Tajiri mmoja wa kihindi aliulizwa aeleze ni kitu gani kimoja ambacho kimumwezesha kufikia mafanikio makubwa sana na kuweza kuwa tajiri sana kupitia biashara anayofanya? Alijibu “mimi ndio nguvu kubwa ya mafanikio yangu, kumfanyia kazi mtu mwingine unarudishwa nyuma au kulazimishwa kufanya kazi chini ya kiwango chako”
Nafikiri kila mmoja wetu anaelewa nini alikuwa anamaanisha hapo. Unapofanya kazi ya kuajiriwa unalazimika kufanya kazi kulingana na majukumu uliyopangiwa au kulingana na ufanisi wa walio juu yako au walio chini yako. Ni vigumu sana kuweza kutumia uwezo mkubwa ulioko ndani yako na hata ukiutumia bado unaweza usionekana au kujaliwa. Watu wengi unaokuwa unafanya nao kazi wameridhika na kazi hizo na hivyo kuendelea kuvuta muda mpaka watakapostaafu na kuanza kupata mafao.
Kwa wewe ambaye una matamanio na mipango mikubwa ya kufikia mafanikio makubwa watu wa aina hii watazima kabisa ndoto zako kama utaendelea kuwa nao muda mrefu. Unakumbuka tulisema maisha yako ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka? Hivyo kama wafanyakazi wenzako wenye fikra hizo wanaweza kukufanya na wewe usahau ndoto zako. Ni mara ngapi umewahi kujaribu kufanya kazi vizuri au kwa uaminifu ila wafanyakazi wenzako wakakuona una kiherehere au unajipendekeza? Hivyo ndivyo wanavyoweza kufanya na kwa ndoto zako pia.
Unaweza kufanya nini ili kuanza safari yako ya kuelekea kwenye utajiri?
1. Je uanze biashara?
Huenda umeshajiuliza swali hili mara nyingi sana kama bado upo kwenye ajira. Je umewahi kukaa chini na kufikiri kwa kina ni jinsi gani utafanya hivyo na lini utaanza ili uweze kuondoka kwenye matatizo ya ajira.
2. Maswali sita muhimu ya kujiuliza.
Jiulize maswali haya kama bado umeajiriwa na yatakupa picha ya kazi unayofanya sasa na malengo yako ya mbeleni.
Je kazi yako ya sasa inakuridhisha?
Je kuna nafasi ya wewe kupandishwa cheo?
Je kama ukipandishwa cheo itakusaidia kufikia malengo yako?
Je utaweza kupata kazi unayopendelea zaidi kama utaendelea kufanya kazi unayofanya sasa?
Je kazi yako inakupa nafasi ya kuonesha uwezo mkubwa ulioko ndani yako?
Je unafurahia kazi unayoifanya?
Kama umejibu hapana kwenye swali lolote hapo juu anza kufikiria jinsi ya kuondoka kwenye kazi hiyo unayofanya kwa sababu kuendelea kuifanya kutafanya maisha yako yawe magumu.
3. Je ufanye biashara gani?
Kama umeshafanya tathmini na kuona kazi yako ya sasa haiwezi kukufikisha kwenye ndoto zako, njia mojawapo ya wewe kufikia ndoto zako ni kuingia kwenye biashara. Sasa swali linakuja je ufanye biashara gani?
Jiulize mzswali haya matatu ambayo yatakusaidia kujua ni biashara gani unaweza kuanzisha na kufanikiwa.
a) Ni aina gani ya biashara unapendelea kufanya? Ni kitu gani unakipenda sana ambacho unaweza kukifanyia biashara.
b) Ni biashara gani ambacho unaweza kukifanya kwa ubora wa hali ya juu? Iwe unataaluma nacho au kipaji chako.
c) Ni biashara gani ambayo ina hitaji kubwa au kuna soko kubwa?
Tafuta biashara ambayo itakuwa na sifa hizo tatu. Utaweza kufikia mafanikio makubwa sana kama utafanya biashara ambayo unaipenda au unashauku nayo kubwa, ambayo una uwezo mkubwa wa kuifanya na ambayo tayari ina soko katika eneo unalopanga kuifanyia.
