USHAURI; Kuanzisha Asasi Zisizo Za Kiserikali(NGO) Kama Njia Ya Kutengeneza Kipato.

Kutokana na tatizo la ajira na maisha kuwa magumu watu wengi wanalazimika kutafuta njia mbadala za kutengeneza kipato. Katika njia hizo mbadala za kuongeza kipato watu wanafikiri kujiajiri, kufanya biashara na hata kufanya kazi za ziada. Kuna njia nyingi sana za kuweza kuongeza kipato.

KUKUA

Mojawapo ya njia mbadala za kuongeza kipato ambazo watu wanafikiria ni kuanzisha asasi zisizo za kiserikali(NGO). Je hii nayo ni njia nzuri ya kutengeneza kipato na kuweza kujikomboa kutoka kwenye umasikini? Watu wengi wamekuwa wakiulizia sana hili na nimeona ni vyema tukashirikishana hapa. Kabla hatujaanza kujadili hili naomba nikushirikishe baadhi ya maswali ya wasomaji kuhusu hili la NGO;

“Mimi nawaza kuanzisha ngo, niwe naandika proposal nakuomba funds, but najiuliza wat if nitakosa funds how will i manage my ngo.
Na je how do u see this idea and Its sustainability”.

Samahani kwa uchanganyaji wa lugha uliotumika na muulizaji, naamini umeelewa anachozungumzia ni nini.

Kwa upande wangu siwezi kumshauri mtu kuanzisha NGO kama sehemu ya kutengeneza kipato. Kama alivyosema msomaji mwenzetu hapo juu ni kwamba unapoanzisha NGO sehemu kubwa ya fedha ya kuiendesha utakuwa unategemea wafadhili.  Na kama unategemea wafadhili au mtu mwingine yeyote ndio atoe fedha nafikiri inaeleweka wazi kwamba ni vigumu sana kuweza kufikia malengo unayotarajia.

Pia unapompa mtu nafasi ya kuwa mtoaji wa fedha kwenye asasi yako unampa pia nguvu ya kufanya maamuzi. Hivyo unaweza kujikuta unafanya mambo ambayo hupendelei kufanya kwa sababu tu anayekufadhili anataka ufanye hivyo.

Asasi hizi sio sehemu ya kutengeneza faida, hivyo ni vigumu sana kusema utaweza kupata kipato cha uhakika kupitia NGO. Labda kama utatumia njia zisizo halali za kujipatia kipato kutoka kwenye NGO kitu ambacho nakushauri sana usifanye, hakItakusaidia hata kidogo.

Nafikiri wakati mzuri wa kuanzisha NGO ni baada ya kuwa na kitu ambacho uko tayari kukitoa kwa jamii bila ya kutegemea malipo yoyote. Kwa njia hii tunaiondoa NGO kama njia mbadala ya kutengeneza kipato ili kuboresha maisha yako binafsi.

Badala ya vijana kujiunga na kuanzisha NGO nashauri wajiunge kufungua biashara au hata kufanya kilimo. Kama vijana wachache wenye malengo na maono sawa wanaweza kukaa chini na kuweka mipango mizuri ya kibiashara hakuna kitakachoweza kuwazuia kuongeza kipato na kuwa na maisha bora.

Tatizo letu kubwa hatupendi kufikiria na tunatafuta sana njia za mkato za kutengeneza kipato.

Na wewe unatafuta njia ya mkato ya kufikia mafanikio? Kwa muda mrefu nimekuwa nikitafuta njia ya mkato ya kuweza kufikia mafanikio na nimeweza kupata njia hii moja(bonyeza hapo kusoma).

Kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ndio njia pekee inayoweza kukuletea mafanikio ya uhakika. Japokuwa kwenye NGO utafanya kazi kwa juhudi na maarifa, ni vigumu sana kuitegemea moja kwa moja kujitengenezea kipato. Hii ni kwa sababu unategemea fedha kutoka kwa wafadhili na huwezi kufanya shughuli ya kukuingizia faida kwa kutumia NGO.

Mimi ni mmoja wa watu ambao siamini kabisa katika msaada ili kuendelea, hasa msaada wa kifedha. Ingelikuwa msaada wa fedha unasaidia maendeleo, nchi za kiafrika zingekuwa mbali sana kimaendeleo. Ila haziwezi kufikia maendeleo makubwa kwa sababu kila msaada unakuja na masharti yake na watoa misaada kuna kitu wanataka kunufaika nacho, hawatoi bure tu. Hivyo ndivyo itakavyotokea pia utakapoanzisha NGO na kutegemea fedha za wafadhili kwa asilimia 100.

Fikiria kuanzisha biashara ambayo itakupatia uhuru wa maisha na kifedha na sio asasi ambayo itakufanya uendelee kuwa tegemezi.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio.

TUKO PAMOJA.

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa kwa email amakirita@gmail.com au simu 0717396253/0755953887.

kitabu kava tangazo

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s