Wiki hii nilikuwa nasoma kitabu kimoja nilichotumiwa na mmoja wa wasomaji wazuri wa AMKA MTANZANIA. Pamoja na vitu vingi ambavyo nimekuwa nikijifunza kwenye vitabu vingi ninavyosoma, kitabu hiki nimejifunza mambo muhimu sana ili kuweza kufikia mafanikio.
Nitawashirikisha wasomaji wote wa AMKA MTANZANIA kitabu hiki wiki ijayo, hivyo kama tayari wewe ni mwanachama utatumiwa kitabu hiki, kama bado hujawa mwanachama jiunge kwa kubonyeza maandishi haya na kuweka email yako.
Pamoja na mengi niliyojifunza kwenye kitabu hiki kuna hadithi moja fupi nimeipenda sana ambayo nataka nikushirikishe hapa ili ujifunze jambo moja muhimu sana kufikia mafanikio.
Sylvester Stallone wengi tunamfahamu kama RAMBO, alizaliwa kwenye maisha ya kimasikini sana. Mama yake alimzalia kwenye ngazi za shuleni. Alikulia kwenye umasikini mkubwa na alikuwa na matatizo ya kuweza kuongea vizuri.
Pamoja na haya yote ndoto yake kubwa ilikuwa kuwa muigizaji mkubwa. Alihangaika sana kupata nafasi ya kuigiza lakini hakuna mtu yeyote aliyetaka kumpa nafasi hiyo. Kila siku alikuwa akikaa mbele ya waongozaji wa filamu mpaka siku moja alipopewa nafasi ya kucheza sehemu ndogo sana ya filamu, na baada ya hapo hakuna mtu aliyetaka kumpa tena nafasi.
Siku moja alikuwa amepigika sana mpaka akafikia kumuuza mbwa wake kwa dola 50, kitu ambacho kilimuuma sana. Baada ya hapo aliandika hadithi ya filamu(script), pamoja na kuizungusha kwa watu wengi wote waliikataa. Hakukata tamaa aliendelea kuzunguka na hadithi yake mpaka alipopata muongozaji mmoja aliyekubali kuinunua. Aliahidi kumlipa dola elfu sabini na tano($75,000) ila kwa sharti moja kwamba sehemu ambayo angecheza Rambo ya mhusika mkuu acheze mtu mwingine. Rambo alikataa ofa hiyo. Wakaongeza dau mpaka dola laki mbili na elfu ishirini na tano($225,000) na baadae wakaongeza mpaka dola milioni moja($1,000,000) kwa sharti kwamba Rambo asiwe mhusika mkuu. Bado alikataa ofa ile.
Baadae walikubali kununua hadithi ile kwa $35,000 na Rambo acheze kama mhusika mkuu. Baada ya hapo kilichotokea ni historia. Filamu hiyo iliuzwa kwa zaidi dola milioni mia moja sabini na moja($171,000,000) ikashinda tuzo kumi na Rambo kuwa muigizaji bora wa mwaka. Filamu hii moja alianza safari kubwa ya mafanikio ya Rambo.
Je kama Rambo angekubali kupokea dola milioni moja(karibu takribani bilioni mbili za kitanzania) angekuwa wapi leo?
Ni dhahiri kwamba Rambo alikuwa na hasira kubwa ya kufikia mafanikio ndio maana hakuna chochote kilichomteteresha na kumuondoa kwenye lengo lake la kufikia mafanikio makubwa.
Je wewe una hasira kiasi gani ya kufikia ndoto yako? Simaanishi hasira ya kupiga watu au kufanya uhalifu, bali ya kutokubali kuondoka kwenye mstari wa kuelekea kwenye mafanikio.
Inawezekana wengi wetu hatufikii malengo makubwa tunayojiwekea maishani kwa sababu tunafumbwa macho na vitu vinavyopita mbele yetu kama fedha na vingine.
Amini kwamba siku moja ndoto yako kubwa unayoota itatimia, ila tu kama utafanya kazi kuelekea kwenye ndoto yako hiyo.
Hakikisha hukosi kitabu hiki kizuri kwa kujiunga na mtandao huu wa AMKA MTANZANIA.
Nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya kufikia ndoto yako kubwa.
Wako katika mafanikio,
TUKO PAMOJA.