Katika kipengele hiki cha tabia za mafanikio tunaendelea kujifunza jinsi ya kujijengea tabia ya kutokuahirisha mambo. Kama ambavyo tumekuwa tukiona awali, tabia ya kuahirisha mambo imekufanya mpaka sasa umeshindwa kufanya mambo makubwa sana kwenye maisha yako.
Leo tutaangalia uhusiano kati ya mafanikio na tabia ya kuahirisha mambo.
Uhusiano kati ya mafanikio na tabia ya kuahirisha mambo unaweza kuwa wa aina mbili. Unaweza kuwa uhusiano chanya ambapo tabua ya kuahirisha mambo inakusaidia kufikia mafanikio makubwa. Pia unaweza kuwa uhusiano hasi ambapo tabia ya kuahirisha mambo inakufanya ushindwe kufikia mafanikio.
Ni wakati gani ambapo tabia ya kuahirisha mambo inaweza kukufanya ufikie mafanikio makubwa?
Katika maisha yako kuna mambo mengi ambayo utahitaji kufanya, lakini sio mambo yote unayotaka kufanya yatakuwezesha kufikia mafanikio. Kama ambavyo tulimeshajifunza mara nyingi, sheria ya pareto inasema kwamba asilimia 20 ya mambo yote unayofanya inakuletea matokeo kwa asilimia 80. Kwa mpango huu ni kweli pia kwamba asilimia 80 ya mambo unayofanya yanachangia asilimia 20 ya mafanikio.
Kwa sheria hii kuna mambo machache ambayo ukiyafanya yanakuletea mafanikio makubwa na kuna mambo mengi ambayo ukiyafanya yanakuletea mafanikio kidogo sana.
Sasa hapa ndio pa kutumia tabia ya kuahirisha mambo. Kazi yako sasa ni kujua ni mambo gani ukiyafanya yanakuletea mafanikio makubwa na ni yapi ambayo ukiyafanya yanakuletea mafanikio kidogo. Baadaya kujua mambo hayo sasa weka tabia ya kuahirisha mambo kwenye mambo yale mwengi ambayo yanakuletea faida kidogo. Kwa kufanya hivi utakuwa umeweza kutumia vizuri tabia ya kuahirisha mambo na kuweza kufikia mafanikio makubwa.
Ni wakati gani ambapo tabia ya kuahirisha mambo inatufanya tushindwe kufikia mafanikio?
Kama umenielewa vizuri hapo juu utakuwa tayari unalo jibu. Tabia ya kuahirisha mambo yale ambayo ndio muhimu na yanaleta faida kubwa ndio inafanya ushindwe kufikia mafanikio makubwa. Kwa kuahirisha yale yanayoleta faida kubwa na kuhangaika na yale yenye faida ndogo ni kikwazo kikubwa sana kwako kufikia mafanikio.
Kama ndio rahisi hivi mbona watu wengi hawafanikiwi?
Kama unachohitaji ni kujua mambo yenye faida kubwa kwako na kuyapa kipaumbele na yale yasiyokuwa na faida kubwa kuahirisha kwa nini kila mtu hafanyi hivyo na kufikia mafanikio?
Ukweli ni kwamba mambo yale ambayo ni muhimu sana ili kufanikiwa sio rahisi kuyafanya, Ni mambo ambayo yanachangamoto na pia yanahitaji mtu kujitoa kweli. Lakini mambo yale ambayo hayana faida kubwa ni rahisi kufanya na wala hayahitaji kufikiri sana.
Hii ndio sababu inayowafanya watu kuahirisha mambo ambayo ni muhimu na kufanya yale ambayo sio muhimu. Na ndio maana tabia ya kuahirisha mambo inakuwa na athari hasi kwetu.
Mpaka sasa umejifunza mengi kuhusiana na tabia hii ya kuahirisha mambo. Tayari unajua ni vitu gani vinaichochea na hivyo kuweza kuviepuka. Pia unajua njia za kuondokana na tabia hii ya kuahirisha mambo.
Sasa fanyia kazi mambo haya uliyojifunza ili yaweze kukusiadia kufikia mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.
TUPO PAMOJA.