Kwa muda sasa umekuwa ukiishi maisha ambayo kila kukicha yanazidi kuwa magumu hali ambayo inasababisha hata wewe mwenyewe ukose raha. Ni maisha ambayo umekuwa ukiyaishi kwa miaka sasa na pengine umekuwa ukijiuliza maswali mengi sana ni kitu gani hasa kinachosababisha uwe hivyo.
Kila ukiangalia juhudi unazopiga unaona zinakwama au hazisogei kabisa na hali hii kuna wakati imekuwa ikikuchanganya na kukukatisha tamaa na kuona kama maisha basi tena, wapo wenye maisha yao.
Watu wengi wanajikuta wapo katika hali hii na hawajui hasa nini cha kufanya na pia hawajui chanzo cha maisha kwao kuwa magumu siku hadi siku ni nini? Kitu pekee ambacho hufahamu na kinachofanya maisha yako kuwa magumu ni wewe mwenyewe. Wewe ndiye unayefanya maisha yako kuwa magumu na hakuna mtu wa kumlaumu.
Ni kivipi hasa unafanya maisha yako kuwa magumu? Hivi ndivyo unavyofanya maisha yako kuwa magumu zaidi:-
1.Unaruhusu kila mtu anakushauri juu ya maisha yako.
Maisha yako yanakuwa magumu kwa sababu unasikiliza na kufanya kila unachoambiwa na watu wengine juu ya maisha yako. Ukitaka kufanikiwa zaidi ni muhimu pia kujisikiliza wewe mwenyewe na kusikiliza sauti ya ndani mwako inasema nini.
Ni vizuri ukawa na uamuzi na msimamo imara juu ya maisha yako na jinsi unavyotaka yawe na sio kutekeleza kila unachoambiwa na watu wengine. Kumbuka wewe ndiye mwamuzi hasa wa mwisho wa maisha yako.

 
2.Umekuwa mwongeaji sana.
Wapo watu ambao ni waongeaji wazuri sana juu ya mipango na malengo waliyonayo katika maisha lakini sio watekelezaji wa haraka. Kama una tabia ya kuongea sana juu ya malengo uliyonayo na vitendo vinakuwa vinachelewa nakupa uhakika utazidi kufanya maisha yako kuwa magumu siku hadi siku.
Hata uwe na mipango na malengo mazuri vipi kama tu wewe utakuwa unaongea na huchukui hatua juu ya ndoto zako basi kwako itakuwa ngumu kufanikiwa na utazidi kufanya maisha yako kuwa magumu. Chukua sasa hatua ya kutekeleza ndoto zako acha kuongea sana hakutakusaidia lolote katika maisha yako ya sasa na baadae.
3.Unajaribu kushindana na kila mtu.
Kama una tabia ya kujaribu kushindana na kila mtu elewa kabisa wewe utakuwa ni mtu wa kushindwa. Acha tabia hii ya kushindana na kila mtu kwani jinsi unavyoiendeleza ndivyo maisha yako yanazidi kuwa magumu. Maisha yanakuwa magumu kwa sababu wengi unaoshindana nao wanakuwa  wanakukatisha tamaa kutokana na mambo wanayoyafanya.
Kama unataka kushinda hili na kuwa huru katika maisha yako jijengee tabia ya kushindana na wewe mwenyewe. Vunja rekodi zote ambazo umeshawahi  kujiwekea hapo utakuwa unaondokana na hali ya kufanya maisha yako kuwa magumu. Ishi maisha yako wala usijaribu kushindana sana hapo utaona mafanikio.
3.Unazingatia sana kila kitu.
Hautaweza kupata kile unachokitaka wala kufanikisha malengo yako kama wewe utakuwa mtu wa kuzingatia kila kitu katika maisha yako. Watu wenye mafanikio wanatabia moja muhimu sana ya kuweka nguvu ya uzingativukwa mambo wanayoyataka tu na si vinginevyo.
Najua una malengo mengi mazuri ambayo unataka kuyatekeleza lakini nakushauri kama unataka kuyaona malengo yako yanatimia jenga tabia moja muhimu sana ya kufanyia kazi malengo machache na weka nguvu zote huko utaona matokeo chanya. Watu wengi ambao wanazingatia kila kitu nikiwa na maana kila kitu kinachopita wanataka kufanya hawa ndio moja ya watu ambao hawafanikiwi katika maisha yao yote.
5.Unaogopa sana watu wanaokuzunguka.
Kama unataka maisha yako yawe ya faida acha kuhofia wala kuogopa watu wanaokuzunguka. Kutokana na kuhofia watu hawa wanaokuzunguka unajikuta unashindwa kufanya mambo yako mazuri kwa kuhofia pengine unaweza ukachekwa kama ikitokea umekosea.
Katika maisha hakuna mtu anayejali sana mambo yako kama unavyofikiria na kama utaogopa sana juu ya watu wanaokuzunguka utazidi kufanya maisha yako kuwa magumu zaidi siku hadi siku kwani hutafanya kitu kwa sababu ya hofu ulizonazo.
6.Unazingatia sana makosa yaliyopita.
Katika maisha yetu tunayoishi kuna umuhimu mkubwa sana wa kujisamehe hasa pale tunapokosea. Tunahitaji kujifunza juu ya makosa yetu na kusonga mbele. Acha kulalamika wala kulaumu sana pale ulipokosea hiyo imeshapita. Panga mipango yako kisha tekeleza na usonge mbele sahau makosa uliyoyafanya. Kama utakuwa unazingatia sana makosa yako utazidi kufanya maisha yako kuwa magumu.
7.Unatumia muda wako vibaya.
Kwa kawaida kila mtu amepewa masaa 24 kwa siku, je hayo masaa unayatumiaje? Kama unatumia muda wako vizuri elewa kabisa utaishi maisha ya mafanikio. Lakini kama unatumia muda wako vibaya na kufanya vitu ambavyo vinakupotezea muda tambua pia hivyo ndivyo unavyopoteza maisha yako . Muda wako unathamani kubwa sana kuliko unavyofikiri.
Hivi ndivyo unavyofanya maisha yako kuwa magumu siku hadi siku.Chukua hatua ya kufanya mabadiliko makubwa katika maisha yako na ili kufanikisha hili hakikisha unatembelea mtandao  huu wa  AMKA MTANZANIA  mara kwa mara na kujifunza mambo haya muhimu sana kwenye maisha yako.Nakutakia kila la kheri katika safari ya ukombozi wa maisha yako.
TUPO PAMOJA!