Kama nilivyoahidi kila jumatano ya mwezi huu wa tisa tutakuwa tunawaletea makala maalumu ya kujadili uhusiano kati ya mafanikio na uchawi.

Katika nchi yetu kila siku tunasikia matukio mbalimbali ya kishirikina au kichawi. Tumekuwa tukisikia na kushuhudia matukio ya mauaji ya vikongwe. Pia tumekuwa tukishuhudia na kusikia mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi(albino).

UCHAWI1

Pamoja na matukio haya kumekuwa na hadithi nyingi sana huku mitaani kwamba baadhi ya watu waliofanikiwa au maarufu ni kwa sababu wametumia uchawi. Tumekuwa tukisikia kwamba wasanii maarufu na hata matajiri wakubwa wanawezeshwa na waganga au wamejiunga na freemason. Hapa freemason ikichukuliwa kama kikundi cha watu ambao wanajihusisha na imani za kishirikina.

Swali ni je mambo yote haya yana ukweli? Je uchawi unaweza kuleta mafanikio?

Jibu ni hapana, uchawi hauwezi kumletea mtu yeyote mafanikio, bali mtu mwenyewe ndio anaweza kujiletea mafanikio. Nafasi ya uchawi katika mafanikio ya mtu ni kumpa imani isiyotetereka kwamba anaweza kufanikiwa. Kwa imani hii mtu anafanya kila anachoweza ili afikie mafanikio makubwa ambayo amehakikishiwa kwamba kupitia uchawi anaweza.

Hii inafanyaje kazi kwa binadamu?

Akili ya kila binadamu inaweza kugawanywa kwenye sehemu tatu, kuna akili inayofikiri na kufanya maamuzi(conscious mind), kuna akili inayopokea na kutoa kila unachofikiri ila haifanyi maamuzi(subconscious mind), na kuna akili yenye kuongozwa kwa imani(superconscious mind).

Katika mafanikio na hata imani nyingine sehemu kubwa inayoathiri maisha yetu ni subconscious. Akili hii haiwezi kutofautisha kati ya mema na mabaya, yenyewe inapokea kila kitu kinachoingizwa(kwa mfumo wa mawazo) na kutoa vitu hivyo katika maisha ya kawaida. Ndio maana mtu anayefikiria kuumwa kila mara hupata ugonjwa kweli. Mtu anayezungumzia ajali kila mara huishia kupata ajali. Na mtu anayefikiria mafanikio kila mara huishia kupata mafanikio. Hii ni kwa sababu akili hii huvuta yale ambayo unayafikiri kila mara na kuyaleta kwenye maisha yako.

Kama ni kufikiria tu mazuri kwa nini kila mtu hafanikiwi?

Kama tulivyoona ni kwamba akili hii inapokea chochote kinachowekwa, haiwezi kutofautisha mema au mabaya. Mawazo yakishaingia yenyewe inayafanyia kazi na kukuletea yale mazingira. Sasa inawezekana umeshawahi kufikiria sana kuhusu kufanikiwa na akili yako ikaanza kukutengenezea mazingira hayo, baadae ukaingiza tena mawazo ya kushindwa, au wasiwasi hivi nitaweza kweli, au kusikiliza wanaokukatisha tamaa kwamba huwezi. Akili yako inachukua mawazo haya pia na kuandaa tena mazingira ya kushindwa. Hivyo unajikuta huwezi kufikia mafanikio kwa sababu huna uhakika na kitu kimoja unachokitaka.

Nini kinatokea kwenye uchawi au imani nyingine?

Kwenye uchawi au imani nyingine kinachotokea ni kwamba mtu anaaminishwa kwamba kwa kitu fulani atakachofanyiwa ni lazima atapata mafanikio makubwa. Kwa mfano mtu anaambiwa ukiwa na hirizi hii utapata chochote unachotaka. Mtu huyu anatembea na hirizi yake akiwa na uhakika asilimia mia moja kwamba atafikia mafanikio anayotaka, na kweli inatokea hivyo. Kilichompa mafanikio sio hirizi ila ile imani yake na mawazo kwamba lazima atafanikiwa kitu ambacho angeweza kukifanya hata bila ya hirizi.

Kwa wale wafuasi wa dini kuna miujiza mingi sana inatokea kwenye dini na imewahi kutokea. Miujiza yote hii inatokana na imani za watu kwamba wanaweza kupona, wanaweza kufikia mambo makubwa.

Hapa nimegusia machache sana na kwa juu ili upate picha ya jinsi gani mambo haya yanakwenda, unaweza kuendelea kujifunza zaidi ili kupata elimu ya ndani sana. Lakini ukweli ndio huu tuliozungumzia hapa.

Wiki ijayo tutaona ni jinsi gani masharti wanayopewa watu kwa waganga yanaweza kuwasaidia kufikia mafanikio makubwa wakati waganga wenyewe wana maisha magumu.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa, usidanganywe kwamba uchawi ndio maajabu ya wewe kufanikiwa, maajabu unayo mwenyewe kwenye kichwa chako. Anza kuyatumia sasa na AMKA MTANZANIA ni uchawi tosha kwako wa kuweza kukuandaa kimawazo na kisaikolojia ili uweze kufikia mafanikio makubwa.

Karibu pia kwenye KISIMA CHA MAARIFA ambapo huko ndio uchawi mkubwa zaidi utakaofungua milango yako yote ya mafanikio na kuanza kuwa na mtizamo mpya utakaokufikiasha kwenye mafanikio makubwa.

TUKO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.