Kila mmoja wetu anapenda kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yake. Na kila mmoja wetu anao uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo makubwa zaidi ya anavyofanya sasa. Namaanisha hapo ulipo wewe bila ya kujali ni mambo mangapi umefanikiwa mpaka sasa bado una uwezo wa kufanikiwa zaidi na zaidi. Lakini cha kushangaza ni watu wachache sana ambao wameweza kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yao.

Hali hii ipo dunia nzima, sio kwetu sisi tu. Inasemekana wanasayansi na wagunduzi wakubwa duniani nao wametumia sehemu ndogo sana ya uwezo wao. Kwa mfano Albert Einstein, mtu anayedhaniwa kuwa na uwezo mkubwa sana wa kiakili alitumia asilimia kumi na tano tu ya uwezo wake au uwezo wa binadamu kwa ujumla.

Swali la kujiuliza ni kitu gani kinafanya watu wengi duniani kushindwa kutumua zaidi uwezo ambao upo ndani yetu? Kwa nini biashara unayofanya sasa isifikie kuwa biashara kubwa sana kitaifa na kimataifa? Kwa nini kazi unayofanya sasa usiweze kuifanya kwa viwango vikubwa sana na hatimaye kuweza kuibuka mfanyakazi bora kabisa? Kwa nini shughuli yoyote unayoifanya isifikie viwango vikubwa vya kimataifa na wewe ukapata mafanikio makubwa sana?

Kuna sababu nyingi sana zinachangia wewe kushindwa kufikia mafanikio makubwa. Nyingi unaweza kuwa unazijua ila huzifanyii kazi, ila nyingine unaweza kuwa huzijui na zinakuwa kikwazo kikubwa sana kwako. Leo tutaona kikwazo kimoja kikubwa sana ambacho ndio sumu kubwa inayokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Kwa hiki utakachojifunza leo, kama utakifanyia kazi siku moja utaangalia nyuma na kusema kwa nini sikujua mapema! Sasa mapema yenyewe ndio hii na jiandae kwa ajili ya mafanikio makubwa.

Kabla hatujaingia kwenye kikwazo hiki kikubwa naomba nikushirikishe habari moja ambayo ilitokea miaka mingi iliyopita.

Mashindano ya riadha yamekuwepo kwa muda mrefu sana duniani. Kabla ya mwaka 1954 haikuwahi kufikiriwa wala kutokea kwa binadamu kuweza kukimbia mile moja(meta 1,600) chini ya dakika nne. Wataalamu wote wa mambo ya riadha na hata wa kitabibu walisema haiwezekani kabisa kwa binadamu kuweza kukimbia kwa kasi hiyo. Walienda mbele zaidi na kudhibitisha kwamba mwili wa binadamu hauna uwezo wa kukimbia maili moja chini ya dakika nne. Na walisema ikiwa mtu atajaribu kufanya hivyo anaweza kupata matatizo makubwa kiafya.

Mwaka 1940 waliweka kiwango kuwa dakika 4 na sekunde 1, lakini bado wanariadha wengi walikazana sana kuweza kumaliza mile moja kwenye muda huo ila bado walishindwa.

Tarehe 06/05/1954 Roger Bannister alivunja kizuizi hiki kwa kuweza kukimbia mile moja kwa dakika tatu na sekunde 59. Roger alikuwa binadamu wa kwanza kuweza kukimbia maili moja chini ya dakika nne, kitu ambacho iliamonika hakiwezekani licha ya watu kujaribu sana kwa zaidi ya miaka kumi.

Roger

Sasa, uzuri wa habari hii hauishii hapa, kwamba Roger aliweza kuweka rekodi ambayo iliaminika haiwezekani. Uzuri wa habari hii unakuja hapa; Wiki sita baada ya Roger Bannister kuweka rekodi hii mwanariadha mwingine aliweza kuweka rekodi ya kukimbia mile moja chini ya dakika nne. Na kwa mwaka huo mmoja tu wanariadha wanne waliweza kukimbia mile moja chini ya dakika nne. Mpaka kufikia sasa kukimbia maili moja chini ya dakika nne ni kitu cha kawaida ambapo hata wanafunzi wa shule wanaweza kufanya zoezi hili.

Unajifunza nini katika habari hii?

Kwa muda mrefu sana watu walishindwa kukimbia maili moja chini ya dakika nne kwa sababu waliaminishwa kwamba haiwezekani. Wanariadha wazoefu, madaktari na wataalamu wengine walidhibitisha kwamba ni hatari kwa binadamu kujaribu kufanya zoezi hilo. Hivyo watu wengi waliojitahidi kujaribu kukimbia mbio hizi walijiwekea ndani ya akili yao kwamba maili moja chini ya dakika nne haiwezekani.

Katika hali hiyo mwanariadha mmoja aliamua kukubaliana na hili na akaweka lengo la kuweka rekodi ya kukimbia maili moja chini ya dakika nne. Alifanikiwa kufanya hivyo baada ya maandalizi makubwa.

Kitu kikubwa cha kushangaza na kujifunza baada ya mwanariadha huyu kuweka rekodi hiyo mwaka mmoja watu wanne waliweza kuweka rekodi hiyo! Yaani zaidi ya miaka kumi watu walishindwa kuweka hii rekodi, lakini mwaka mmoja baada ya mmoja kuweka rekodi wengine wanne waliweza kufanya vile.

Hii inatokana na kwamba mwanzoni waliaminishwa haiwezekani na hivyo hata walipoweka juhudi kubwa bado walikubali haiwezekani. Lakini baada ya mtu mmoja kuweza kila mtu aliona inawezekana na walipofanya juhudi kubwa waliweza kufikia rekodi hiyo.

Hivi ndivyo ilivyo kwenye mafanikio yako binafsi. Mambo mengi unayoshindwa kuyafikia ni kwa sababu ndani ya nafsi yako unaamini haiwezekani. Na imani hii inatokana na jamii inayokuzunguka, hakuna aliyeweza kufanya hivyo. Kwa hiyo unakubali haiwezekani na unaendelea kufanya kile ambacho kila mtu anafanya.

Leo nataka nikuambie wewe ni zaidi ya unavyojifikiria sasa. Chochote unachofanya unaweza kukifanya kwa ubora na mafanikio makubwa sana kuliko watu wengine wote wanaokifanya duniani kote. Kataa kuingizwa imani hizi ambazo jamii na huenda dunia nzima inaamini haiwezekani. Chagua kufikia mafanikio makubwa na anza kazi kufikia mafanikio hayo.

Jua kikwazo chako kikubwa kwenye kufikia mafanikio amkubwa ni nini na anza kufanyia kazi kikwazo hiko. Ondoa kabisa imani kwamba huwezi kufikia kile unachofikiri kwa sababu hakuna aliyeweza kufikia. Wewe ni wa pekee na una uwezo mkubwa sana ulio ndani yako. Tumia uwezo huu kufikia mafanikio makubwa na utawafungulia wengine njia waone kwamba inawezekana nao kufikia mafanikio makubwa.

Amua leo kuwa Roger Bannister kwenye kile unachokifanya na tenga miaka kumi ya kufanya kitu hiki kimoja kila siku na hata kabla ya muda huo kuisha tutakutana kileleni kwa kuwa wote tutakuwa tumefikia mafanikio makubwa sana.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio.

TUKO PAMOJA NA TUTAKUTANA PALE KILELENI.