Habari za leo msomaji wa KISIMA CHA MAARIFA, natumaini wewe ni mzima wa afya na unaendelea vizuri na mpango huu wa kutengeneza tabia za mafanikio. Mpaka sasa utakuwa umeshaanza kuwa na utaratibu wa kujisomea kama umefuatilia makala hizi kwa umakini.

Leo tutazungumzia mambo muhimu ya kuzingatia ili uweze kujenga tabia imara ya kujisomea. Mpaka sasa unajua ya kwamba kujisomea ni kitu muhimu sana kwenye maisha yako. Kwa kuwa na tabia ya kujisomea tu na kutumia yale uliyojifunza unaweza kuongeza kipato chako mara mbili ya unavyopata sasa.

Kama ilivyo kwenye kujenga tabia yoyote ile, tabia ya kujisomea utaijenga kwa kufanya na kurudia mpaka iwe sehemu ya maisha yako. Ili kuweza kuimarisha tabia hii ni vyema kufanya yafuatayo;

1. Jisomee kila siku.

Isipite siku bila ya kujisomea kitabu kizuri ambacho utajifunza. Weka utaratibu kwamba kila siku lazima usome angalau nusu saa ndio siku yako iwe imekamilika. Katika masaa 24 huwezi kukosa nusu saa ya kujisomea. Jitahidi sana uwe kitu cha kwanza unachofanya kila unapoamka asubuhi ni kusoma, wakati huu ni mzuri sana kwako kuelewa na unakuwa na utulivu wa hali ya juu.

2. Kuwa na kitabu popote ulipo.

Popote pale unapokuwa hakikisha umebeba kitabu, au unaweza kusikiliza kitabu. Kila siku kuna muda tunaopoteza kwa kusubiri huduma fulani au watu fulani. Badala ya kupoteza muda huo kushangaa shangaa unaweza kutoa kitabu chako na kuanza kusoma au kusikiliza. Kwa njia hii utajikuta unaweza kusoma vitabu vingi sana na kujifunza mengi.

3. Rudia vile ulivyosoma.

Kusoma ni hatua moja, kurudia kile ulichokisoma ni hatua nyingine muhimu zaidi. Unaposoma au kusikiliza kitabu kwa mara ya kwanza kuna vitu vingi sana unashindwa kuvipata. Ila unaporudia kwa mara nyingine utaona unajifunza vitu vingi zaidi. Hivyo ni vizuri sana ukawa na utaratibu wa kurudia kusoma vitabu ulivyokwishasoma baada ya muda fulani. Hii itakusaidia kujifunza na kukumbuka zaidi.

4. Weka malengo ya kiasi cha kujisomea.

Japokuwa unajenga tabia ya kujisomea kila siku bado hiyo haitoshi kukuwezesha kusoma na kujifunza mengi. Unaweza kuwa unaisomea kila siku ila unasoma ukurasa mmoja tu. Ili kuhakikisha unapata majibu mazuri kutokana na tabia hii ya kujisomea ni lazima uweze kujua ni kiwango gani unajisomea. Weka malengo ya idadi ya vitabu utakavyosoma kwa muda fulani.

Kwa mfano kwa sasa weka lengo la kusoma kitabu kimoja kwa wiki na ukishafanikiwa sana unaweza kuwa unasoma kitabu kimoja kwa siku. Unashangaa, watu wengi sana waliofanikiwa wamefikia hatua ya kuweza kusoma kitabu kimoja kwa siku, usihofu hata wewe utafikia hatua hiyo ila kama utaanza kufanya hiki ninachokwambia. Nilitoa utaratibu mzuri wa kuweza kusoma kitabu kimoja kwa wiki kwenye makala iliyopita. Ukisoma vitabu 50 kwa mwaka kwa utaratibu huu utakuwa mbali sana.

5. Tumia yale unayojisomea kwenye maisha yako.

Hata ungesoma vitabu 1000 kama hutachukua hatua maisha yako yatabaki vile yalivyo. Ni lazima uwe makini sana na  utumie yale unayojifunza kwenye maisha yako. Kama umejifunza jinsi ya kutunza muda anza kutumia yale uliyojifunza kwenye maisha yako na uache kupoteza muda. Kama umejifunza jinsi ya kuweka akiba na kuwa na matumizi mazuri ya fedha anza kutumia hayo unayojifunza. Hii ndio njia pekee ambapo vitabu vitakuwa na msaada kwenye maisha yako.

Kama unasoma halafu huvitumii ni sawa na kujifunza kuogelea wakati huna mpango wa kwenda mtoni, ziwani au baharini. Ni lazima utasahau na unapoteza muda wako. Kuwa makini sana na tendo la kujisomea na kujifunza.

Zingatia mambo hayo matano kila siku na utaona jinsi gani tabia hii ya kujisomea itakavyobvadili maisha yako kwa kiasi kikubwa. Nimeweza kufanya mambo mengi sana yenye manufaa kwenye maisha yangu na kwa wanaonizunguka kutokana na tabia hii ya kujisomea. Nina uhakika na kwako pia itatokea kama utafuata hayo niliyokushauri. Najua ni magumu kufuata ila hiyo ndiyo gharama unayotakiwa kulipa ili uweze kufikia mafanikio makubwa. Ukiona unapata mawazo ya kujishawishi kutofanya hayo jua kabisa wewe sio mmoja wa watu watakaofanikiwa sana, mafanikio sio lele mama, yanahitaji kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Maarifa yenyewe ndio hayo unayoyapata kwa kujisomea.

ZOEZI LA WIKI.

Hii ndio wiki ya mwisho ya kujijengea tabia ya kujisomea. Najua tatizo letu kubwa lipo kwenye muda, hata kujisomea unaweza kujiaminisha kwamba unakosa muda wa kutosha kufanya hivyo. Mimi napinga sana hilo swala la kwamba huna muda wa kutosha kuweza kuongoza tabia ya kujisomea. Naamini huna matumizi mazuri ya muda wako. Moja ya sababu za kukosa muda ni tabia ya kuahirisha mambo.

Leo nakutumia tena kitabu cha EAT THAT FROG kilichoandikwa na Brian Tracy. Kitabu hiki niliwahi kukituma tena kwa wasomaji wa AMKA MTANZANIA. ni kitabu kizuri kitakachokuwezesha kuondokana na tabia ya kuahirisha mambo.

Kisome na anza kutumia yale unayojifunza mara moja, ni kitabu kifupi sana. Kama utaacha kuahirisha kama kitabu hiki kinavyofundisha unaweza kukimaliza kusoma ndani ya siku moja. Kupata kitabu hiko bonyeza hayo maandishi ya jina la kitabu.

Asante sana kwa kuendelea kuwa mwanachama na msomaji mzuri wa KISIMA CHA MAARIFA. Naamini utafikia mafanikio makubwa sana kama utaweka juhudi na maarifa kwenye jambo lolote unalofanya.

Nakutakia kila la kheri,

TUKO PAMOJA.