Karibu kwenye uchambuzi wa vitabu ambapo tutakuwa tukichambua baadhi ya vitabu vizuri ambavyo vinaweza kuwa msaada mkubwa kwenye kuboresha maisha yetu. Katika uchambuzi huu tutajifunza yale mambo muhimu ambayo yameandikwa kwenye kitabu husika na tutaona ni jinsi gani tunaweza kutumia tunayojifunza kwenye maisha yetu.
Katika uchambuzi wa vitabu tutaanza na kitabu; RICH DAD POOR DAD, kitabu ambacho kimeandikwa na Robert Kiyosaki. Kitabu hiki kinaelezea jinsi mfumo wa elimu ulivyo tofauti na maisha halisi ambayo yanabadilika kwa kasi sana. Pia katika kitabu hiki tunajifunza somo muhimu la kuhusu matumizi na usimamiaji wa fedha binafsi ili kuweza kuwa na uhuru wa kweli kwenye maisha.
UTANGULIZI WA KITABU.
Kitabu kinaanza kwa Robert kusema kwamba alibahatika kuwa na baba wawili, mmoja alikuwa baba yake mzazi na mwingine alikuwa baba wa rafiki yake. Aliweza kujifunza mambo mengi sana kwa baba hawa wawili ambao walikuwa karibu naye.
Baba yake mzazi alikuwa msomi mwenye shahada ya uzamivu(PHD), wakati baba wa rafiki yake hakumaliza darasa la nane. Baba wote wawili walikuwa na mafanikio makubwa kwenye kile wanachofanya. Wote walikuwa wanapata kipato kizuri. Ila mmoja alikuwa akipata shida sana kifedha, wakati mwingine alikuwa tajiri mkubwa sana. Mmoja alikufa na kuacha fedha nyingi kama urithi kwa watoto na pia kutoa msaada wakati mwingine alikufa akiacha madeni yalipwe na watoto wake. Wote walimshauri Robert ila ushauri ulikuwa tofauti.
Kwa kupata bahati ya kushauriwa na baba wawili ilimwezesha Robert kujua ni ushauri gani wa kuchukua na upi wa kuacha.
Baba zake hawa walikuwa na ushauri unaokinzana linapokuja swala la fedha. Mmoja alisema fedha ndio chanzo cha matatizo na mwingine alisema ukosefu wa fedha ndio chanzo cha matatizo.
Mmmoja alimshauri Robert aende shule asome kwa bidii na kufaulu vizuri ili aweze kupata kazi nzuri na yenye usalama. Mwingine alimshauri aende shule ajifunze vizuri ila pia ajifunze jinsi ya kuifanya fedha imfanyie kazi. Mmoja alimshauri Robert kutafuta kampuni nzuri ya kufanya kazi, mwingine alimshauri kutafuta kampuni nzuri ya kununua. Mmoja alisema kinachomfanya asiwe tajiri ni kwa kuwa ana watoto, mwingine alisema kitakachomfanya awe tajiri ni kwa kuwa ana watoto. Mmmoja alisema nyumba ni mali inayozalisha, mwingine alisema nyumba ni mali isiyozalisha(mzigo/deni). Baba mmoja alishawishi kuzungumzia fedha na uwekezaji, mwingine alizuia watoto kuzungumzia fedha na uwekezaji.
Robert anasema sababu kubwa inayofanya matajiri wanaendele akuwa matajiri, na masikini wanaendelea kuwa masikini huku tabaka la kati likiteseka ni kwa kuwa somo la fedha linafundishwa nyumbani. Hivyo mzazi ambae ni masikini na hana uelewa wa fedha anawafundisha watoto wake kile anachokijua kuhusu fedha na ambacho kimemfanya awe masikini. Na mzazi tajiri anafundisha watoto wake mbinu za fedha zilizomfanya awe tajiri na hivyo kuendeleza utajiri wao.
Elimu ya fedha haifundishwi shuleni, ndio maana utakuta madaktari, wanasheria na wanataaluma wengi ambao wamefaulu vizuri sana masomo yao ila wanateseka na fedha maisha yao. Robert alibahatika kujifunza kutoka kwa wazazi hawa wawili na hivyo kujua ni kipi cha kuepuka na kipi cha kuchukua. Kwa mfano baba mmoja anasema siwezi kupata fedha ya kununua kitu fulani, baba mwingine anasema nitapataje fedha ya kununua kitu fulani.
Kuna tofauti kubwa sana ya kauli; SIWEZI KUPATA na kauli; NITAPATAJE. Moja inafanya mtu akate tamaa na kuamua kushindwa wakati nyingine inamfanya mtu afikiri zaidi na hivyo aweze kupata suluhisho. Kutumia kauli ya SIWEZI KUPATA ni kufanya ubongo ulale na kuwa mvivu, kutumia kauli ya nitapataje inafanya ubongo ufikiri zaidi na hivyo kuweza kutatua tatizo.
Mawazo ya wazazi hawa wawili yalikuwa tofauti kabisa na tofauti hii ndio iliyotokea pia kwenye fedha na utajiri. Baba mmoja alisema hawezi kuwa tajiri mwingine alisema ni lazima awe tajiri.
Akiwa na miaka tisa Robert aliamua kuwa anasikiliza na kuchukua ushauri wa baba aliyekuwa tajiri na kuacha ushauri wa baba aliyekuwa masikini. Baba aliyekuwa tajiri ni yule ambaye hakuwa na elimu kubwa ya darasani, na baba aliyekuwa masikini ni yule aliyekuwa na shahada ya uzamivu.
Kwa miaka 30 Robert alijifunza masomo sita muhimu kuhusu fedha kutoka kwa baba yake tajiri na masomo hayo ndio atatufundisha kwenye kitabu hiki. Masomo hayo yatakuwa nguzo ya wewe kufikia uhuru wa kifedha kwako mwenyewe na hata kwa watoto wako.
TUNAJIFUNZA NINI?
Katika sehemu hii ya utangulizi tunajifunza kwamba mfumo wa elimu hautoi elimu ya fedha ambayo ni muhimu sana kwenye maisha. Pia tunajifunza kwamba sehemu kubwa ya umasikini wetu inatokana na mawazo ambayo tumejijengea kwenye vichwa vyetu.
Tubadili mawazo haya na tuendelee kujifunza kila siku kuhusu fedha na uwekezaji ili tuweze kuondoka kwenye utumwa wa fedha.
Tutaendelea na uchambuzi wetu na kujifunza zaidi.
TUKO PAMOJA.
Kama huna kitabu hiki unaweza kukipata kwa kubonyeza maandishi haya Robert Kiyosaki – Rich Dad, Poor Dad
kwa mwendo huu lazima umasikini uuishe kabisa kwenye maisha yangu asante sana.
LikeLike
Ni kweli umasikini hauwezi kupata nafasi kwa elimu hii.
Karibu sana, TUKO PAMOJA.
LikeLike
kaka kiukwel kwa elimu hii hata hiyo elf hamsn ni ndogo sana.thamani yake akiln n kubwa kushinda.mazuzu hawawez kulitambua hlo
LikeLike
Asante sana Godlove,
Ni kweli gaharama ya elimu hii ni kubwa sana ila kwa kuwa tunapenda kila mtanzania aweze kuipata tunaweka gharama ambazo yeyote mwenye nia ya kujifunza anaweza kumudu.
TUKO PAMOJA.
LikeLike
asante sana kwa uchambuzi mzuri inafundisha sana
hongera aman kwa kazi nzuri unayotushirikisha
ubarikiwe zaidi
LikeLike