Wakati tunaelekea mwishoni mwa mfululizo huu wa makala za ushauri kwa wahitimu nina imani umeshajifunza mengi sana. Kama kuna makala ambazo hukupata nafasi ya kuzisoma unaweza kuzipitia makala zote kwa kubonyeza hayo maandishi ya mwanzo ushauri kwa wahitimu yenye kiungo cha makala zote. Hata kama wewe sio mhitimu bado unaweza kutumia ushauri huu muhimu na ukafanya mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.

Wiki iliyopita nilishauri wahitimu kutenga mwaka mmoja na kuchagua kitu kimoja cha kufanya bila ya kuangalia nyuma wala kusikiliza wakatishaji tamaa. Mwaka mmoja ni mdogo sana ila kama utautumia ipasavyo utaona mabadiliko makubwa na utafanya maamuzi yenye manufaa kwneye maisha yako.

kilimo

Leo nataka tuzungumzie kauli mbiu ya nanenane mwaka huu 2014 na tuone ni jinsi gani unaweza kuitumia kuboresha maisha yako.

Kabla hatujaanza kuijadili kauli mbiu hiyo naomba nikuulize swali moja, je kauli mbiu ya nane nane mwaka huu 2014 inasemaje? Sawa najua inawezekana hujui na hii ni kwa sababu kilimo bado hakijawa na maana kubwa kwako hivyo huna muda wa kukifuatilia. Na hapa ndio tatizo linapoanzia.

Kauli Mbiu ya Maonesho ya Kilimo Nane Nane mwaka huu inasema ‘’Matokeo Makubwa Sasa Kilimo Ni Biashara”

Ni ukweli usiopingika kwamba kilimo na mifugo inaweza kuwa biashara nzuri kama itafanyika kibiashara.

Nachokushauri wewe mhitimu na mtu mwingine yeyote ambaye unataka kuboresha maisha yako kiuchumi fanya kilimo kibiashara. Ila kabla hujaanza kilimo ni vyema kufanya utafiti wako kidogo ili ujue ni nini unakwenda kufanya. Jua ni kilimo cha mazao gani unataka kufanya na pia unataka kufanyia wapi. Baada ya hapo jua mahitaji na changamoto za kilimo hiko. Ukichajiridhisha kwa taarifa utakazopata kinachofuata ni wewe kuanza kilimo na kufanya kazi kwa bidii na maarifa.

Usilete sababu zile zile.

Najua pamoja na ushauri huu bado utang’ang’ania sababu zile zile ambazo zinatumika na watu ambao hawataki kufikiria zaidi na kufanya mambo makubwa. Sababu hizo ni kama, sina mtaji, kilimo hakilipi, mvua sio za kuaminika na kadhalika.

Ni kweli sababu hizi zinaweza kuwa sahihi kabisa kwako, lakini je zina nguvu ya kukuzuia wewe kufanya kilimo? Kama una nia ya kweli ya kufanya kilimo na kuboresha maisha yako, changamoto hizi haziwezi kukuzuia hata kidogo.

Kwa mfano changamoto ya mtaji, badala ya kusema sina mtaji halafu ukaacha kabisa kufikiria, hebu jua ni kiasi gani cha fedha unahitaji ili kuanza kilimo na baada ya hapo gawanya kwa kiwango kidogo unachoweza kuanzia. Kama bado kiwango hicho kidogo ni kikubwa kwako tafuta mwenzako muunganishe nguvu na muanze kidogo na baadae muendelee kukuza mtaji wenu.

Changamoto zozote unazofikiria zinaweza kutatulika kama utakuwa na mtazamo chanya wa kuangalia suluhisho badala ya kung’ang’ana na tatizo.

Unaweza kupata mwanga kuhusu kilimo kwa kusoma makala hii; unaweza kujiajiri kupitia kilimo cha vitunguu.

Chukua hatua sasa ya kuboresha maisha yako, anza kwa kufanya kilimo cha kibiashara. Changamoto utakazokutana nazo zisikukwamishe bali angalia jinsi ya kuzitatua.

Nakutakia kila la kheri kwenye harakati zako za kuboresha maisha yako.

TUKO PAMOJA.