Fedha ni moja ya vitu muhimu sana kwenye maisha yetu. Fedha ina mchango mkubwa sana katika maendeleo na hata furaha kwenye maisha. Pamoja na umuhimu huu wa fedha bado jamii ina mtazamo hasi sana juu ya fedha.

Mtizamo huu hasi umekuwa unapandikizwa kila siku na hivyo umefikia hatua ya kuamini. Kwa kuamini mtizamo huu kimekuwa kikwazo kikubwa kwako kuweza kufikia kuwa na uhuru wa kifedha.

Leo nataka tuangalia kauli tatu ambazo zimetawala sana mawazo yetu na ambazo zinatuzuia kuwa na uhuru wa kifedha. Unaweza kuona kauli hizi ni kitu cha kawaida ila zina matokeo hasi sana kwako na ndio zinakurudisha nyuma kila siku.

Hizi ndizo kauli tatu kuhusu fedha ambazo zinakurudisha nyuma.

1. Fedha haileti furaha.

Hii ndio kauli maarufu kuliko zote kuhusu fedha. Kila mtu utamsikia akisema kauli hii kwamba fedha haileti furaha au fedha haiwezi kununua furaha. Naweza kukubaliana na wewe ila naomba unijibu swali hili, Je umasikini unaleta furaha? Unaweza kuona ni jinsi gani tunajiaminisha kwamba fedha haileti furaha wakati hata umasikini nao hauleti furaha. Tena ni afadhali ukawa huna furaha ila hela ikawepo kuliko ukawa huna furaha halafu hela nayo ni tatizo. Fedha ina mchango mkubwa sana katika furaha, unapokuwa na uhakika wa kula, kupata malazi mazuri, kupata huduma bora za afya unaweza kuwa na furaha kuliko anayekosa vitu hivyo.

2. Maisha ni mafupi.

Nakubaliana kabisa na kauli hii kwamba maisha ni mafupi, ila nakataa inavyotumika kwenye jamii. Watu wote wanaopenda kutumia kauli hii huitumia kama kisingizio cha kutokujipanga kwa ajili ya baadae. Kwa kujiaminisha kwamba maisha ni mafupi wanaona hakuna haja ya kuweka mipango mokubwa ya baadae, hakuna haja ya kuweka akiba na hata kuwekeza kwa ajili ya maisha ya baadae, mwishowe maisha yanakuwa magumu. Maisha ni mafupi kama ukiwa na fedha ya uhakika, ila ukiwa na za kuunga unga utayaona maisha ni marefu sana na ya mateso.

3. Nakula ujana.

Kwa vijana hii ni moja ya kauli inayowapoteza sana. Cha kusikitisha siku hizi nasikia mpaka ikiimbwa kwenye nyimbo, yaani msanii ambaye anaaminika ni kioo cha jamii anawahamasisha vijana wenzake wale ujana. Na kutokana na ushawishi wake mkubwa kuna kundi kubwa sana la vijana ambalo linafuata ushauri huo. Unawezakukataa na kusema ni wimbo tu au ni kauli tu, ila utakapoangalia matendo yako au ya wenzako utaamini kabisa kuna wakati unafanya mambo yasiyo na msaada kwako kwa sababu tu unaamini unakula ujana. Kwa kauli hii unaendekeza starehe ukiamini kwamba ujana ukiisha utajipanga, kwa bahati mbaya hakuna mtu atakuja kukuambia kwamba hapa ndio mwisho wa ujana(sahau kuhusu miaka 35), unakuwa umeshajijengea tabia ya kizembe, majukumu yanakuwa mengi na unaanza kujuta.

Kauli hizi tatu na nyingine nyingi zimekuwa kikwazo cha watu wengi kuwa na uhuru wa kifedha. Tunaendelea kuteseka na fedha kila siku kwa sababu akili zetu zina mtizamo tofauti kabisa kuhusu fedha.

Huwezi kutengeneza uhuru wa kifedha bila ya kuondoa mtizamo huu hasi kwenye kichwa chako na pia huwezi kuondoa msimamo huu hasi kwa mara moja tu. Hii ni tabia ambayo umeijenga kwa miaka mingi na hivyo unahitaji muda mrefu kuibadili.

Kama unataka kubadili tabia ya kushindwa kuwa na uhuru wa kifedha nakukaribisha kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Kwenye KISIMA CHA MAARIFA mwezi wa saba na wa nane tunajadili jinsi ya kujenga tabia ya kuweza kutunza na kuongeza fedha zako ili kuwa na uhuru wa kifedha. Kama bado hujajiunga na kisima cha maarifa jiunge sasa ili uweze kupata mambo haya mazuri sana ya kuboresha maisha yako.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA jiunge mapema kabla ya mwezi huu kuisha. Kujiunga tuma fedha tsh elfu kumi(10,000/=) kwa mpesa 0755953887 au tigo pesa 0717396253 kisha utume email yako(email ya GMAIL ni bora zaidi) na utaunganishwa.

Mwisho wa kujiunga ni leo jumatatu, fanya hima usipoteze nafasi hii muhimu kwenye maisha yako.

Nakutakia kila la kheri kwenye safari ya kuboresha maisha yako.

TUKO PAMOJA.

kitabu-kava-tangazo4