Je, Unataka Kuishi Maisha Ya Mafanikio Siku Zote? Hakikisha Unaishi Maisha Haya Kila Siku.

Kuna wakati ninapojaribu kuzungumza na watu kuhusu mambo ambayo ninayajua kuhusu maisha, yakiwemo mambo ya mafanikio na yale ya utambuzi kuna kipindi huwa napambana na upinzani mwingi sana. Inatokea kwamba, unazungumza juu ya jambo la wazi kabisa kuhusu maisha ya mafanikio, lakini inakuwa ni vigumu kwa wengi kuuona ukweli.

Kama ingekuwa watu wengi wanafungua milango ya mabadiliko kwenye maisha yao, dunia ingekuwa ni mahali salama sana kwa watu kuishi. Lakini, hilo sio linalotokea  bado kuna ugumu kwa wengi kuwa tayari kwa mabadiliko ya kimaisha, hiyo yote inaonyesha ni kwa jinsi gani binadamu tulivyokuwa wagumu kubadilisha tabia zetu.

Tunaona ni rahisi kufanya jambo lilelile kabla ya kukubali kulibadilisha, tena baada ya muda mwingi kupita. Kutokana na kujitumbukiza katika duara hili la kitabia tumejikuta maisha halisi yakituponyoka. Kutokana na sababu hiyo pia tunakosa uhuru wa kufanya mambo kwa ubora zaidi, na kupelekea kuishi maisha yaleyale kila siku bila mafanikio makubwa tunayoyataka.

Je, umeshawahi kujiuliza “nitafanyaje maisha yangu ili yawe bora zaidi”? kama unataka kuboresha maisha yako ya kila siku, unalazimika kuachana na tabia zako nyingi mbaya zilizokukwamisha na kukufikisha hapo ulipo. Jiulize, utaendelea kuishi hivyo kwa kulalamika na kukosa pesa mpaka lini? Ni wakati sasa wa kufanya mabadiliko. Na kama unataka kuishi maisha ya mafanikio siku zote, hakikisha unaishi maisha haya:-
1. Jiangalie undani wako wewe ni nani.

Ni wangapi kati yetu waliojaribu kujiliza wao ni akina nani? Ni wangapi wanakijua wakitakacho? Kama unataka kukijua ukitakacho katika maisha yako jiulize swali moja, je, nikifanyacho kinanipa furaha? Ni swali linalotakiwa kujibiwa kwa moyo mkunjufu na bila mzaha wala kuogopa. Kama jibu ni hapana, basi huna budi kubadili aina ya maisha yako unayoishi sasa.

Hili ni swali ambalo unatakiwa ujiulize mara kwa mara. Utakapogundua kile kikuleteacho furaha kishikilie kwa nguvu zote maana hapo ndipo mafanikio yako yalipo. Kuwa kiongozi wa maisha yako na siyo mfuasi. Unatakiwa kushika usukani wa maisha yako wewe mwenyewe kwa kufanya kile unachokipenda kwani kitakuletea mafanikio makubwa.
2. Acha kuishi maisha ya kujiangusha kila wakati.
Unapokosea kitu usijilaumu. Sisi sote huwa tunafanya makosa na kuna wakati tunafanya mambo yanayotia kinyaa. Badala ya kulaani na kujikatisha tamaa baada ya kufanya kosa, jipe moyo. Ongea chanya juu yako, hata kama umefanya jambo hasi kiasi gani. Kanuni kama hizi zitakubadilisha maisha yako na kuishi maisha yenye uhai na mafanikio makubwa.

Kumbuka, makosa ni kitu cha kawaida katika maisha. Wakati mwingine utakuta tunarudia kufanya makosa yaleyale mara nyingi. Kuna wakati mwingine unarekebisha kosa baada ya kosa la kwanza tu. Wakati mwingine unajifunza na kuweza kuelewa baada ya kufanya makosa mengi. Sisi ni binadamu tuko tofauti, usikate tamaa jirekebishe tu. Acha kuwa hakimu wa kujihukumu nafsi yako kwa kile ulichokifanya, utakuwa unajiumiza mwenyewe.
3. Jiambie wewe mwenyewe kuwa ni mtu wa mafanikio.

Kujitabiria au kujiambia wewe mwenyewe kuwa ni mtu wa mafanikio ni kitu muhimu sana kwa ajili ya kukua kwetu. Kila kitu ukisemacho kinadakwa na mawazo ya kina na kutuzwa kwa ajili ya rejea. Ni mbaya kama kila wakati utakuwa unajiambia tena na tena kuwa siwezi! siwezi! siwezi!. hutoweza kufanikiwa. Utakuwa kama zuzu! Hivyo ndivyo mawazo yako ya kina yatakavyokua.

4. Kuwa na tabia ya kujifunza mara kwa mara.

Kupata uzoefu mpya kupitia kujifunza ni jambo jema sana. Ujuzi mpya huongeza upeo. Hukupeleka kwenye neema mpya. Maisha yanabadilika muda wote. Njia pekee ya kukabiliana na mabadiliko haya ya mara kwa mara ya dunia ni kujifunza mambo mapya tu kila siku. Unaweza ukujifunza kupitia vitabu, semina au mitandao mizuri kama AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFAkwa kujifunza zaidi, mambo yatakayobadili maisha yako.

5. Usiwe na tabia ya kupoteza muda wako sana.

Ni ukweli usiofichika watu wengi ni watu wa kupoteza muda katika maisha yao. Ni watu wa kukurupuka na kutaka kufanya kila kitu katika maisha yao. Kama unaishi maisha haya ya kupoteza muda mara kwa mara kwako itakuwa ngumu kufanikiwa, kwa sababu utakuwa unapoteza kitu ambacho huwezi kukirudisha tena. Kama kuna kitu unaweza kukifanya leo, kifanye acha kukipeleka kesho utakuwa umepoteza muda wako.( Soma pia Hivi Ndivyo Vitu Vinavyo Kupotezea Muda Sana Katika Maisha Yako )
Kumbuka siku zote ukiishi hovyo maisha kwako yatakuwa mzigo kila siku, ishi maisha yako leo yatakayokuongoza katika mafanikio ya kesho. Na dalili za mafanikio yako ya baadae ni jinsi unavyoishi leo. Fungua milango kwa ajili ya mafanikio makubwa unayoyataka katika maisha yako. Unataka kuishi maisha ya mafanikio, hakikisha unaishi maisha hayo kila siku.

Nakutakia ushindi katika safai yako ya mafanikio, endelea kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa kuongeza maarifa bora yatakayobadili maisha yako.

Kwa makala nyingine nzuri, zitakazo badili mwelekeo wa maisha yako hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.

TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.

IMANI NGWANGWALU


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: