Jinsi Ya Kujijengea Uwezo Wa Kujiamini

Huwezi kupambana na adui unayemuogopa hata siku moja. Yabidi kwanza kutomuogopa adui yako ndio uweze kupambana naye. Sifa ya kwanza inakupasa kumjua adui yako, kujua uwezo na udhaifu wake. Adui mwenyewe wa kumjua ni wewe mwenyewe. Kama nilivyosema katika makala iliyotangulia kwamba chanzo cha matatizo mengi ni woga. Kuogopa kitu ambacho kinaweza kutokea ama kisitokee. Kitokee ama kisitokee hupaswi kukiogopa. Kukosa kujiamini ni tatizo linalowakwamisha watu wengi. Hakuna anayeweza kukuondolea tatizo hili zaidi yako mwenyewe, hivyo basi fanya yafuatayo na utaliepuka tatizo lenyewe.

1. JIPENDE

Labda kuna watu wangeuliza kujipenda vipi? Hakika kuna watu hawajipendi. Kama hujipendi wewe utawezaje kumpenda mtu mwingine? Na unategemea vipi watu wengine wakupende? Ninaposema kujipenda simaanishi kuwa mbinafsi. Namaanisha kwamba inakupasa kujithamini. Jithamini kwa kula vizuri, kujipamba, kujipumzisha na hata kuoga. Kama wewe hujipendi jiandae kutopendwa na watu wengine. Na kitendo cha kutopendwa na watu wengine kinaweza kwa kiasi kikubwa kukuondolea kujiamini na kujaa woga wa kukosolewa. Kwa mfano hakuna mtu anayependa kukaa na mtu mchafu ama anayenuka, anayekasirika bila sababu nk. Jipende nawe utapendwa, pia utajiamini.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuwa Jasiri Na Kufanya Mambo Makubwa Zaidi Ya Unavyofikiria. ( 2)

2. VAA VIZURI

Kuvaa vizuri hakukugharimu kitu kwani mavazi ni mojawapo ya mahitaji muhimu matatu ya binadamu. Mengine ni chakula na malazi. Ninaposema kuvaa vizuri nina maana kujua vyema ni nguo zipi zinazokupendeza. Si lazima ziwe za bei ghali. Hata mtumbani unaweza kupata nguo nzuri kwa bei nafuu. Jitahidi pia kuvaa nguo kulingana na mahali na pia utamaduni wa jamii inayokuzunguka. Usipende kuvaa nguo zinazoonyesha sehemu kubwa ya mwili wako ama nguo zinazobana sana mwili wako. Hii itakusaidia kuondokana na wasiwasi wa kujihisi kuvaa vibaya.

3. KUWA NA MAISHA YENYE MTAZAMO CHANYA

Ili uwezekujiaminiinakupasa kujijengea maisha yenye mguso na mtazamo chanya. Kwanza kabisa acha kujiwazia kushindwa. Waza uwezekano wa kitu na akili itakupa jinsi ya kutatua tatizo linalokukabili. Usiseme jambo hili ni gumu ama haliwezekani bali sema jambo hili litafanikiwa ama tatizo hili nitalitatua na kwa hakika akili yako itakupa mbinu nyingi za kulifikia lengo lako. Lakini ukishasema siliwezi akili yako itajifunga na jambo hilo hutafanikiwa. Usijinenee maneno ya kukatisha tamaa. Pia haitoshi tu kuwaza katika hali ya uwezekano (chanya), bali pia anza kuchukua hatua chanya. Jiulize kwanini wenzako wameweza? Kwa kuanza jaribukujitathminina kujijua vizuri, ni vitu gani unaweza kuvifanya, vikwazo unayohisi yapo na uhalisia wa uwepo wake isije ikawakwamba umejiumbia ulimwengu wako mwenyewe wa vikwazo. Kwa hiyo basi jijue na jitambue. Jua adui namba moja wa kushindwa kwako ni wewe.

SOMA; Jinsi Ya Kuondokana Na Hofu Ya Kuongea Mbele Za Watu.

