali ni kugumu.

Kama unafikiri kujiajiri au kuingia kwenye ujasiriamali ndio nJia rahisi kwako kufanikiwa ni vyema ukabadili mawazo yako mara moja kabla hujaingia na ukashindwa vibaya. Zaidi ya nusu ya biashara zinazoanzishwa zinakufa ndani ya mwaka mmoja baada ya kuanzisha. Na hata zile zinazoendelea kudumu zinakuwa na hali ngumu sana na hazitengenezi faida kubwa. Hizi ni takwimu ambazo zinasikitisha sana ila ndio ukweli wenyewe.

Kujiajiri ni kugumu, ujasiriamali ni mgumu na biashara ni ngumu. Jua kabisa unaingia kwenye njia ambayo uwezekano wa kushundwa ni mkubwa hivyo mipango na kufanya kazi kwa bidii na maarifa ni muhimu sana.

2. Utafanya kazi kuliko ulivyokuwa umeajiriwa.

Unafikiri ukishajiajiri wewe ndio bosi mwenyewe unakaa nyuma ya meza kubwa yenye kiti cha kuzunguka huku ukiongea na simu au wageni na wateja waliokutembelea ofisini. Ndoto za mchana hizo. Unaweza kukaa kwenye kiti cha kuzunguka na meza kubwa ila utafanya kazi zaidi ya unavyofanya kwenye ajira. Unaweza kujikuta unafanya kazi masaa kumi na mbili ofisini na ukirudi nyumbani unaendelea tena na kazi kwa zaidi ya masaa mawili. Mwanzo wa biashara au ujasiriamali kuna misingi mingi unayotakiwa kuijenga na ni wewe pekee utakaefanya hivyo.

3. Utavaa kofia nyingi kwa wakati mmoja.

Kwenye ajira yako una jukumu moja tu au machache yaliyoelezwa. Labda unafanya kazi kwenye idara ya masoko, au idara ya uzalishaji au idara ya huduma kwa wateja na kadhalika. Unapojiajiri utajikuta unafanya kazi za kila idara katika biashara yako. Kuna wakati utavaa kofia ya kiongozi, wakati mwingine masoko, wakati mwingine huduma kwa wateja na kadhalika. Kuwa tayari kubadilika kutokana na hitaji la biashara yako kwa wakati husika.

4. Usichome madaraja.

Kuna dhana moja iliyokuwa ikitumika sana kipindi cha nyuma ambapo mtu alikuwa akiondoa uwezekano wowote wa kurudi nyuma. Kwa mfano kama wewe unataka kuacha kazi na kwenda kujiajiri basi unagombana na waajiri wako kiasi kwamba huwezi kurudi tena kwenye ulimwengu wa ajira, hii inakusababisha uhakikishe unafanya kila mbinu kufanikiwa kwani huna kimbilio jingine. Dhana hii ilifanya kazi sana zamani ila kwa sasa usijaribu kuitumia. Ondoka kwa amani na kama ikiwezekana mwambie muajiri wako unakwenda kufanya nini, mwajiri wako tayari ana mtandao mkubwa hivyo anaweza kukusaidia kupata wateja wa biadhaa au huduma uayokwenda kutoa. Nguvu ya mtandao ni kubwa sana kwenye ulimwengu wa sasa wa biashara na ujasiriamali.

5. Kuwa na uhakika wa kuishi angalau miezi sita mbeleni.

Usifikiri kienda kuanzisha biashara leo basi wiki ijayo mambo yataanza kuwa mazuri na utaweza kuendesha maisha yako kupitia biashara yako. Hicho hakiwezi kutokea, itakuchukua angalau miezi sita ndio uanze kupata faida ya uhakika kutoka kwenye biashara. Hivyo kabla ya kuacha kazi na kuingia njia hii hakikisha una uwezo wa kuishi angalau miezi sita. Namaanisha kama matumizi yako ni laki tano kwa mwezi basi uwe na fedha itakayokutosha kwa matumizi ya miezi sita ya mbele. Hii itakuwezesha kuondoa hofu ya fedha na kuweza kuwekeza nguvu zako kwenye kukuza biashara yako.

