Pamoja na umuhimu mkubwa wa kuwa na kipaumbele kwenye maisha, bado watu wengi sana hawana kipaumbele au hata kama wakiwa nacho wanashindwa kukitekeleza. Kuna changamoto nyingi sana zinazowafanya watu kushindwa kuweka kipaumbele au kushindwa kufanyia kazi kipaumbele walichoweka. Na changamoto hizi zinaanzia kwenye tabia ambazo mtu anakuwa nazo. Katika makala ya leo kwenye muendelezo huu wa makala za tabia za mafanikio tutaangalia tabia zinazoharibu kipaumbele chako kwenye maisha.

1. Kukosa malengo.

Kama huna malengo ni vigumu sana kuwa na kipaumbele au kufanyia kazi kipaumbele. Malengo yanakuwa kama ramani yako kwenye maisha, yanakuwa na vitu vyote unavyotaka kufanya kwenye maisha yako na muda unaotaka kuvifanya. Kwa kuwa na malengo ambayo unayafanyia kazi, kila wakati utakuwa na kipaumbele ambacho kinatokana na malengo hayo. Pia kama ukiwa na malengo ambayo sio makubwa na hayakuhamasishi unaweza kushindwa kufanyia kazi kipaumbele chako.

Kuwa na malengo ambayo umeyawekea tarehe ya mwisho ya kuyafikia, na hii itakusukuma uweze kuwa na kipaumbele ambacho unakifanyia kazi kwenye wakati husika. Kama malengo yako hayana kikomo cha muda wa kuyafikia ni vigumu kukusukuma wewe uyafanyie kazi na hivyo kushindwa kuwa na kipaumbele.

2. Tabia ya uvivu.

Kama huwezi kujituma, kama huna msukumo wa ndani wa kufanyia kazi mipango yako ni vigumu sana kuwezakukamilisha kipaumbele chako. Watu wengi wanakuwa na malengo na mipango mizuri sana, ila inapofika wakati wa utekelezaji hakuna kikubwa ambacho wanaweza kukifikia.

Unahitaji kuwa na msukumo mkubwa na hamasa kubwa itakayokuwezesha wewe kufanyia kazi mipango yako. Na hii itakuwezesha kukamilisha kipaumbele ambacho utakuwa umejiwekea.

3. Kuwa rahisi kusumbuliwa.

Kama tulivyosema, tunaishi kwenye dunia ambayo usumbufu ni mwingi sana. Na mbaya zaidi usumbufu huu tunatembea nao na tunalala nao. Yaani tumeipa dunia ruhusa ya kutusumbua kwa masaa 24 kwa siku na siku 7 kwa wiki. Simu yako yenye uwezo mkubwa ni chanzo kikubwa cha usumbufu kwako. Kama utaruhusu vitu hivi vyenye usumbufu kwako kuwa muhimu sana kwako basi itakuwa vigumu sana kukamilisha kipaumbele chako.

Hakikisha sio rahisi wewe kusumbuliwa pale ambapo unafanya jambo ambalo ni muhimu na ambalo ni kipaumbele kwako. Hii inamaanisha kuwa eneo ambalo ni tulivu, kutokuwa karibu na simu na pia kutokuwa na mtandao wa intaneti. Hii itawezesha akili yako kutulia na kufanya jambo ambalo lipo mbele yako kwa wakati huo ambalo ndio kipaumbele chako.

4. Tabia ya kuahirisha mambo.

Hii ndio tabia ambayo itaua kila kitu ambacho unataka kuwa nacho kwenye maisha yako. Kama una tabia ya kuahirisha mambo, unaweza kuwa na kipaumbele ila inapofika wakati wa kutekeleza ukaahirisha. Na ukishaahirisha mara moja, una uwezekano mkubwa sana wa kuendelea kuahirisha tena na tena. Ndio maana tabia hii ni sumu kubwa sana kwako kufikia mafanikio makubwa.

Tumeshajadili jinsi ya kuondokana na tabia ya kuahirisha mambo. Pitia makala za nyuma kwenye kipengele hiki cha tabia za mafanikio na utaweza kujifunza mbinu bora za kuondoa tabia hii ya kuahirisha mambo.

5. Tabia ya matumizi mabaya ya muda.

Kama hujali muda ni vigumu sana kuweza kukamilisha kipaumbele chako. Muda ndio kitu ambacho upatikanaji wake ni mdogo ila umekuwa na matumizi mengi sana. Kama katika matumizi haya unashindwa kuweka mambo yako muhimu basi hutaweza kukamilisha kipaumbele unachojiwekea.

Tulishajadili tabia hii ya muda na unaweza kurejea makala zile na kujifunza njia bora za kuweza kutumia muda wako vizuri ili uweze kufikia mafanikio makubwa.

Fanyia kazi tabi hizi ambazo zinakuzuia kuweza kukamilisha kipaumbele chako. Tabia hizi zipo kwa watu wengi sana na zimekuwa kikwazo cha wengi kuweza kufanya mambo makubwa.

Nakutakia kila la kheri.

TUPO PAMOJA.