Kuna changamoto nyingi sana zinazokabili biashara nyingi za Tanzania. Moja ya changamoto kubwa ni ukosefu wa rasilimali watu yenye uwezo na ujuzi wa biashara husika. Kila biashara inahitaji usimamizi mzuri, inahitaji uendeshaji bora, inahitaji huduma bora kwa wateja na pia inahitaji mbinu mpya za ubunifu ili iweze kuendelea na kukua.

Biashara nyingi za Kitanzania zinakosa vitu hivyo kutokana na kukosa watu wenye uwezo mzuri na wenye kupenda kazi waliyopewa wafanya. Hii imekuwa changamoto kubwa na imezuia biashara nyingi kukua.

Kabla hatujajadili nini cha kufanya ili kuondokana na changamoto hii tuangalie moja ya maoni ya msomaji mwenzetu wa AMKA MTANZANIA aliyetuandikia kuhusuana na changamoto hii.

Changamoto yangu kubwa ni kukosa wasaidizi wenye uzoefu au taaluma kwenye biashara yangu na hiyo imenifanya kutokufikia malengo yangu makubwa niliyojiwekea. biashara ninayo ifanya ni duka la vifaa vya ujenzi. Ambalo analisimamia mke wangu na vijana wa kazi. Na mimi najishughulisha na biashara ya mbao katika nchi ya malawi, naomba ushauri wenu.

Hii ni changamoto kubwa sana kwa wafanyabiashara walio wengi. Na pia imekuwa kikwazo kikubwa kwa biashara nyingi kuweza kukua na kufikia mafanikio makubwa.

urbanity8

Unawezaje kukabiliana na changamoto hii?

Kama zilivyo changamoto nyingine, changamoto hii ina njia nyingi sana unazoweza kutumia kukabiliana nayo na hatimaye kuweza kuipunguza kwa kiasi kikubwa sana au kuiondoa kabisa. Hapa nitazungumzia mambo matano muhimu ya kufanya ili kukabiliana na changamoto hii.

1. Wajue vizuri watu unaowaajiri.

Wafanyabiashara wengi tunachukua zoezi la kuajiri kama kitu rahisi sana, yaani anakuja mtu kuomba ajira na wewe unampa kwa sababu unahitaji mtu wa kufanya kazi. Au wakati mwingine unasema kabisa nitafutie kijana yeyote anayeweza kukaa kwenye biashara yangu. Hili ni kosa kubwa sana unalofanya kwenye biashara yako. Mjue vizuri mtu unayemuajiri, fanya nae usaili ana kwa ana na muulize maswali mengi zaidi ya yanayohusiana na nafasi unayotaka kumuajiri. Pia fuatilia kwa watu wanaomfahamu historia yake kwa sababu mambo mengine anaweza asikwambie ukweli. Ni muhimu ujue kama ana ndoto zozote kubwa kwenye maisha yake, anajiona wapi miaka fulani ijayo, anategemea kupata nini kutoka kwenye kazi utakayompa na pia anategemea kutoa nini kwenye kazi hiyo. Tunafikiri kazi ya usaili ni kwa makampuni makubwa tu ila ni kazi ya kila anayetaka kuajiri msaidizi, hata kama angekuwa ni wa kazi za ndani.

Hata kama unaajiri mtu wa kufanya usafi kwenye biashara yako ni muhimu sana kumjiua na kujua kama anapendelea kufanya kazi hiyo kwa sababu kama hatakuwa na mapenzi mazuri na kazi hiyo anaweza kuwa mtu wa kwanza kufukuza wateja.

2. Wekeza kwenye kuajiri.

Hili nalo ni kosa linalofanywa na wengi sana, tunatafuta sana wafanyakazi wa bei rahisi. Kuna kauli moja inasema rahisi ni ghali (cheap is expensive), kama unategemea kupata wafanyakazi wa bei rahisi sana jua hilo litaathiri ukuaji wa biashara yako. Kama unategemea kupata faida ya laki mbili kwa siku na wewe umeajiri wafanyakazi wawili ambao unawalipa laki moja kwa mwezi unaweza tu kusahau kuhusu kufikia lengo lako. Haya mambo hayaendi kwa bahati, jinsi ambavyo unawekeza ndivyo jinsi ambavyo unavuna.

Tatizo kubwa wafanyabiashara wanafikiri ili kupata faida kubwa basi ni lazima uwe na wafanyakazi unaowalipa mshahara kidogo. Jinsi malipo yako yanavyokuwa kidogo ndivyo ukuaji wa biashara yako unavyozidi kuwa kidogo kwa sababu utaajiri watu ambao hawana uwezo mkubwa na hata wakiwa na uwezo hakuna kitakachowasukuma kufanya kazi kwa bidii na maarifa.

