Pesa ni tatizo, Pesa ni ngumu, Pesa hazionekani na kadhalika haya ndio maneno yaliyojaa kwenye akili za watu wengi. Huenda na wewe umeshayasema maneno haya mara kadhaa au umekuwa wimbo mzuri kwako.

Sasa leo nakwambia unafanya makosa makubwa sana ndio maana unaimba wimbo huu. Kosa kubwa unalofanya unakimbiza pesa ambazo huwezi kuzikamata hata ungekuwa na kasi gani. Na ili uweze kuondokana na tatizo hili inabidi fedha zikukimbize wewe na sio wewe uzikimbize.

Fedha zinawezaje kukukimbiza? Hilo ni swali ambalo unajiuliza, nitakupa jibu muda sio mrefu. Kabla ya kukupa jibu hilo naomba nikuulize swali moja, umesoma kitabu cha mwisho nilichotuma? Kama umekisoma tayari una majibu ya swali hilo, kama hujakisoma na ulikipata basi sina cha ziada cha kuzungumza hapa zaidi ya kukwambia kitafute ukisome. Kitabu hiko kinaitwa CHOOSE TO BE WEALTHY. Unaweza kukipata kwenye makala iliyoandikwa; Kitabu; chagua kuwa tajiri, sifa nane za mamilionea wenye furaha.

Nimeanza na kitabu hiko kwa sababu hapa nitatumia mfano mmoja uliotumiwa kwenye kitabu hiko ili kuelezea vizuri hilo swali hapo juu. Mfano wenyewe unakwenda hivi;

Siku moja viumbe wa sayari ya mbali walitembelea dunia. Walipofika duniani walizunguka kuangalia maisha ya wanadamu, waliumizwa sana na umasikini mkubwa uliokuwa kwa baadhi ya wanadamu. Waliamua kutoa msaada ili japo kuokoa hali hiyo ya umasikini. Hivyo walikubaliana kuacha kuku wao wa dhahabu. Usiku sana walichagua nyumba ya mkulima mmoja masikini, jina lake Mwendapole wakamuweka kuku yule nyuma ya nyumba yake na kisha wakatoweka kurudi huko sayari ya mbali.

GOLDEN

Mwenda pole alipoamka alishangaa kuona kuku wa ajabu nyumbani kwake. Kuku huyo alikuwa mkubwa sana na alikuwa na manyoya ya dhahabu. Wakati anaendelea kutafakari kuku yule ametoka wapi, kuku aliinuka na Mwendapole alishangaa kuona kitu kinang’aa chini ya kuku yule, kuangalia vizuri lilikuwa yai la dhahabu. Mwendapole alishangaa sana na alichukua yai lile na kwenda kuliuza na alipata fedha nyingi sana. Kwa fedha alizopata alininua vyakula, nguo, vyombo vya ndani na vitu vingine alivyokuwa anahitaji.

Mwezi uliofuata Mwendapole hakuamini macho yake, kwani kuku yule alitaga yai lingine la dhahabu. Alichukua yai lile na kwenda kuliuza na akanunua simu ya kisasa, tv kubwa, kompyuta, gari na vingine vingi.

Mwezi wa tatu kuku alitaga tena na Mwendapole aliuza yai lile na kununua kila kitu alichotamani kwneye maisha yake. Siku iliyofuata Mwendapole alipatwa na shauku ya hali ya juu, alifikiria inabidi asubiri mwezi mzima ndio apate yai lingine. Wakati huo alikuwa anahitaji hela ili anunue helikopta yake. Hivyo alijiuliza kwani haya mayai yanatoka wapi? Akasema yanatoka ndani ya huyu kuku, hivyo wazo likamjia kwamba ili kuyapata mayai hayo haraka amchinje kuku yule na kutoa mayai yote yaliyoko ndani yake.

Alichukua kisu kikali na kumchinja kuku yule, kumpasua tumboni hakukuta yai lolote. Mwendapole alilia sana kwa sababu kuku ameshampoteza na mayai hawezi kupata tena.

Maisha yalianza kuwa magumu tena na akaanza kuuza kila alichonunua, ndani ya mwaka mmoja alikuwa amerudi kwenye umasikini aliokuwa nao mwanzo, tena wakati huu akiwa na majuto makubwa.

Siku moja Mwendapole alikuwa anapita mjini akiwa na mawzo mengi. Alikutana na tajiri mmoja ambae alimshukuru sana, akamuuliza kwa nini unanishukuru? Akamwambia nashukuru yai uliloniuzia nililiweka kwenye kitamizi na baada ya muda alitoka kifaranga ambae alikuwa na sasa kila mwezi anataga yai la dhahabu. Mayai hayo naendelea kuyatamisha na naendelea kupata kuku wengi wa dhahabu.

Mwendapole alizidi kuumia sana, kumbe kila yai alilouza lingeweza kutoa kuku mwingine wa dhahabu! Kama asingeuza mayai yale angekuwa na kuku wengi ambao wanampatia mayai ya dhahabu kila siku badala ya kusubiri kila mwezi kwa kuku mmoja.

Baada ya miaka mingi, viumbe wale wa ajabu walirudi duniani kuja kuangalia mabadiliko, walishangaa kuona baadhi ya watu ni matajiri na wengine ni masikini sana akiwemo waliyemwachia kuku wa dhahabu. Matajiri walikuwa na kuku wanaotaga mayai ya dhahabu.

Nimeupenda sana mfano huu kwa sababu unaonesha uhalisia wa maisha ya wengi wetu. Tatizo kubwa linalokufanya unateseka kutafuta pesa ni kwa sababu unachukulia pesa kama bwana Mwendapole. Unakazana kutafuta pesa badala ya kukazana kutafuta mashine ya kutengeneza fedha.

Pesa ni yai la dhahabu na mashine ya kutengenezea pesa ni kuku anayetaga mayai ya dhahabu. Kama utahangaika kutafuta fedha na baadae unatumia zote kila siku utakuwa na matatizo ya fedha. Kama utatafuta fedha ila ukatumia kidogo na nyingine ukaiwekeza sehemu ambapo inaweza kuzalisha faida hata kama ni kidogo utakuwa na uhuru wa fedha baada ya muda fulani.

Tunaweza kuchukua mfano huu wa kuku kama kazi ambayo umeajiriwa au umejiajiri au biashara ambayo unafanya. Kila mwezi au baada ya muda fulani unapata mshahara au malipo au faida. Kwa kuwa akili yako inafikiria kutafuta fedha tu, unatumia fedha yote uliyopata kwenye matumizi na inapoisha unasubiri tena nyingine(kama Mwendapole alivyokuwa anasubiri yai). Mwisho wa siku kazi inaisha au biashara inapata hasara na unabaki mikono mitupu huku ukirudi kwenye umasikini wa kupindukia.

Kama akili yako ingekuwa inafikiria kutengeneza mashine ya kuzalisha fedha zaidi, hela unayopata kutokana na shughuli zako ungetumia kiasi na nyingine inayobaki ukaiwekeza kwenye sehemu mbalimbali ambazo zinaleta faida. Kwa kuendelea kufanya hivyo unafikia wakati unakuwa na uwekezaji mkubwa ambao unazalisha fedha nyingi bila hata ya wewe kufanya kazi. Hapo unakuwa umepata kuku wa dhahabu anayetaga mayai ya dhahabu.

Nakushauri sana ubadili mtazamo wako juu ya fedha, usijaribu hata mara moja kutumia fedha yote uliyopata kwenye matumizi, kuwa na sehemu ndogo ambayo utaiwekeza ili iendelee kuzalisha zaidi. Hivi ndivyo unavyoweza kutengeneza uhuru wa kifedha.

Kujifunza zaidi juu ya kutengeneza uhuru wa kifedha ikiwa ni pamoja na kubadili mtazamo wa kimasikini uliojengengewa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA ambapo kwa miezi miwili tutajadili kwa kina kuhusu fedha.

Kujiunga tma fedha tsh 10,000/= kwa 0717396253 au 0755953887 na kisha tuma email yako ya gmail na utaunganishwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

Karibu sana katika ukombozi wa kiuchumi kwa kukomboa fikra zako na mitazamo yako juu ya fedha.

Nakutakia kila la kheri, usiendelee tena kuwa kama Mwendapole.

TUKO PAMOJA.

kitabu kava tangazo