Habari za leo mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA, karibu kwenye kipengele cha ushauri wa changamoto mbalimbali zinazokuzuia kufikia mafanikio kwenye kile unachofanya. Leo hii tutajadili kuhusu changamoto ya kujenga au kuwekeza kwenye biashara. Changamoto hii imekuwa ikiwasumbua watu wengi sana na kujikuta wanafanya maamuzi ambayo yanawanyima fursa nzuri za kufikia mafanikio makubwa.
Kabla hatujaingia kwenye mjadala wa changamoto hii naomba tuone maoni yaliyotumwa na msomaji mwenzetu kuhusiana na changamoto hii;
Changamoto yangu mimi nahitaji nyumbani kwangu kwanza (niwe na uhakika wa malazi) kabla ya kuanza biashara ila naona kama nachelewa kufiikia malengo yangu.
Nawaza pia nyumba yangu inaweza kunisaidia kuwa colateral kukopa benki ili nianzishe biashara yangu.
Kufanya maamuzi kati ya kujenga au kuwekeza kwenye biashara ni changamoto inayowapata watu wengi. Je ni kipi bora kufanya? Kujenga au kufanya biashara?
Hapa nitatoa maoni yangu kulingana na changamoto hii na wewe utafanya maamuzi kulingana na hali yako ilivyo.
Kama upo tayari kuingia kwenye biashara na una muda wakutosha kusimamia biashara zako nakushauri uingie kwenye biashara na uachane na kwanza kujenga. Na hii nasisitiza sana hasa kwa watu ambao hawana kipato kikubwa sana cha kuweza kujenga kwa mara moja. Nashauri hivi kwa sababu kujenga kunaweza kuwa njia ya kuzika fedha na hivyo kushindwa kuzitumia mara moja kuzalisha fedha zaidi.
Tatizo la kujenga linaanzia hapa.
Tatizo la kujenga hasa kwa watu ambao wana vipato vidogo na vipato vya kati ni kwamba huwezi kujenga kwa mara moja. Hivyo watu wengi hujikuta wanaanza kujenga kidogo kidogo na kutumia muda mwingi sana kwenye kujenga. Kwa mfano unajidunduliza na kununua kiwanja, kisha unaanza tena kujiwekea akiba na kidogo kidogo unapeleka kwenye ujenzi. Ujenzi huu wa kufanya kidogo kidogo unaweza kukuchukua muda mrefu sana na chini sana inakuwa miaka mitano. Kwa miaka hii mitano hata kama kila mwezi unapeleka laki moja kwenye ujenzi kwa mwaka ni zaidi ya milioni mbili na kwa miaka mitano itakuwa zaidi ya milioni kumi. Na kwa miaka hii mitano fedha zako zote zitakwenda kwenye ujenzi ambao utakuwa hauzalishi kwa kipindi hiko, huku ukiamini kwamba nyumba ikikamilika ndio utaweza kufanya vizuri biashara.
Pia ujenzi huu wa muda mrefu utatumia muda wako mwingi kufikiria ujenzi na hivyo kushindwa kufikiri zaidi kuhusiana na biashara au fursa nyingine.
Kama ungetumia fedha hizi ulizowekeza kwenye biashara na kwa kipindi hiki cha miaka mitano ungekuwa umefikia mafanikio makubwa sana kwenye biashara na utaweza kujenga nyumba yako kwa wakati mfupi zaidi. Unaweza kujifunza kutoka kwa John jinsi alivyoweza kuanza na mtaji wa milioni 4 na kufikia milioni 100 ndani ya miaka mitatu. bonyeza maandishi hayo kusoma.
Kutumia nyumba kama dhamana ya kupata mkopo wa kuanzia biashara.
Kama tulivyoona kwa msomaji mwenzetu hapo juu na hata kwa wengi tunafikiria kwamba tukishakuwa na nyumba itakuwa rahisi kwetu kupata mkopo kwenye taasisi mbalimbali. Ni kweli nyumba itakusaidia kupata mkopo ila sio mkopo wa kuanzia biashara. Taasisi nyingi za fedha hazitoi mkopo kwa mtu ambaye anakwenda kuanza biashara hata ungekuwa na dhamana kubwa kiasi gani. Hii ni kwa sababu unapokwenda kuanza biashara hujui vitu vingi na hivyo kuna changamoto nyingi sana ambazo kama usipokuwa imara zinaweza kukurudisha nyuma. Ndio maana inashauriwa kuanza biashara na akiba zako kwanza na pale unapokuwa umeshaielewa vizuri, angalau miezi sita ndio uchukue mkopo ili uweze kuikuza zaidi.
Hivyo kikubwa hapa ni wewe kuamua kama kweli unataka kufanya biashara na kufikia mafanikio makubwa wekeza fedha na muda wako ulionao sasa kwenye kukuza biashara yako. Ikishakua utakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuweza kujenga au hata kununua nyumba iliyokamilika.
Nakutakia kila la kheri katika mafanikio ya biashara yako.
Karibu kwenye KISIMA CHA MAARIFA, mwezi huu wa tisa tutakuwa na SIKU 30 ZA MAFANIKIO ambapo utajifunza misingi muhimu ya kufikia mafanikio makubwa. Bonyeza maandishi haya kupata UTARATIBU WA KUJIUNGA NA KISIMA CHA MAARIFA
TUKO PAMOJA.
Kama kuna chamngamoto yoyote inayokuzuia kufikia mafanikio na ungependa kupata ushauri bonyeza maandishi haya na ujaze fomu. Hakuna malipo yoyote.
Nyumba na biashara ni vitu tofauti kumbuka biashara ina vitu viwili kufanikiwa au kupata hasara ukipata hasara umepoteza vyote lkn ukijenga unapoteza pesa unapata nyumba halafu unaendelea kutafuta kwa wakati mwingene
LikeLike
Ni kweli kabisa kwamba nyumba na biashara ni tofauti. Na kama umesoma na kuielewa vizuri makala nimeshauri kwamba kama mtu ana mpango wa kufanya biashara ni heri asijenge nyumba kwanza kwa sababu ujenzi unatumia muda mwingi sana na utatumia fedha nyingi sana. Labda iwe anaweza kujenga kwa mara moja.
Ila kama mtu hana mpango na biashara, kujenga ni muhimu zaidi kwake.
LikeLike
Nimeelewa sana na hii imenivusha ktk pointi nyingine ni kitu kilichokuwa kigumu sana kwangu. Ila kwa maelezo Haya na stori hii nimepata kitu. Good work. Kikubwa ni uamuzi sababu nafanikio ya MTU au kutokufanikiwa kumefungwa ktk maamuzi ya MTU mwenyewe.
LikeLike
Asante sana.
LikeLike