Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu RICH DAD POOR DAD, kusoma chambuzi zilizopita bonyeza maandishi haya. Makala za juu ndio mpya, za chini ni za zamani, hivyo kusoma kwa mtiririko mzuri anza na za chini ndio uje za juu.
Katika uchambuzi uliopita RICH DAD alimfundisha Robert somo la kwanza katika kuelekea kwenye mafanikio na uhuru wa kifedha. Somo lenyewe ni kwamba matajiri hawaifanyii kazi fedha ila fedha inawafanyia kazi wao. Masikini wanafanya kinyume chake.
RICH DAD aliendelea kuongea na Robert na alimweleza kwamba kama anataka mafanikio ni lazima ajifunze jinsi ya kuifanya fedha imfanyie kazi. Na alimwambia kwamba kujifunza kuifanya fedha ikufanyie kazi ni elimu ya maisha yote na sio ya siku moja. Alimwambia watu wengi wanakwenda vyuoni na baada ya kuhitimu elimu yao wanaacha kujifunza. Aliendelea kumwambia jinsi unavyoendelea kujifunza ndio jinsi unavyoona kuna vingi huvijui, ila watu wengi sana hawajifunzi somo la fedha. Wanakwenda kazini, wanapata mshahara na kujitahidi kuishi kwa mshahara huo basi. Baadae wanaanza kujiuliza kwa nini wana matatizo ya kifedha na wanafikiri wakipata fedha nyingi zaidi ndio tatizo lao litaisha. Wachache ndio wanafahamu kwamba kukosa elimu ya fedha ndio tatizo kubwa kwao.
Baada ya maelezo haya, RICH DAD alimuuliza Robert kama bado anataka kuendelea kujifunza, Robert alimjibu ndio. RICH DAD alimwambia sawa nenda kafanye kazi, sasa hivi sitakulipa chochote. Robert alishangaa sana, RICH DAD akamwambia umeshakubali kutokufanyia kazi fedha, sasa nenda kafanye kazi. Aliendelea kulalamika pale kwamba alikuja kuomba kuongezewa mshahara na sasa anakwenda kufanya kazi bure? RICH DAD alimshika kichwani na kumwambia tumia hii, akimaanisha atumie kichwa chake na kisha akamwambia ondoka.
Mbio za panya.
Robert hakumwambia POOR DAD kwamba alikuwa anafanya kazi bure. Yeye na Mike kwa wiki tatu waliendelea kufanya kazi bila ya kulipwa chochote. Wiki ya tatu RICH DAD alikuja walipokuwa wanafanya kazi, akawaambia waende nae kwenye matembezi. Aliwauliza mambo yanakwendaje? Kuna mambo mapya mmejifunza? Robert na Mike waliangaliana, akawaambia mnahitaji kujifunza mambo mengi ili muweze kuondoka kwenye kuifanyia kazi fedha kama ambavyo wafanyakazi wake wanafanya.
RICH DAD aliwaambia mkijifunza mambo hayo muhimu kuhusu fedha mtakuwa na maisha yenye uhuru na furaha. Ila msipojifunza mtaishia kuwa na maisha magumu ya kuifanyia kazi fedha kama wafanyakazi wangu wanavyofanya. Aliwaambia kama hiko ndio wanataka basi atawaongeza mshahara na kufikia senti ishirini na tano kwa saa. Aliwaambia anataka kukuza mtazamo wao ili waweze kuona mambo muhimu ambayo wafanyakazi wengine hawawezi kuyaona. Mike na Robert hawakujibu kama wamekubali ongezeko lile, akawaambia atawalipa dola moja kwa saa, hawakujibu, akawaambia atawalipa dola mbili kwa saa. Bado walikaa kimya ila kimoyo moyo walikuwa wanatamani wakubali malipo yale kwa sababu ni makubwa sana kwa umri wao. Baadae RICH DAD aliwaambia atawalipa dola tano kwa saa, hawakukubali ila moyoni walikuwa wanasukumwa sana kukubali ofa ile.
