Kila mjasiriamali ana ndoto siku moja aweze kufikia mafanikio makubwa sana. Haijalishi ni kiwango gani cha mafanikio ulichofikia mpaka sasa, bado unahitaji kukua zaidi na kufikia mafanikio zaidi. Ndio maana hata wajasiriamali waliofanikiwa sana bado wanafanya kazi kwa juhudi na maarifa kila siku ili waendelee kufanikiwa zaidi.
Kama umejikuta tu kwenye ujasiriamali kwa sababu fulani ambazo zilikusukuma uwe mjasiriamali au mfanyabishara, huenda huzijui mbinu muhimu zitakazoweza kukuletea mafanikio makubwa. Leo tutajadili mbinu hizo muhimu na jinsi utakavyoweza kuzitumia ili kufikia mafanikio makubw akupitia ujasiriamali au biashara. Uzuri ni kwamba mbinu hizi hazihitaji kiwango fulani cha elimu, au kabila au rangi. Ni mbinu ambazo mtu yeyote mwenye nia ya kweli ya kufanikiwa kwenye ujasiriamali anaweza kuzitumia na akafikia mafanikio makubwa.
1. Fanya kitu ambacho unakipenda, fuata ndoto yako.
Tofauti ya ajira na ujasiriamali ni kwamba kwenye ajira unaweza kufanya tu kazi yoyote unayopangiwa kwa kuwa lengo lako kubwa ni mshahara. Ila ukifanya hivi kwenye ujasiriamali huwezi kufikia mafanikio. Kama utafanya ujasiriamali au biashara kwa sababu tu unapata faida safari yako itakuwa fupi sana. Chagua kufanya ujasiriamali katika kitu ambacho wewe mwenyewe unakipenda sana. Hakikisha kitu hiko kinakuwa ndoto yako kubwa na unaweza kuwa tayari kukifanyia kazi hata kama hakuna mtu anayekulipa. Ukifanya kitu ambacho unakipenda, kila siku utakuwa na hamsa kubwa itakayokufanya uwe mbunifu zaidi na kuweza kufikia mafanikio makubwa.
2. Fanya kwa ubora wa hali ya juu.
Chochote unachofanya kwenye ujasiriamali wako, fanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Toa bidhaa au huduma ambazo zitakwenda kubadilisha na kuboresha maisha ya wateja wako. Kwa njia hii utawaridhisha wateja wako na kukufanya uwe na wateja wengi sana. Kama utaishia kufanya kwa kawaida tu kama wengine wengi wanavyofanya sahau kuhusu mafanikio makubwa.
3. Amini kwenye kile unachokifanya.
Kama tayari unafanyia kazi kitu ambacho unakipenda na ambacho kipo kwenye ndoto zako, unahitaji kuamini katika kile unachofanya. Amini kwamba ni kitu ambacho kinaweza kuwasaidia watu wengi na weka ubora wako wote katika kitu hiko. Kwa kuamini hivi itawafanya wateja nao waamini na wakuamini wewe pia. Kwa njia hii watatatua matatizo yao na kuendelea kufanya biashara na wewe kwa muda mrefu. Haya yote yatakupelekea kufikia mafanikio makubwa sana.
4. Tengeneza timu imara.
Kwenye ujasiriamali huwezi kufanya kila kitu mwenyewe, labda kama huna mpango wa kukua zaidi. Ili uweze kukua na kufikia mafanikio makubwa unahitaji timu ya watu unaowaamini na wanaokuamini. Utakapoweza kujenga timu hii itakusaidia wewe kuweka nguvu kidogo na kupata mafanikio makubwa. Utatengeneza timu imara kwa kuajiri wafanyakazi wenye uwezo mzuri, kujadili nao majukumu yao na kuwafanya waweze kujiongoza wenyewe na kufanya maamuzi ambayo yatakuwa na faida kwenu wote. Ni muhimu kujenga utamaduni wa kifamilia katika ujasiriamali hivyo kila mfanyakazi anaona hiyo ni sehemu ya maisha yake.
5. Usikate tama.
Katika mambo yote tuliyojadili kutokukata tama ndio jambo muhimu sana. Kwa sababu kama utafanya hayo yote tuliyojadili hapo juu ila ukawa mtu wa kukata tama haraka huwezi kufikia mafanikio makubwa. Kuna vikwazo vingi sana kwenye safari ya ujasiriamali. Unaweza kuweka mipango mizuri sana ila kitu ambacho kipo nje ya uwezo wako kikavuruga mipango yako. Ni lazima uweze kuendelea na safari hata pale mambo yanapoonekana kuwa magumu. Hapa ndio utakapojifunza ni mambo gani unatakiwa kufanya vizuri ili uweze kufikia mafanikio makubwa.
Fanya mambo hayo matano na utaona mabadiliko makubwa snaa kwenye ujasiriamali au biashara unayofanya. Usidanganyike kwamba wewe huwezi kufikia mafanikio makubwa, unaweza kama utafuata njia zinazokupeleka kwenye mafanikio.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.
TUPO PAMOJA.
AHSANTE MUNGU AKUBARIKI
LikeLike