3. Toa elimu ya biashara kwa wafanyakazi wako.

Kuajiri ni hatua moja, kumweka mfanyakazi aweze kuzalisha kwa hali ya juu ni jambo jingine ambalo ni muhimu zaidi. Mara kwa mara toa elimu ya biashara kwa wafanyakazi wako, na elimu hii sio unaitoa wewe mwenyewe bali unatafuta mwalimu au mshauri wa biashara anakuja kukaa na wafanyakazi wako na anawafundisha mbinu mbalimbali za kuongeza mauzo, kuwajali wateja na mengine muhimu.

Wafanyabiashara wengi wa kitanzania wanapuuza sana jambo hili ila ni jambo muhimu sana kwenye ukuaji wa biashara yako. Usitegemee kufanya biashara kwa mazoea halafu ukapata faida kubwa.

Pia wafanyakazi wako wanahitaji kuhamasishwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa, kujiwekea malengo kwenye maisha yao na kuboresha maisha yao na kazi zao kila siku.

4. Weka malengo ya biashara pamoja na wafanyakazi wako.

Mara nyingi mfanyabiashara anaweza kujiwekea malengo yeye mwenyewe labda mwezi huu nataka nitengeneze faida ya milioni kumi. Baada ya hapo unakwenda kuwaambia wafanyakazi fanyeni kazi kwa bidii tupate faida kubwa, hili ni kosa kubwa. Malengo yoyote yanayohitaji ukuaji wa biashara yako ni vizuri sana kama utayajadili na wafanyakazi wako. Baada ya kuwaambia lengo unaweza kupata mawazo mazuri kutoka kwao kwa sababu wao ni sehemu muhimu ya biashara yako.

Najua hapa kuna changamoto kubwa kwa sababu wafanyabiashara wengi huwa hawataki wafanyakazi wao wajue wanatengeneza faida kiasi gani, japokuwa hutaki wajue ila nakuhakikishia wanajua vizuri sana. Hivyo acha mambo haya ya kizamani na weka mipango yako mikubwa kwa kuwashirikisha wafanyakazi wako. Kwa kuwa nao watajiona ni sehemu ya maamuzi itakuwa rahisi kwao kutekeleza yale mliyokubaliana ili kufikia malengo makubwa.

5. Kuwa makini sana unapoajiri ndugu au watu ambao mna uhusiano wa karibu.

Ni kitu cha kawaida sana mtu kufungua biashara na kuweka watoto, ndugu, mke/mume kuwa wasimamizi au wafanyakazi. Ni kitu kizuri kwa sababu unawapatia kazi na pia usimamizi unaweza kuwa mzuri zaidi. Pamoja na kuwa kitu kizuri inabidi uwe makini sana, narudia tena kuwa makini sana unapoajiri watu hawa. Kama ni mtu ambaye amekosa uaminifu au ni msumbufu ni bora akuone tu mbaya kwa kumnyima kazi kuliko kumwajiri halafu akaja kuua biashara yako. Na pia nashauri unapoajiri watu hawa ambao mna uhusiano ukaendelea kuwachukulia kama wafanyakazi hivyo kama akikosea anaadhibiwa kama wafanyakazi wengine na asijione tofauti sana na wafanyakazi wengine wa daraja lake. Akianza kuleta tofauti itaharibu ufanyaji kazi kama timu ambao ni muhimu sana ili kuweza kufikia mafanikio makubwa.

Kikwazo kikubwa cha biashara yako kukua ni wewe mwenyewe kutokana na mipango yako na uwekezaji wako kwenye biashara hiyo. Wafanyakazi ni sehemu muhimu sana kwenye ukuaji wa biashara yako. Fuata ushauri huo hapo juu na mwingine utakaoendelea kujifunza ili uweze kufikia mafanikio makubwa kwenye biashara yako. Pia unaweza kuwasiliana na mimi kwa mawasiliano hayo hapo chini ili kupata ushauri zaidi wa kivitendo.

Kumbuka hakuna kikomo cha biashara yako kukua ila kile ulichokiweka wewe mwenyewe.

Nakutakia kila la kheri kwenye ukuaji wa biashara yako.

TUKO PAMOJA.

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa kwa email amakirita@gmail.com au simu 0717396253/0755953887.

kitabu-kava-tangazo4