6. Itakuchukua muda kufanya biashara isimame yenyewe.

Kujiajiri sio njia ya kutajirika haraka, sahau kabisa hicho kitu. Itakuchukua muda kujenga biashara mpaka isimame na kuweza kujiendesha mwenyewe. Katika muda huo kuna kushindwa, kukatishwa tamaa na hata kukosa mwelekeo. Ni uvumilivu wako, ubunifu, malengo na kufanya kazi kwa bidii kutakuwezesha kushinda safari hii ngumu.

7. Kuwa na matumizi mazuri ya fedha.

Unapokuwa umeajiriwa una uhakika wa kukinga mshahara mwisho wa mwezi na una huduma nyingine kama za bima hivyo una uwezo wa kupata matibabu muda wowote wewe au mwanafamilia wako anapougua. Unapokwenda kujiajiri mambo yanabadilika haraka sana, kwanza uhakika wa kipato haupo na pili kuna baadhi ya huduma unazonufaika nazo kwenye ajira utazikosa, kama bima ya afya. Ni vizuri ukaanza kujifunza kuwa na matumizi mazuri ya fedha na kuweka akiba ili mambo yasijekuwa magumu kwako baadae.

8. Kuwa na matumizi mazuri ya muda.

Muda ndio kila kitu. Wakati umeajiriwa unaweza usione sana thamani ya muda kwa sababu muda hauna madhara makubwa kwenye kipato chako. Ufanye kazi sana au ufanye kawaida mshahara ni ule ule. Kwenye kujiajiri muda wako ndio kila kitu, jinsi unavyoweza kuupangilia vizuri ndivyo unavyoweza kuwa na uzalishaji mkubwa na ndivyo unavyoweza kukuza biashara yako na kupata faida kubwa zaidi. Anza kujifunza nidhamu ya muda.

9. Bobea kwenye mambo machache.

Kama huna wazo moja au machahe ni nini unakwenda kufanya kwenye kujiajiri uko kwenye njia mbaya. Huwezi kufanya kila kitu na hata ukijaribu kufanya hivyo utashindwa vibaya sana. Chagua vitu vichache utakavyofanya kisha wekeza muda wako na nguvu zako baada ya muda utaona majibu mazuri.

10. Jifunze kusema hapana.

Kwa kuwa unakwenda kujiajiri haimaanishi unakuwa tayari kukubaliana na kila wazo la biashara unalopewa au kila maoni unayopewa na watu wengine au wateja. Anza kujifunza kusema hapana kwa sababu kila unaposema ndio kuna kitu fulani itabidi ukiweke kwenye hapana. Kama utakuwa unasema ndio kila siku utajikuta hujui hata unafanya nini na muda mfupi mambo yatakushinda.

Haya ni baadhi ya mambo kumi muhimu unayotakiwa kuyajua kabla hujaacha kazi na kwenda kujiajri. Jambo kubwa zaidi ni kujua kile unachokwenda kukifanyia kazi, kujua soko na kuweka mipango yote muhimu kabla ya kuanza.

Pamoja na haya yote usikate tamaa, kama umedhamiria kweli unaweza kufanya mambo makubwa hata kama huna baadhi ya hayo niliyoandika hapo juu. Kuna wengi sana wametoboza huku wakiwa hawana hata nusu ya hayo hapo juu, kufanya kazi kwa bidii na maarifa, uvumilivu na kutokata tamaa ni muhimu sana kila mahali. Kumbuka hata ujiandae vipi changamoto huwa hazikosekani. Hivyo kama umedhamiria kuwa bosi wako mwenyewe weka mikakati na anza kufanya kazi.

Nakutakia kila la kheri kwenye harakati zako za maisha.

Kumbuka TUKO PAMOJA.