Mabadiliko makubwa duniani yameletwa na wajasiriamalia au watu wenye mawazo ya kijasiriamali. Hii ni kwa sababu watu hawa wanakuwa na mawazo tofauti ukilinganisha na watu wengine kwenye jamii. Wajasiriamali wanaiona dunia tofauti na ile inayoonekana na watu wengine na ndio maana huja na ugunduzi unaobadili maisha ya watu wengi sana.

Katika ujasiriamali kuna wajasiriamali ambao wanamafanikio makubwa sana kwenye kile wanachofanya. Na pia kuna wengine wana mafanikio ya kawaida au hata hawana mafanikio kabisa. Ni kitu gani kinawatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa kwenye ujasiriamali? Leo tutaona sifa tatu za wajasiriamali waliofanikiwa sana na jinsi unavyoweza kuzitumia ili na wewe uweze kufikia mafanikio makubwa. Sifa hizi ziko wazi kabisa na unaweza kujifunza hata wewe na ukaweza kufikia mafanikio makubwa kwenye ujasiriamali.

  1. Wama udhubutu.

Wajasiriamali wenye mafanikio makubwa wana udhubutu wa kuanzisha mambo mapya ambapo hawana uhakika wa kufanikiwa. Pia wapo tayari kukutana na changamoto katika hayo wanayoanzisha na kuzivuka ili kuweza kufikia mambo hayo makubwa. Mara nyingi mambo haya makubwa yanatokana na ndoto kubwa wanazoota za kuibadili dunia. Na ndoto hii inakuwa haijafanyika au haina uhakika mkubwa wa kufanikiwa. Kwa vile wajasiriamali ni watu wakuchukua mazingira ya hatari wanakuwa na udhubutu wa kufanya yale wanayoota na yanakuwa na mafanikio makubwa.

Anza sasa kujenga udhubutu wa kutekeleza yale ambayo unayaona kwenye ndoto zako. Kma unaona kuna njia inaweza kuwasaidia watu na kufanya maisha yao kuwa bora zaidi anza kutekeleza ndoto yako hiyo. Utakutana na changamoto nyingi ila mwisho wa siku utafikia mafanikio. Ukiogopa kufanya jambo kwa sababu hakuna mwingine anayefanya au aliyewahi kufanya utaishia kuwa kawaida tu.

  1. Wana shauku kubwa.

Wajasiriamali wenye mafanikio makubwa wana shauku kubwa ya kufikia mafanikio, wana mtizamo chanya juu yao na biashara zao na pia wanajiamini kwa kile wanachofanya. Shauku hii ndio inawapa nguvu ya kuendelea hata mambo yanapokuwa magumu. Shauku hii ndio huwafanya kutaka kujifunza zaidi ili kuweza kuvuka changamoto wanazokutana nazo.

Jenga shauku kubwa kwenye kile unachofanya, kwanza kipende na jione unaweza kufikia mafanikio makubwa kwa kufanya kitu hiko. Kuwa na mtizamo chanya kwako mwenyewe na kile unachofanya. Baada ya hapo kifanyie kazi huku ukiendelea kujifunza kila siku ili ujue njia bora za wewe kuweza kufikia mafanikio makubwa.

  1. Wana uvumilivu.

Wajasiriamali wenye mafanikio makubwa wanauvumilivu mkubwa. Hawa ni watu ambao hawakati tamaa na kwao kushindwa sio chaguo lao. Wanajua katika safari ya ujasiriamali vikwazo ni sehemu ya safari, ila hawako tayari kukwamishwa na vikwazo hivyo. Wanajua kama wanaweza kuvumilia na kuvivuka vikwazo hivyo watakuwa wamejifunza mengi sana na watafikia mafanikio makubwa. Uvumilivu huu ndio unawawezesha kufikia mafanikio.

Kuwa mvumilivu katika safari yako ya ujasiriamali. Unapokutana na vikwazo usione kama huo ndio mwisho wa safari ila jua kama ukiweza kuvuka vikwazo hivyo utafikia mafanikio makubwa. Vikwazo vilivyopo kwenye safari hii ya ujasiriamali ndio vinawazuia wale ambao hawajajitoa kuwa wajasiriamali wasiweze kuvuka. Ila kama wewe umejitoa kweli vumilia na jifunze jinsi ya kuvuka changamoto unazokutana nazo. Utaweza kufikia mafanikio makubwa sana.

Hizi ndio sifa tatu za wajasiriamali wenye mafanikio makubwa. Kwa kuwa na wewe unategemea kufikia mafanikio makubwa anza kujijengea sifa hizi na taona mabadiliko makubwa kwenye ujasiriamali na maisha kwa ujumla. Mafanikio yoyote uliyonayo sasa sio mwisho wa mafanikio, jua unaweza kufikia mafanikio zaidi ya hapo. Na kama utajenga sifa hizi tatu ulizojifunza leo safari yako ya ujasiriamali itakuwa rahisi zaidi.

Nakutakia kila la kheri katika mafanikio ya biashara na ujasiriamali.

TUKO PAMOJA.