Karibu sana kwenye SIKU 30 ZA MAFANIKIO MAKUBWA, katika siku hizi 30 utajifunza mambo yote muhimu unayohitaji kujua ili kuweza kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Kumbuka kwamba unaweza kufikia mafanikio makubwa kwenye jambo lolote unalofanya au unalotaka kufanya. Kikubwa ni wewe kujua misingi unayotakiwa kufuata na kisha kuifuata na hatimaye utafikia mafanikio makubwa.
Kitu kikubwa ninachokushauri kabla ya kuendelea na siku hizi 30 ni kwamba yale unayojifunza yatumie kwenye maisha yako. Kwa mfano kama kwenye makala ya leo kuna kitu utajifunza, anza mara moja kukitumia kwenye maisha yako. Usiseme nikishafanya kitu fulani ndio nitafanya hivi, haitakuja kutokea. Pata wazo jipya angalia jinsi ya kuliingiza kwenye shughuli zako na maisha yako kisha liweke kwenye kazi mara moja.
Leo siku ya kwanza kabisa kwenye siku 30 tunaangalia msingi wa kwanza kabisa wa kufikia mafanikio yoyote kwenye maisha yako.
Sababu namba moja kwa nini watu wengi hawafanikiwi kwenye maisha ni kwamba hawajui ni kitu gani hasa wanataka.
Sasa wewe usiwe mmoja wa watu hawa, ni lazima uwe tofauti nao ili uweze kufikia mafanikio makubwa. Hivyo msingi wa kwanza kabisa ni JUA NI KITU GANI UANATAKA NA JINSI GANI UNAWEZA KUKIPATA. Watu wengi wanakwenda tu na maisha bila ya kujua ni nini wanataka hivyo wanaishi kila siku kama walivyoishi jana yake, wanajikuta wanazunguka na kurudi pale pale walipoanzia.
Anza leo kufikiria ni kitu gani unataka kwenye maisha yako, sio lazima ufanye maamuzi leo, ila fikiria kwa undani ni nini hasa unataka. Unataka furaha? Unataka mafanikio? utajiri? nguvu ya utawala? umaarufu? ushawishi? ni nini hasa unataka?
Unaweza kupata chochote kile unachotaka ila kwanza ni lazima ujue ni kipi hasa unachotaka. Ukishafikiria na kufikia muafaka kwamba kwenye maisha yangu nataka kitu fulani, fanya maamuzi ya kwamba hiko ndio kitakachokuongoza kwenye maisha yako.
Hiki ni kitu cha kwanza kabisa ambacho hakuna anayeeza kukusaidia kufanya, utajifunza yote mengine kwenye siku hizi 30, ila ni nini unataka hiko utaamua wewe mwenyewe.
Kujua ni jinsi gani ya kupata kile unachotaka.
Baada ya kujua kile unachotaka kwenye maisha yako, sasa unaweza kupanga ni jinsi gani ya kupata kile unachotaka. Kwa vile wewe ni tofauti na watu wengine wanaokwenda tu na msafara, hata mipango yako itakuwa tofauti na ya watu wengine.
Katika siku hizi 30 utajifunza mbinu mbalimbali za kupata kile ambacho unataka kwenye maisha yako. Utajifunza jinsi ya kuwa na mawazo sahihi, na jinsi ya kujihamasisha ili kuweza kuzivuka nyakati ngumu kwenye safari ya mafanikio.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)
TUKO PAMOJA.