4. KUWA MTU WA WATU

Kuwa mtu watu ni kuwa mwema na kuelewana na watu wote kadiri inavyowezekana. Watu kukuona kama adui au mtu asiyeelewana na watu kunaweza kukuondolea ujasiri wako. Simaanishi kwamba uwaachie watu nafasi ya kutawala maisha yako bali simamia yale unayoyaamini wewe. Simamia misingi yako uliyojiwekea. Kujihisi kwamba wewe ni mtu mzuri kutakujenga kuliko kujihisi wewe ni mtu mbaya. Kumbuka Imani huja kwa kusikia, kusikia watu wakikuongelea vibaya kutakuvunja moyo.

5. JIANDAE VYEMA

Katika makala iliyopita nilijaribu kueleza kuhusu suala la kujiandaa kwa jambo lolote. Kujua kitu kutakufanya ujisikie vizuri na hivyo kujiamini. Ndio maana basi wachezajihujiandaa vyema kabla ya kucheza mechi zao na hujiandaa zaidi pale wanapokabiliwa na mechi ngumu. Vile vile mwanafunzi ambae hajajiandaa vyema kwaajili ya mtihani, huwa na wasiwasi mwingi kabla na baada ya mtihani. Kulijua jambo kutakufanya ujiamini zaidi na kuondokana na wasiwasi.

SOMA; NENO LA LEO; Kitu Kimoja Kitakachokujengea Kujiamini Na Kujithamini.

6. ZUNGUMZA TARATIBU

Siku za nyuma kidogo kuna rafiki yangu aliniambia kwamba watu wasiojiamini huongea haraka sana na kwa sauti kubwa. Nilikuja kulithibitisha hili siku moja. Kuongea taratibu kutakufanya uonekane mwenye kujiamini. Watuwasiojiaminihuongea kwa haraka kwani wanahisi wanachokiongea hakina thamani mbele ya msikilizaji. Pia ongea kwa sauti ya kawaida inayosikika. Kuongea kwa sauti kubwa sanakunaonyeshakwamba wewe hujiamini na unataka kuwateka watu wasikie kelele zako na siyo maneno yako.

7. BADILI KUTEMBEA NA KUSIMAMA KWAKO

Labda inaweza kuonekana ni sababu ndogo lakini, lugha ya alama pia inazungumza mengi. Jinsi unavyosimama ama kutembea unawatumia watu taarifa nyingi za jinsi ulivyo ndani. Penda kusimama wima bila kuegemea vitu. Pia jitahidi kutembea mwendo wa kawaida ambao ni wa kikakamavu. Usitembee kwa kunyong’onyea wala kwa kuburuza miguu. Tembea wima huku mabega yakiwa nyuma na usitembee kwa kutazama chini kama afanyavyo kondoo. Kusimama kilegevu ama kutembea kilegevu watu watakusoma na kuhitimisha kuwa hujiamini.

SOMA; SIRI YA 10 YA MAFANIKIO; Jinsi Ya Kujiamini.

8. TAFUTA MAJIBU YA MATATIZO YAKO

Katika kitabu cha WinnersandWinners (washindi na washindi)mwandishi anatuambia kuwa walalamikaji ni wale watu ambao hutazama matatizo yao bila ya kutafutia majibu. Jua kuwa kulalamikia tatizo sio njia ya kulitatua. Ukiwa na tatizo kaa chini waza na hakika utapata majibu yake. Huna hela? Jibu lake ni kufanya kazi, hujui kusoma? Nenda shule au tafuta mtu akufundishe? Huna ajira? Tafuta ajira ama jiajiri. Majibu ya matatizo yako unayo mwenyewe. Jiamini jikubali usikate tamaa.

Mwandishi ni: Nickson Yohanes ambaye ni mjasiriamali na mhamasishaji. Unaweza kuwasiliana na naye kwa: simu: 0712843030/0753843030 e-mail:nmyohanes@gmail.com Pia unaweza kutembelea blogu yake: www.lifeadventurestz.blogspot.comkujifunza zaidi.

Makala imehaririwa kwa Kiswahili fasaha na Rumishael Peter ambaye ni Mhariri wa vitabu/makala za Kiswahili na Mjasiriamali Email: rumishaelnjau@gmail.com simu 0713 683422.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: