Karibu mpenzi msomaji kwenye kipengele cha kujenga tabia za mafanikio na mwezi wa kumi na wa kumi na moja tunajenga tabia ya kujiamini.

Kama tulivyoona kwenye makala zilizopita, kijiamini ni kiungo muhimu sana cha kuweza kufikia mafanikio makubwa. Pia tuliona njia mbalimbali za kujijengea tabia ya kujiamini.

Leo tutajadili mazoezi unayoweza kuanza kuyafanya kwenye maisha yako na ikakuongezea kujiamini sana. Hivi ni vitu ambavyo unaweza kuanza kujifunza leo na ukaleta mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako.

1. Pendelea kukaa viti vya mbele.

Kama umewahi kuchunguza kwa makini sehemu yoyote ambayo ina mkusanyiko wa watu ambao wanakaa kwenye viti, watu wengi hupendelea kukaa viti vya nyuma. Maeneo kama shuleni, kumbi za mikutano, sherehe na hata nyumba za ibada watu wengi hupendelea kukaa viti vya mwisho. Unaweza kuona ni kitu cha kawaida au ni mazoea tu ila inaonesha ni jinsi gani watu wengi hawajiamini. Na wale wanaopenda kukaa mbele mara nyingi huwa ni watu ambao wanajiamini.

Hivyo kuanzia leo, pendelea kukaa viti vya mbele katika sehemu yoyote ambayo utakuwepo. Hii itakuongezea kujiamini, mwanzoni unaweza kuona aibu ila utakavyofanya mara nyingi utaona ni kitu cha kawaida.

2. Angalia watu machoni.

Kama unazungumza na mtu au watu, waangalie machoni, hii ni njia nzuri sana ya kujijengea kujiamini. Mara nyingi watu huzungumza huku wakiangalia chini au kuangalia pembeni. Hii ni dalili ya kukosa kujiamini.

Kuanzia sasa kila unapozungumza na mtu muangalia machoni moja kwa moja itakufanya uweze kuzungumza kwa kujiamini na kueleweka vizuri pia. Mara nyingi watu wanaokwepa kuangalia machoni wakati wanazungumza wanakuwa hawajiamini au wakati mwingine wanakuwa wanadanganya.

3. Tembea haraka kidogo.

Kwa mwendo wako wa kawaida unaotembea ongezakasi kidogo kwa asilimia 25. Unapokuwa unatembea haraka inakuongezea kujiamini na unaonesha kwamba kuna kitu cha muhimu unawahi au huna muda wa kupoteza. Unapokuwa unatembea taratibu unaonesha kutokujiamini au hujali sana unakoelekea.

Kuanzia sasa unapotembea ongeza kasi yako kidogo na tembea kwa kujiamini. Hii itakujengea kujiamni na pia itatoa picha kwa wengine kwamba wewe unajiamini na una mambo muhimu unayokwenda kufanya.

4. Ongea, toa maoni yako.

Umewahi kuona kunakuwa na mkutano au kikao ambapo watu wachache wanazungumza na wengi hawazungumzi ila baada ya kikao watu wanaanza kusema pale bora ingekuwa hivi au ingekuwa vile? Hii yote inatokana na kutokujiamini. Mtu ambaye hajiamini anaogopa hata kutoa maoni yake au mawazo yake mbele za watu wengine. Kwa tabia hii anashindwa kuwa na mchango mzuri kwenye sehemu alipo.

Kuanzia sasa unapokuwa kwenye mkutano au kikao chochote na ikatolewa nafasi ya watu kutoa maoni yao, toa maoni yako. Sema chochote ambacho unaona kitakuwa kizuri au kitasaidia kuboresha zaidi. Kwa njia hii utajiamini zaidi na utaweza kutoa maoni yako sehemu mbalimbali.

5. Tabasamu.

Vaa tabasamu kubwa sana kwenye uso wako na hii itaondoa kutokujiamini na mashaka pia. Huwezi kuwa unajiona huna thamani au huna mchango wowote kisha ukatabasamu. Ila unapoanza kutabasamu utajiona kwamba ni muhimu na una mchango mkubwa kwa wengine.

Kwanzia sasa jijengee tabia ya kutabasamu. Hata pale unapokutana na wakati mgumu tabasamu kwanza, hii itakujengea kujiamini na kuweza kupambana na wakati huo mgumu.

Fanya mazoezi hayo kila mara ili ujijengee kujiamini zaidi. Kumbuka kujiamini ni nyenzo muhimu sana ya kufikia mafanikio.

Nakutakia kila la kheri katika safari ya kufikia mafanikio makubwa.

TUPO PAMOJA.