Wiki iliyopita katika tabia za mafanikio tulijadili umuhimu wa kuwekeza fedha baada ya kuweka akiba kwa muda fulani. Hii inatokana na thamani ya fedha kushuka haraka sana hivyo bila ya kuwekeza unaweza kujikuta unapoteza fedha kwa kuziweka tu benki au kwingine unakuweka.
Leo tutaangalia aina mbalimbali za uwekezaji ambapo mtu anaweza kufanya utakaosaidia kuongeza thamani ya fedha yake. Kwa kuwa tunatofautiana katika shughuli tunazofanya pia nitazungumzia uwekezaji huu kwa makundi mawili. Kundi la kwanza kwa wale ambao wapo kwenye ajira na hivyo hawawezi kupata muda wa kutosha wa kufuatilia uwekezaji wao. Na kundi la pili ni wale ambao wamejiajiri wenyewe hivyo wana muda wa kutosha kufuatilia uwekezaji wao.
Makundi haya mawili nimeyatenga tu ili kuweka urahisi wa kufanya maamuzi ila sio kwamba ni sheria unaweza kuchagua uwekezaji wowote kulingana na mapenzi yako na muda wako unavyoweza kuutumia vizuri.
Uwekezaji kwa watu ambao wamejiajiri au wanafanyabiashara.
Kwa watu ambao wamejiajiri au wanafanya biashara wana uhuru mkubwa na utawala wa muda wao hivyo wanaweza kufanya mambo mengi bila ya kuhofia kubanwa. Hapa nitazungumzia aina chache za uwekezaji kwenye mazingira ya kitanzania kwa watu ambao wamejiajiri au wanafanya biashara.
1. Kuongeza uwekezaji kwenye biashara yako.
Unaweza kuwekeza fedha zako za akiba kwenye ukuaji wa biashara yako. Japo unaweza kuwa unaongeza mtaji kwenye biashara yako kuna umuhimu mkubwa wa wewe kuendelea kukuza biashara yako zaidi kwa kila chanzo cha fedha unachopata. Biashara au shughuli yoyote unayofanya kwa sasa inaweza kukua zaidi ya hapo ilipo. Ni muhimu kujua ni sehemu zipi ambazo ukuaji wake utaleta mabadiliko makubwa kwenye biashara yako na kuwekeza sehemu hizo zaidi.
Pia unaweza kuwekeza kwenye biashara nyingine ambapo itakupatia mafanikio makubwa zaidi. Fanya uchunguzi wa biashara gani nyingine ambayo unaweza kuifanya na baada ya kuijua unaweza kuwekeza fedha zako kwa kufanya biashara hiyo.
2. Wekeza kwenye kilimo au ufugaji.
Kilimo kinachofanyika kwa utaalamu na maarifa kinalipa sana. Unaweza kutumia fedha uliyojiwekea akiba katika kilimo na ukapata mafanikio makubwa sana. Ila unahitaji kujua vizuri kilimo unachotaka kufanya na pia kuwa na muda wa kufuatilia shughuli hizo za kilimo. Kama unafikiri kuwa tu na fedha kunatosha kuajiri watu wengine wakufanyie kilimo ni rahisi sana kuingia kwenye hasara.
Kama unajiuliza ni kilimo gani kinalipa, jibu ni kwamba karibu kila kitu kinalipa kwa sasa. Kuna watu wanalima matunda na wanapata faida kubwa, kuna watu wanalima nafaka na wanapata faida kubwa pia. Fanya uchunguzi wa mazao gani yanakubali kwa eneo ambalo unataka kufanya kilimo kisha jifunze kuhusu kilimo cha mazao hayo na anza kukifanya.
Hii inakwenda pia kwenye ufugaji ambapo unawezakuwekeza fedha zako katika ufugaji na ukapata faida kubwa. Unaweza kufanya ufugaji wa kuku, mbuzi, ng’ombe na hata mifugo mingine ambayo ina matumizi kwa binadamu.
Unaweza kujifunza juu ya uwekezaji wa kilimo kwa kusoma makala hii; Unaweza kujiajiri kupitia kilimo cha vitunguu.
Hizi ni baadhi ya sehemu ambazo mtu aliyejiajiri au anayefanya biashara anaweza kuwekeza na akapata mafanikio makubwa. Wiki ijayo tutaona aina nyingine za uwekezaji ambazo zinaweza kufanyika na watu ambao wameajiriwa au hawana muda wa kutosha kufuatilia uwekezaji wanaofanya. Kumbuka aina hizo tutakazojadili wiki iliyopita pia zinaweza kufanyika na watu ambao wamejiajiri au wanafanya biashara. Pia aina hizi tulizojadili leo zinaweza kufanyika na watu ambao wameajiriwa ila inabidi kutoa muda wa kutosha kufuatilia mambo haya kama wanataka kupata mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.
TUKO PAMOJA.