Mafanikio kwenye ujasiriamali yanatokana na vitu vingi sana. Ni muhimu sana kujifunza mambo yote yatakayokuletea mafanikio ili uweze kufikia mafanikio makubwa kupitia ujasiriamali. Leo tutaona hisia mbili zinazowaongoza au kuwatawala binadamu na jinsi unavyoweza kuzitumia kufikia mafanikio makubwa sana. Wakati mwingine tutajifunza mambo mengine yatakayokuletea mafanikio makubwa.

Hisia ya kwanza; hofu ya kupoteza.

Binadamu wote huwa tunapata hofu ya kupoteza kitu kizuri ambacho tayari tunacho. Au tunakuwa na hofu ya mambo kuwa mabaya zaidi siku za mbeleni kama tusipochukua hatua fulani sasa. Watu wanahofia kupoteza fedha, wanahofia kupoteza muda, wanahofia kupoteza afya zao, wanahofia kupoteza watu wao wa karibu na pia wanahofia kupoteza hadhi yao katika jamii. Kutokana na hofu ya kupoteza kuwa kubwa sana, mtu yupo tayari kutoa chochote anachoweza ili kulinda kile anachokipenda sana kisipotee.

Unawezaje kutumia hofu ya kupoteza ili kufanikiwa kwenye ujasiriamali? Wewe kama mjasiriamali ambaye unaijua vizuri bidhaa au huduma unayotoa jaribu kujiuliza ni kwa jinsi gani bidhaa au huduma hiyo itamwondolea mtu hofu ya kupoteza. Je inaweza kuwasaidia watu wasipoteze muda? Au wasipoteze fedha? Au wasipoteze afya zao? Baada ya kujua ni kitu gani bidhaa au huduma yako inazuia mtu asipoteze tumia hiyo kama njia yako ya kutafuta masoko. Kama ukiweza kufanya hivi utapata wateja wengi sana wa bidhaa au huduma yako. Kwa mfano makampuni ya bima yanapata wateja wengi kwa sababu watu hawataki kupoteza nyumba, magari, afya na mali nyingine. Hivyo wanazilipia bima ili ikitokea vinapotea anapatiwa vingine.

Hisia ya pili; tama ya kupata zaidi.

Hisia ya pili ambayo ipo kwa kila binadamu ni tama ya kupata zaidi. Haijalishi mtu kwa sasa ana nini bado atataka zaidi, wenye fedha atataka fedha zaidi. Watu wanataka usalama zaidi, ufahari zaidi, hadhi kwenye jamii, heshima na hata furaha zaidi. Hakuna kikomo cha tama hii ya kutaka zaidi kwa binadamu, kwa sababu jinsi wanavyopata ndio wanataka zaidi.

Unawezaje kutumia hisia hii kufikia mafanikio makubwa. Ijue vizuri bidhaa au huduma unayoitoa wewe kisha jiulize ni vitu gani itaviongeza kwa mtumiaji uliyemlenga. Ukishajua vitu hivi itangaze bidhaa au huduma yako kwa faida hizo ambazo mtu atazipata kwa kuitumia. Kwa njia hii utapata wateja wengi. Kwa mfano simu za kifahari na hata magari ya kifahari havina tofauti sana na vile vya kawaida ila kwa vile anayetumia vile vya kifahari anaonekana kuwa na hadhi kubwa kwenye jamii basi watu wako tayari kulipa fedha nyingi kwa bidhaa hizo kwa vile hadhi yao kwenye jamii itaongezeka zaidi na wakati mwingine wataheshimiwa zaidi.

Tumia hisia zote mbili kufanikiwa zaidi.

Baada ya kuona hisia hizi mbili na kwa kuwa unaifahamu vizuri bidhaa au huduma unayotoa jipange kutumia hisia hizi mbili kuongeza wateja na watumiaji. Andaa mpango wako wa masoko au matangazo yako kwa kulenga ni vitu gani mtu anavipata kwa kutumia bidhaa au huduma yako. Vieleze kwa kifupi na kwa undani ili mtu aelewe vizuri. Kisha angalia itamsaidia mtu kutopoteza vitu gani na vieleze vizuri kwa ufupi na kwa kueleweka. Ukiweza kuiweka bidhaa au huduma yako vizuri kwa hisia hizi mbili utapata wateja na watumiaji wengi sana wa bidhaa au huduma yako.

Mjasiriamali mwenzangu anza kutumia mbinu hii nzuri kuweza kuwafikia wateja wako. Achana na ile dhana ya zamani kwamba watu watanunua kwa sababu wewe unauza. Ni muhimu sana wewe kuwashawishi waje kununua na utafanya hivyo kwa kuhusisha bidhaa au huduma yako na hisia mbili ambazo ni hofu ya kupoteza na tama ya kupata zaidi.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara.

TUKO PAMOJA.