Katika moja ya maswali ambayo huwa napata kutoka kwa wasomaji wengi ni mtu afanye ujasiriamali wa aina gani? Au wengine huuliza nina kiasi fulani cha mtaji, naomba unishauri nifanye biashara gani? Hili ni swali ambalo linawasumbua watu wengi sana na kukosekana kwa ushauri mzuri kumewafanya watu wengi kufanya maamuzi ambayo sio sahihi na kujikuta wakipata hasara au kushindwa. Leo katika makala hii tutachambua taratibu ni biashara au ujasiriamali wa aina gani unaweza kufanya na ukafikia mafanikio makubwa.
Jibu la swali kwamba nifanye biashara gani haliwezi kuwa sawa kwa watu wote. Jibu la swali hili linategemea na mtu na ili kuweza kupata jibu la swali lako wewe mwenyewe unatakiwa kujiuliza na kujipa majibu sahihi maswali haya matatu;
- Ni kitu gani unapendelea kufanya?
Katika maisha yako kuna vitu fulani ambavyo unavipenda sana au unapendelea kufanya. Inawezekana unapenda mitindo, inawezekana unapenda michezo, inawezekana unapenda magari au kusafiri na kadhalika. Kwa kuangalia mambo haya unayopenda sana kufanya unaweza kufikiria ni jinsi gani unaweza kuyageuza kuwa biashara. Kwa mfano kama unapenda sana kusafiri unaweza kuanzisha biashara ya usafirishaji. Kama unapenda sana mifugo au wanyama unaweza kuanzisha biashara ya ufugaji. Ni vizuri sana kufanya biashara unayoipenda kwa sababu utakuwa na shauku ya kujifunza zaidi na hutokata tama mapema hasa mambo yanapokuwa magumu.
- Una uzoefu au taaluma gani?
Swali hili ni muhimu na litakuwezesha kujua kitu ambacho unaweza kukifanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Kumbuka ili kufikia mafanikio kwenye jambo lolote ni lazima uweze kufanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Kama kuna kitu ambacho umekisomea na una taaluma nacho ni dhahiri kwamba kuna mambo mengi sana ambayo unayajua kuhusu kitu hiko. Na kama una uzoefu wa kitu au jambo fulani ni rahisi kwako kufikia mafanikio kwenye kulifanya kuliko anayeanzia mwanzo kabisa. Hivyo fikiria ni vitu gani umevipata kupitia taaluma yako na angalia ni jinsi gani unaweza kuvitumia kwenye ujasiriamali na biashara. Pia jiulize ni uzoefu gani ambao tayari unao na jinsi gani unaweza kuutumia kwenye biashara unayoweza kuanzisha. Kwa mfano kama umeajiriwa kwenye kampuni ya wanasheria hii inamaana kwamba tayari wewe una taaluma ya sheria na pia una uzoefu wa kuendesha kesi, kutafuta wateja na hata uendeshaji wa kampuni. Unaweza kutumia taaluma yako hii na uzoefu ulioupata kwenye kampuni uliyofanyia kazi na kwenda kuanzisha kampuni yako mwenyewe ambayo itakupatia mafanikio makubwa sana kama ukiweza kuisimamia na kuiendesha vizuri.
- Ni kitu gani ambacho kina uhitaji mkubwa.
Swali la tatu na muhimu kujiuliza ni kitu gani ambacho kina uhitaji mkubwa kwa eneo ambalo unafikiri kufanyia biashara. Angali ni kitu gani ambacho tayari kina soko au unaweza kukitengenezea uhitaji ili uweze kupata wateja pale utakapoanzisha biashara yako. Pia angalia ni jinsi gani unaweza kulifikia soko hilo kulingana na bidhaa au huduma ambayo unatarajia kuitoa.
Kama ukiweza kujiuliza na kujipa majibu sahihi kwenye maswali hayo matatu utapata aina nzuri ya biashara ambayo utaifanya kwa moyo na utaweza kufikia mafanikio makubwa. Njia nzuri ya kufanya hivi ni wewe kuchukua kalamu na karatasi kisha kuorodhesha vitu vyote vinavyohusiana na maswali hayo matatu na kisha kuoanisha na kuona ni kitu gani ambacho kinaweza kuingia kwenye sehemu zaidi ya moja.
Usichukue ushauri wa biashara kwa sababu tu kwamba watu wengi wanafanya au inaonekana kulipa. Ni muhimu biashara utakayokwenda kufanya iwe inatoka ndani yako kweli ndio utaweza kufikia mafanikio makubwa kupitia biashara hiyo.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.
TUKO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI
kaka habari za asubuh.ndugu Yang mimi napenda sana kufannya na kumiliki biashara mbalimbal.ila kipengele cha taaluma/uzoefu ndio kinanpga chenga ndio maana tunaulizia kwenu wazoefu I’ll mtuambukize maarfa.naomba mschoke kutufundsha.mungu na azd kukufunulia hekma
LikeLike