Wewe kama mjasiriamali kuna wakati ambapo utahitaji fedha zaidi ili uweze kukuza biashara yako. Fedha hizi unaweza kuzipata kupitia mikopo inayotolewa kwenye taasisi mbalimbali za kifedha. Wiki iliyopita hapa kwenye KONA YA MJASIRIAMALI tulijadili umuhimu wa taasisi za kifedha katika maendeleoa ya ujasiriamali. Katika makala ile tuliona vigezo muhimu unavyotakiwa kuwa navyo ili uweze kupata mkopo wa kibiashara. Kuwa tuu na vigezo hivi bado hakutoshi kukufanya wewe uende ukachukue mkopo wa biashara.

Kuna mambo muhimu sana ya kuzingatia kabla ya kuchukua mkopo wa biashara. Kushindwa kuzingatia mambo haya imekuwa chanzo kikubwa cha wafanyabiashara wengi kupata hasara na hivyo kushindwa kulipa mikopo yao na biashara zao kuwa hatarini. Leo tutajadili mambo haya muhimu ya kuzingatia ili wewe kama mjasiriamali uweze kunufaika na mkopo utakaochukua badala ya mkopo huo kuwa hasara kwako.

Yafuatayo ni mambo muhimu unayotakiwa kuzingatia kabla hujachukua mkopo wa biashara.

Jambo la kwanza jua unachukua mkopo kwa ajili ya nini. Ukisema tu unachukua mkopo kwa ajili ya biashara kuna mambo mengi sana kwenye biashara, kuna kuongeza uzalishaji, kuna kuongeza mauzo na kuna kuongeza usambazaji. Ni muhimu kujua mkopo unaochukua ni kwa ajili ya nini ili uweze kutumia kwa sababu hiyo. Kama mkopo unaocukua ni kwa ajili ya kuongeza uzalishaji hiyo inamaanisha kwamba utatumia mkopo huo kununua bidhaa au mali ghafi zaidi, na pia kuongeza nguvu kazi zaidi. Kama mkopo unaochukua ni kwa ajili ya kuongeza mauzo hapo utauelekeza kwenye matangazo na ofa mbalimbali. Unapojua ni kipi hasa unachotaka kufanya na mkopo wako inakufanya uwe na nidhamu nzuri kwenye matumizi ya mkopo wako.

Jambo la pili muhimu ni kuujua vizuri mkopo kabla ya kuuchukua. Wafanyabiashara wengi, hasa wadogo wadogo wakishakubaliwa kupewa mkopo hufurahia sana na kuona mambo yameshakuwa mazuri. Wanasahau kwamba mkopo huo una riba na hivyo utalipa fedha nyingi kuliko ulizokopa. Ni vizuri kujua vizuri mkopo kabla hujakubali kuuchukua. Jua ni riba kiasi gani utatakiwa kulipa kwa kipindi utakachokaa na mkopo huo. Pia ni muhimu kuzingatia marejesho ya mkopo huo kama yanaendana na biashara yako. Unaweza kupewa mkopo ambao unahitaji kurejesha kiasi kikubwa kuliko faida yako unayoipata. Kama utachukua mkopo wa aina hii ni lazima utaaingiza biashara yako kwenye matatizo makubwa.

Jambo la tatu ambalo ni muhimu kuzingatia hasa pale unapokuwa umeshachukua mkopo ni kutoingiza fedha yote ya mkopo kwenye biashara. Kumbuka mkopo tunaozungumzia hapa sio wa kuanza biashara bali wa kukuza biashara yako zaidi. Unapochukua mkopo huu ambao umeshapanga ni kitu gani utaufanyia, bado usiingize mkopo wote kwenye eneo hilo la biashara. Unaweza kuwa umeweka mipango mizuri sana ila mambo yakabadilika, hivyo ni vyema kuweka nafasi ya kufanya mabadiliko kama mambo hayatakwenda kama ulivyotarajia. Kuwa na angalau theluthi moja ya mkopo wako pembeni ambayo itakusaidia kama mambo yatakwenda vibaya.

Jambo la mwisho kuzingatia ili uweze kunufaika na mkopo unaochukua ni nidhamu yako kwenye fedha. Mkopo unahitaji uwe na nidhamu kubwa sana kwenye matumizi yako ya fedha hasa fedha za biashara. Kama huna mahesabu mazuri ya matumizi yako ya fedha kwenye biashara utajikuta unashindwa kujua unatumiaje mkopo wako na hivyo kushindwa kufikia malengo ya mkopo uliochukua. Hakikisha unatumia mkopo uliochukua kufanya mambo yale yaliyokufanya uchukue mkopo, kama una tatizo jingine kwenye biashara kabla ya kukimbilia kutumia mkopo huo kwa tatizo hilo jiulize kwanza kama usingekuwa na mkopo ungetatuaje tatizo hilo. Nidhamu inahitajika sana ili uweze kufikia malengo yaliyokufanya uchukue mkopo.

Mkopo ni muhimu sana kwenye ukuaji wako wewe kama mjasiriamali. Ila kabla ya kuchukua mkopo ni muhimu kuzingatia sababu inayokufanya uchukue mkopo, kujua mkopo wenyewe, kutoweka mkopo wote kwenye biashara na pia kuwa na nidhamu kwenye matumizi yako ya fedha za biashara.

Nakutakia kila la kheri katika mafanikio ya biashara yako.

TUPO PAMOJA.