Kama Unafanya Kitu Hiki Mara Kwa Mara Katika Maisha Yako, Mafanikio Ni Yako.

Inaweza kuonekana kuwa ni kama jambo la kuchekesha labda, pale unapomwambia mtu aendelee kuvuta subira na kumsisitiza kwamba, baada ya muda atapata anachotafuta, atapata kile anachokitaka. Ni jambo lenye kuchekesha kwa sababu, huenda wakati unamwambia hivyo, ameshatimiza miaka 15 au zaidi akihangaikia kutafuta anachotafuta.
 

Kama ambavyo tumekuwa tukisema mara kwa mara katika mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwamba, kama mtu ameamua kutafuta mafanikio fulani na akitarajia kwamba yawe au yazae matunda mara moja, ni wazi kabisa atapata maumivu pale atakapoona ndoto zako hazijatimia.
Nimeanza hili kwenye suala zima la mafanikio, kwani huwa linatuumiza sana. Wengi wetu tunafanya jambo, tukitarajia mafanikio ya hapo kwa papo, yasipopatikana, tunaanza kuamini kwamba, tumeshindwa au tumekosea hata pale ambapo, hatuoni tulipokosea.
Nijuavyo mimi, mafanikio ni hatua. Inabidi tutembee hatua kwa hatua, tena wakati mwingine hata hatua za mtoto. Hatua za mtoto, siku baada ya siku, hatimaye kutufikisha mahali ambapo tulitaka kufika. Uzuri wa kutembea hatua kwa hatua ni ule uhakika wa kufika.( Unaweza ukasoma pia Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuwa Tajiri Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja )
Pamoja na kutembea hatua kwa hatua kuendea lengo letu la mtu, bado kuna suala zima kulalamika. Kanuni ya mvutano inasema maisha hurejesha kwetu kile tulichokiweka. Kwa kulalamika kutokana na shida na misukosuko ya maisha, tunakaribisha malalamiko na walalamikaji kufurika kwetu, badala ya mafanikio.
Mzee mmoja kijijini kwetu tukiwa wadogo alizoea kusema, ‘ngoja niende shamba nikaangalie mahindi ambayo sikuyapanda kama hayajaota’ wakati ule sikuweza kumuelewa, lakini sasa naelewa vema kile alichokuwa akimaanisha. Kama hufikirii au kutoamini katika jambo fulani, ina maana hujalipanda na hivyo, matarajio yako lazima yawe kutolivuna au kutolipata.
Wale watu wote waliofanikiwa kwenye mambo yao wanajua kwamba, suala sio kujua jinsi tundu liliovyopatikana kwenye mtumbwi, bali kuziba tundu kwanza. Lakini linakuwa tatizo sana kama nahodha wa mtumbwi atakwaa mwamba ule ule na mtumbwi kupata tundu kila wakati. Baada ya kuziba tundu, inabidi atafute chanzo au sababu ya kutoboka kwa mtumbwi.
Kwenye maisha tunatakiwa kutatua tatizo linapojitokeza kwa kujiuliza chanzo cha tatizo, badala ya kulalamika na kuacha kila kitu.( Soma Kama Unaendelea Kufanya Kosa Hili Katika Maisha Yako Utakufa Maskini ). Tukishajua chanzo cha tatizo, hilo haliwi tena tatizo, bali huwa shule. Kwa kutumia shule hiyo tunamudu kwa ubora zaidi na mafanikio yanakuwa makubwa zaidi.
Kuna jambo lingine ambalo nalo hushangaza pia. Hebu tujiulize kwa mfano, hivi inakuwaje mtu anasema, ‘Kama ningekuwa msomi, tajiri, mfanyabiashara mkubwa, askari, ingekuwa safi sana’halafu unajiuliza ina maana kuna siku taaluma au shughuli hizi ziligaiwa rasmi kwa watu wanaozifanya na huyu bwana anayezitamani, labda hakuwepo kwenye mgawo, ndiyo maana hakuzipata.
Jibu ni hapana, tena hapana kubwa sana. Ukweli ni kwamba wote hao walichagua, wakaamua kufanya. Ukweli ni kwamba wote hao walichagua, wakaamua kufanya. Wakati mwingine na mara nyingi, walipata shida na misukosuko na pengine kuwachukua muda mrefu kumudu. Tusipochagua wenyewe kuna kitu kingine kitatufanyia uchaguzi na ni wazi uchaguzi huo hautaupenda.
Kitu pekee unachotakiwa kujua, ni kufanya uchaguzi wa maisha unayotaka uyaishi. Huu ndiyo uchaguzi mkuu mhimu katika maisha yako. Ni lazima ujue unataka kutimiza nini katika maisha yako. Kama unafanya kitu hiki mara kwa mara katika maisha yako, mafanikio ni yako. Kumbuka waliofanikiwa wamechagua kufanikiwa, bila kujali vikwazo vilivyowazuia lakini walitoka.
Kwa ujumla, kuna sifa nyingine kadhaa mbaya zenye kutuzuia kufika kule tunakotamani kufika. Nimetaja hizo chache ili uweze kujiuliza maswali, kama nawe huna moja au mbili ama zote kati ya hizo, ili uweze kujirekebisha na kusonga mbele katika maisha yako.
Kumbuka kwamba, kila binadamu ameletwa hapa duniani kwa sababu maalum, kwa kusudi mahsusi, ndiyo maana tuna vipaji mbalimbali na tofauti. Kwa wale wanaochagua kwa makusudi na kufanya huku wakijifunza tena na tena, hatimaye kufanikiwa.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio.
TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI NGWANGWALU – 0713 048035/ingwangwalu@gmail.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: