Ili kuweza kufikia uhuru wa kifedha ni muhimu sana kujua tupo kwenye hali gani kwa sasa. Kama ilivyo kwenye tatizo lolote huwezi kulitatua kama hujajua tatizo liko wapi na chanzo cha tatizo ni nini. Hivyo kwenye matatizo yako ya fedha ni muhimu sana kujua hali yako ya kifedha kwa sasa. Kuna mambo mawili muhimu unayotakiwa kujua kuhusu fedha zako binafsi;

1. Zinatoka wapi na ni kiasi gani?

2. Zinakwenda wapi na ni kiasi gani?

Unaweza kuona ni maswali rahisi sana na huenda ukayapuuza ila ndio chanzo kikuu cha matatizo yako ya fedha unayopitia sasa. Yachukulie haya maswali kwa uzito wa hali ya juu sana ili uweze kubadili hali na mtizamo wako wa kifedha.

Wakati wa kufanya zoezi hili nitakuomba uwe na kalamu na kitabu kidogo ambacho utaweka kumbukumbu zako zote za kifedha. Najua unafikiria ya kwamba unaweza kukumbuka tu kichwani kwako ila nakushauri usiamini sana kumbukumbu zako, mambo uliyoandika yanakuwa na uzito zaidi ya yale uliyofikiria tu.

Fedha zako zinatoka wapi na ni kiasi gani?
Tuanze na jambo la msingi kabisa ambalo ni vyanzo vyako vya mapato. Kwenye upande mmoja wa kitabu chako andika vyanzo vyako vyote vya mapato na kiasi unachopata kwenye kila chanzo. Kumbuka katika mwezi mmoja au hata wiki moja iliyopita ni kiasi gani cha fedha ulichopata na kilitoka wapi?

Kama ni mshahara andika, kama ni faida kutoka kwenye biashara andika, kama ni msaada au zawadi andika, kama ni kipato kutoka kwenye uwekezaji andika, kama ni rushwa au wizi andika(ndio andika na hii, hakuna atakayesoma ila itakusaidia sana wewe maka unataka kujikomboa kifedha). Usiache chanzo chochote ambacho umewahi kupata fedha ndani ya mwezi mmoja uliopita.

Kama umesahau vyanzo vyote vya fedha andika vile unavyokumbuka ila kwanzia leo utakuwa unaandika kila fedha unayopokea kiasi na imetoka wapi.

Usijaribu kujidanganya kwenye hatua hii, andika ukweli ambao unaujua wewe ili uweze kujua ni wapi unaanzia kubadili tabia na mtazamo wako kuhusu fedha.

Fedha zako zinakwenda wapi na kiasi gani?

Hii ndio sehemu muhimu zaidi kuhusu fedha zako, maana hapa ndio wengi tunapomtafuta mchawi au chuma ulete kwa kutojua tumepeleka wapi fedha zetu.

Kwenye kitabu chako ulichonunua maalumu kwa ajili ya zoezi hili la kujua fedha zako zinatoka wapi na zinakwenda wapi, upande mwingine andika fedha zinakwenda wapi.

Andika matumizi yako yote uliyofanya kwa mwezi uliopita au kama hukumbuki mwezi basi andika hata kwa wiki chache zilizopita. Naposema andika matumizi yako yote, namaanisha yote, usiache hata shilingi mia uliyotumia. Andia fedha ulizotumia kwenye matumizi ya msingi, kwenye starehe, kwenye kuhonga au kutoa rushwa, kwenye matibabu na matumizi mengine yote. Hata kama ulipoteza fedha kwa kuibiwa, kutapeliwa au kwa njia nyingine yoyote andika hapo.

Wakati huu unaandika usijaribu kujidanganya mwenyewe, andika kila kitu kinachohusu matumizi ya fedha zako. Pia usijaribu kuacha kuandika kitu kwa kufikiri kwamba umeamua kuachana nacho, nafasi kubwa ni kwamba huwezi kukiacha kwa urahisi hivyo.

Leo nimeona tufanye zoezi hili kwa sababu watu wengi hatujui ni kiasi gani cha fedha tunapata kwa ujumla, wengi wanajua tu mshahara wanaopata au faida kidogo wanayopata. Na pia wengi hatujua ni kiasi gani cha fedha tunachotumia, wengi tunatoa tu fedha bila ya kujua zinakwenda wapi. Mwisho wa siku tunajikuta fedha tuliyopata imekwisha yote na bado haijatosheleza mahitaji yetu ndio sasa mtu unaanza kuingia kwenye madeni. Na ukishaingia kwenye madeni unajikuta ni vigumu sana kuondoka kwa sababu bado hujajua tabia zako za kifedha zinatokana na nini. Hivyo unaendelea kukopa na kutumia kwenye matumizi ambayo huyajui sawa sawa. Maisha yako yanahama kutoka kuishi kwa mipango na  furaha na badala yake unaanza kuishi kwa kulipa madeni.

Maisha ya kulipa madeni sio maisha ambayo wewe unastahili kuishi, una uwezo mkubwa sana zaidi ya hapo, anza na zoezi hili ili kujua fedha zako zinatoka wapi na zinakwenda wapi ili uweze kujua ni hatua gani ya kuchukua kukabiliana na tatizo hili.

ZOEZI LA WIKI.

Katika zoezi la wiki huwa napendelea kutoa kitabu ambacho utaendelea kujifunza zaidi kuhusu somo husika. Ila wiki hii sitatoa kitabu kwa sababu kuna zoezi kubwa sana nataka ulifanye kila siku, nakuomba sana ulifanye kila siku kwa sababu hii ndio njia yako ya kwanza kwenye ukombozi wa kifedha. Naomba kila siku uandike kiasi cha fedha ulichopayta kwa njia yoyote ile kwenye kitabu chako ulichonunua kwa ajili ya zoezi hili. Baada ya kuandika ulichopata andika pia kiasi ulichotumia kwa siku nzima, kama una familia andika kiasi ambacho familia imetumia kutoka kwenye mapato yako wewe. Fanya hivi kila siku kwa kuanza leo na usiache kufanya hivi hata siku moja. Utafanya hivi kwa muda mrefu, ila kwa wiki hii ya kwanza usijaribu kufanya marekebisho yoyote, endelea na maisha yako kama kawaida ila kila siku andika hela uliyopokea na hela uliyotoa.

Zoezi hili litakuchukua muda mfupi sana, unaweza kuwa na kitabu chako karibu na ukawa unaandika kila unapotoa au kupokea fedha au unaweza kutenga dakika kumi kabla ya kulala au kumaliza siku yako na ukaandika choni mzunguko wako wa hela kwa siku nzima.

Fanya hivi halafu wiki ijayo tutaangalia jinsi ya kubadili mzunguko huo wa fedha.

Nakutakia kila la kheri katika harakati zako za kufikia uhuru wa kifedha.

TUKO PAMOJA.