RICH DAD aliwaambia vizuri sana, kwa kuwa hawakukubali, aliwaambia watu wengi wana bei na bei hiyo inasababishwa na hisia mbili nazo ni hofu na tamaa. Kwanza hofu ya kutokuwa na fedha inatufanya tufanye kazi kwa bidii sana na tukishapata hiyo fedha tamaa ya kuitumia inakuwa kubwa. Na hapa ndio utaratibu unajengeka na utaratibu huu ni AMKA, NENDA KAZINI, PATA MSHAHARA, LIPA MADENI. na kujirudia hivyo kila mwezi. Maisha ya watu wengi yanaendeshwa na hisia hizo mbili, na kama fedha ikiongezeka, tamaa ya kuitumia nayo inaongezeka. Hizi ndio zinaitwa MBIO ZA PANYA.
Mike alimuuliza RICH DAD je kuna njia nyingine? Alimjibu ndio ipo ila kuna watu wachache sana wanaoijua. Alimuuliza ni njia ipi hiyo? RICH DAD alimjibu hiyo ndio nataka mjifunze na kuijua wakati tunafanya kazi pamoja na ndio maana nimeondoa mifumo yote ya malipo kwenu. Mike alimuuliza je una maoni yoyote maana tumefanya kazi kwa juhudi kwa muda sasa na hatuoni mabadiliko. RICH DAD alimjibu hatua ya kwanza ni kusema ukweli wa hisia zilizopo ndani yao. Aliwaambia wafanyakazi wengi wanapata hisia za hofu ya kutokuwa na fedha ila badala ya kuikabili kwa kufikiri wanakimbilia kupata fedha na fedha inawaendesha.
Tunajifunza nini hapa?
Kuna mambo mengi ya kujifunza katika sehemu hii ya uchambuzi, baadhi ni;
1. Ili kufikia mafanikio na kupata uhuru wa kifedha ni muhimu kujifunza jinsi ya kuifanya fedha ikufanyie kazi.
2. Wafanyakazi wengi wanaishia kuwa watumwa wa fedha kwa sababu hawapati elimu ya fedha.
3. Kuna hisia mbili zinazotutawala binadamu kwenye suala la fedha nazo ni, HOFU NA TAMAA.
4. Hisia hizi mbili zinawafanya watu wengi kuingia kwenye MBIO ZA PANYA maisha yao yote.
5. Mbio za panya ni pale ambapo mtu anafanya jambo kwa kurudia rudia japo halina manufaa kwake. Kwa mfano watu wengi wanakwenda shule, wanamaliza na kuomba ajira kiahs maisha yao yote yanakuwa; AMKA ASUBUHI, NENDA KAZINI, PATA MSHAHARA, LIPA MADENI.
Tutaendele akujifunza katika sehemu ya uchambuzi itakayofuata.
Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa na uhuru wa kifedha.
TUKO PAMOJA.
Nilikuwa naomba makala hii ya uchambuzi iwe ndefu kidogo.
sasa naona fupi sana.
LikeLike
Asante kwa maoni. Nilipanga kuenda taratibu ili kila mmoja aweze kuelewa na kujifunza kwa hatua. Kama maoni yakiwa mengi tutaongeza urefu. Mara nyingi makala hazizidi maneno elfu moja ili kutochoka wakati wa kusoma.
LikeLike
Naungana na mdau hapo juu makala iwe ndefu zaidi au uiongezee idadi ya siku ya kutoka…ushatufundisha vizuri sana namna ya kusoma kwa mazingatio..kwa yule ambaye spidi yake ya kusoma ndogo itabidi awe anasoma polepole kulingana na spidi yake..tuna hamu kubwa ya kukimbizana na muda ili tuyajue mengi zaidi..sasa hivi hatutambai bali tunakimbia..ingawa wanasema slow but sure nadhan hiyo imekua slow zaidi kwetu…asante sana wazo langu ni hilo tu
LikeLike
Asante kwa maoni, nitayafanyia kazi.
LikeLike