Unaweza kuanzisha biashara yoyote kwenye eneo lolote kama itaweza kuwa na sifa hizo tatu. Ukiweza kufanya biashara inayotokana na hayo huna haja ya kuogopa kuhusu ushindani maana utakuwa hushikiki.
4. Ahadi ya kufanikiwa.
Moja ya nguvu kubwa itakayokuwezesha wewe kufikia mafanikio makubwa kwenye biashara unayofanya ni kujitoa kwa ajili ya mafanikio. Jiahidi kwamba lazima utafanikiwa na amini bila ya kutetereka kwamba hiki ndio kitakachotokea. Usifikiri kwamba itatokea kwa bahati, jiwekee ahadi na jitoe kwa ajili ya kufikia mafanikio makubwa. Jiambie ni lazima utafikia mafanikio hata kama kutakuwa na kikwazo gani. Jiahidi kwamba hutoshindwa au hutokubali kushindwa. Jiahidi kwamba hutorudi nyuma na wala hutomfanyia tena mtu kazi. Ni lazima uamini kila kitu kuhusu wewe na ujiamini ili uweze kufikia mafanikio makubwa.
5. Yatambue malengo yako.
Watu wengi hupelekwa tu kwenye maisha bila ya kuwa na malengo yoyote makubwa. Hujikuta wanapelekwa tu na kazi au ugumu wa maisha bila ya kujua wafanye nini ili kujiondoa kwenye matatizo waliyonayo. Hii ndio sababu kubwa watu wengi hawana furaha na wamekosa mafanikio kwenye kazi zao na hata maisha kwa ujumla.
Kuna malengo ambayo binadamu wengi tunayo na yanafanana. Kila mtu anapenda kuwa tajiri au kuwa na uhuru wa kifedha, kila mtu anapenda kuwa na furaha kwenye maisha. Kila mtu anapenda kuwa na usalama, kila mtu anapenda kuwa na familia bora na watoto wenye furaha na wanaopata elimu nzuri. Kila mmoja wetu anataka kuishi maisha yenye maana kwake na kwa wale wanaomzunguka
Yote hayo yanawezekana kwako na kwa mtu yeyote kama atachukua hatua ya kuweka malengo na mipango ya kuyafikia. Pia ni muhimu kufanyia mipango yako kazi na kujitoa kweli kwa ajili ya kufikia mafanikio makubwa.
Weka malengo ya kifedha.
Ili kuweza kuwa tajiri na kufikia uhuru wa kifedha ni muhimu kuweka malengo ya kifedha. Watu wengi wanakwenda kazini kila siku wakiishia kupata mshahara ambao hauwatoshi hata kutimiza mahitaji yao. Wanaishia kuamini kwamba labda mwaka kesho mambo yatakuwa mazuri zaidi hivyo hawafanyi chochote na maisha kuendelea kuwa magumu.
Wewe usiwe kama watu hawa. weka malengo ya kifedha, jua ni kiasi gani unataka kutengeneza kila mwaka ili uweze kufikia utajiri au uhuru wa kifedha. Kwa mfano kama unataka kutengeneza milioni mia moja kwa mwaka, kila mwezi inabidi utengeneze milioni tisa na kila siku inabidi utengeneze laki tatu. Kama unafanya kazi masaa kumi kwa siku inabidi kila saa utengeneze elfu thelathini. Sasa weka mipango kwamba kila saa yako moja itagharimu tsh elfu 30 na hivyo usipoteze muda wako kwenye kitu ambacho hakikupatii fedha hiyo.
Utakapoanza kufikiria jinsi ya kutengeneza fedha nyingi zaidi utaona njia nyingi za kutengeneza fedha na utaanza kupata fedha nyingi. Unaweza kuona kama ni maajabu ila sio maajabu makubwa kwa sababu yote yalikuwa ndani ya mawazo yako sema ulikuwa hujajua jinsi ya kuyatumia vizuri.
Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa. Karibu kwenye FORUM YA SIKU 30 ZA MAFANIKIO ili tuweze kuendelea kujadiliana.(bonyeza hayo maandishi kuingia kwenye mjadala)
TUKO PAMOJA.