Mafanikio yako wewe kwenye ujasiriamali yanatokana na mambo mengi sana. Moja ya jambo muhimu litakalokuletea mafanikio makubwa ni kulijua soko lako vizuri na jinsi ya kulifikia soko hilo. Na ili kufanikiwa kwa kiwango kikubwa sana unatakiwa uweze kulitawala soko kwa kiwango cha kutosha kuifanya biashara yako ipate faida kubwa na kuendelea kukua.

Kabla ya kuingia kwenye ujasiriamali ni lazima ufanye utafiti mdogo kuhusu soko la bidhaa au huduma unayopanga kutoa. Hii kila mtu hufanya ila ni wachache sana ambao wanafanya kwa kiwango kizuri ambacho kitawawezesha kupata taarifa sahihi kuhusu soko lako. Leo nitakushirikisha maswali matatu muhimu ya kujiuliza wakati unafanya utafiri wa soko la bidhaa au huduma yako.

1. Je kuna soko?

Hili ni swali la kwanza kabisa kwa kila mjasiriamali au mfanyabiashara kujiuliza kabla ya kuingia kwenye biashara husika. Utakuwa mtu wa ajabu sana kama utaamka na kuanza kuuza bidhaa au huduma ambayo hujui kama kuna mtu yuko tayari kuinunua. Hatua hii muhimu kila mtu anaipitia ila watu wengi huishia hapa tu. Wakishauliza na kuona soko lipo wanafikiri tayari wanaweza kuingia na kufanya biashara. Endelea kusoma mambo mengine muhimu unayohitaji kujiuliza wakati wa kufanya utafiti wa soko.

Katika kujiuliza kuhusu soko ni muhimu pia kujua soko lako ni lipi yaani wateja wako ni watu gani. Jua umri wao, hali zao za maisha, kipato chao na hata tabia zao katika maisha kwa ujumla. Hii itakuwezesha kutoa bidha au huduma yako kwa njia itakayoweza kuwafikia vizuri.

2. Je soko lina ukubwa wa kutosha.

Baada ya kujua kwamba soko lipo swali la pili na muhimu sana kujiuliza ni je soko hilo lina ukubwa wa kutosha. Yaani watu hao ambao wako tayari kununua bidhaa au huduma zako wanatosha kununua kiwango kikubwa kitakacokuwezesha kurejesha gharama na kukupatia faida? Usipojiuliza swali hili utaingia kwenye biashara ambayo umeona ina soko kumbe soko hilo halitoshi wewe kuweza kuendelea kukua zaidi. Kwa mfano kama unataka kuanzisha duka la vifaa vya ujenzi kwenye eneo ambalo hakuna makazi mapya yanayojengwa, soko linaweza kuwepo ila sio kubwa sana kutosha kurudisha gharama zako na wewe kupata faida.

3. Je soko lina mkusanyiko wa kutosha?

Hili ni swali muhimu sana ambalo watu wengi sana huwa hawajiulizi. Unaweza kukuta kweli bidhaa au huduma unayotoa au unayotaka kutoa ina soko na soko lina ukubwa wa kutosha kurudisha gharama zako na kukuletea faida. Ila kuna swali muhimu la kujiuliza ambalo ni je soko lina mkusanyiko wa kutosha? Hapa namaanisha kwa jinsi unavyofanya biashara yako unaweza kulifikia soko lako kwa urahisi kwenye eneo unalofanyia biashara? Unaweza kuwa na biashara ambayo wateja wako mbalimbali sana kiasi kwamba gharama za kuwafikia wateja hao zikawa kubwa sana na hivyo kukufanya ushindwe kupata faida ya kutosha kuifanya biashara yako ikue. Kwa mfano unauza vifaa vya wakulima wa zao fulani ila wakulima hao wamesambaa nchi nzima na kila mkoa wako wachache sana. Gharama ya kuwafikia wakulima hawa inaweza kuwa kubwa sana ukilinganisha na faida unayopata.

Jiulize maswali haya matatu ili uweze kulifikia soko lako vizuri na kuweza kupata mafanikio makubwa kupitia ujasiriamali. Jua soko lako ni lipi na lijue soko hilo vizuri, baada ya hapo jua ukubwa wa soko lako na kama ukubwa huo utakuwezesha wewe kupata faida na kukua zaidi. Baada ya kujua haya pia jua kama soko lako lina mkusanyiko wa kutosha kwa wewe kuweza kulifikia na ukapata faida ya kuweza kukuza biashara yako zaodi.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.

TUKO PAMOJA, TUTAKUTANA KILELENI.