Kama Unaendelea Kuamini Hivi Katika Maisha Yako, Sahau Kuhusu Mafanikio.

Chochote kile unachoamini katika maisha yako uko sahihi. Kama unaamini utafanikiwa na hatimaye kuwa tajiri hilo sawa, kama unaamini wewe ni mtu wa kushindwa siku zote na una mikosi na laana hilo nalo sawa kwako, kwani utapata kile unachofikiria na kukiamini ndicho kitakachokuwa chako.
 

Ili uweze kufanikiwa kwa ngazi yoyote ile unayotaka imani ni kitu muhimu sana katika maisha yako, ingawa inategemea wakati mwingine unaamini nini, kushindwa au kufanikiwa zaidi. Kwa hiyo unaona kuwa jinsi mtu anavyozidi kuamini juu ya mafanikio katika maisha yake , hujikuta ndivyo anavyomudu kufanikiwa.
Na kwa jinsi mtu anavyozidi kuamini kushindwa ndivyo hujikuta anakuwa ni mtu wa kushindwa karibu siku zote. Kwa vyovyote vile iwavyo imani ni muhimu sana kukufikisha pale unapotaka kufika kama imani unayoamini iko sahihi. ( Soma pia Hii Ndiyo Imani Unayotakiwa Kuwa Nayo Ili Kufanikiwa )
Unapojikuta unaamini sivyo ndivyo juu ya mafanikio inakuwa ni ngumu sana kwako kufanikiwa. Kama zilivyofikra ambazo zinaweza kuturudisha nyuma katika maisha yetu, hali kadhalika zipo imani, ambazo kama tukiziendekeza na kuzitumia katika maisha yetu ujue hakuna mafanikio.
  
Zipo imani nyingi ambazo wengi wetu huziamini ambazo huturudisha nyuma pasipo kujua, lakini moja ya imani hizo ni kuamini kwamba kuwa na mafanikio inategemeana na ‘bahati’  hii ndiyo imani inayokukwamisha sana katika maisha yako na kama unaendelea kuamini hivi katika maisha yako, sahau mafanikio. 
Inakuwa inakera na inauma kwa wengi wetu wanapoamini mafaniko ni bahati. Kwa kawaida, mtu anapozungumzia bahati kwenye mafanikio, anakuwa na maana kwamba, mwenye mafanikio hayo ana mchango mdogo sana au hana kabisa kwenye kuyapata, zaidi ya kutegemea hiyo bahati iliyopelekea mtu huyo kufanikiwa.
Hata pale mtu anapopata mafanikio ya kushinda fedha nyingi kwenye bahati nasibu, bado kitendo cha kwenda mahali wanapouza tiketi za bahati nasibu, kwa kuamini kwamba, atapata, kutoa fadha na kununua tiketi, hakuhusiani na bahati, bali zaidi, ni nia na utendaji wa mtu binafsi ndiyo uliomfanikisha.
Kwanini hutokea mara nyingi tunapozungumzia mafanikio fulani ya mtu, tusiseme ukweli mkubwa zaidi kuhusu mafanikio hayo na badala yake kuyashusha na kuyapa kibandiko cha bahati? Kwanini tusiwe wakweli kwa kutaja juhudi, uvumilivu, na sifa nyingine? Labda ni kwa sababu mara nyingi tunataka kupata matunda au mazao ya haraka bila jasho lolote.
Hivyo, kusema mafanikio ni bahati ni moja ya njia ya kujipa moyo kwamba, huenda hata sisi tutapata mafanikio hayo, kwa kasi ya kufumba na kufumbua kwa sababu ni suala la bahati zaidi kuliko sifa nyingine. Pengine kitu usichokijua wale wenye mafanikio kwenye mambo yao, kilichowaongoza hadi kufikia mafanikio ni dira, dhamira, juhudi pamoja na uvumilivu.
Wengi tumekuwa tunaogopa au hatuko tayari kukubali kirahisi kwamba, dira, juhudi, nia na kupania pamoja na sifa nyingine za aina hiyo, ndizo zitakazo au zinazomwezesha mtu kufikia mafanikio anayoyataka katika maisha yake na sio kinyume chake kama wengi wanavyoamini katika suala zima la bahati.
Kutokana na wengi kuiamini bahati, hujikuta maisha yao yote ni watu wasiofanya juhudi  sana katika maisha, bali maisha yao yamekuwa ni ya kuangalia na kutaka njia za mkato ikiwemo na kutaka bahati ije, hata kama ni kwa muujiza. Unapoishi na kuendelea kuamini kitu hiki kinachoitwa bahati inakuwa ni ngumu sana kufanikiwa.
Huwa ni rahisi sana mtu kujikuta kusema, fulani kafanikiwa kwa sababu ana bahati, kuliko kujiambia, nitajaribu na kujitahidi kufuata njia aliyofuata hadi nami nipate mafanikio. Kwa wale wanaoamini sana bahati ni kila kitu, mara nyingi huwa hawataki sana kuumia katika kutafuta mafanikio, zaidi ya kukaa na kusubiri bahati ije upande wao.
Tukumbuke kwamba, wakati watu wengine wanapokuwa wakijishughulisha kutafuta mafanikio  mara nyingi huwa hawatupi taarifa zao. Kwa kuwa tunakuwa hatuwaoni, na tunachokuja kukiona ni mafanikio yao tu,  hivyo inakuwa rahisi kwetu kusema wana bahati. Na tunakuwa tumeshindwa kuona juhudi, nia , uvumilivu na kujua dira zao hadi wakafanikiwa.
Lakini, hata tunapowaona wengine wakiwa wanajishughulisha tokea chini kabisa, bado wanapofanikiwa, tunasema wana bahati. Tunaamini kwamba, kwa sababu walikuwa chini kabisa kule, bila kujali nia, dira, juhudi na sifa nyingine tunaamini kufika kwao huko juu bado ni suala la bahati.
Siku ukisikia mtu anaelezea mafanikio ya wengine au hata yake kama jambo la bahati tu, jua huyo hajui hasa anachokizungumza. Kwa juhudi zetu, wakati mwingine hata bila wenyewe kujua, ndipo tunapoweza kufanikiwa. Hakuna kitu kinachoitwa bahati katika mafanikio, utafaniwa tu kama utachukua uamuzi wa kufanikiwa na kuamini. 
Kwa kuamini na kuamua kufanya, hata kama ni kwa kujiambia bahati itakuwa upande wetu, na kitakachokuwezesha kufanikiwa siyo bahati, ni uamuzi wako binafsi wa kuyafikia maisha unayoyataka. Acha kuendelea kuamini kuwa mafanikio ni bahati, tenda vitu vitakavyoleta hiyo bahati katika maisha yako, matokeo chanya utayaona.
Nakutakia mafanikio mema na endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku kwa kujifunza zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAIMARIKE.
IMANI NGWANGWALU – 0767048035/ingwangwalu@gmail.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: