Leo naomba niongee na wasomaji wa KISIMA CHA MAARIFA ambao bado wapo kwenye ajira ila haziwaridhishi na wanataka kuingia kwenye biashara au ujasiriamali. Kwanza nikupongeze sana kama wewe ni mmoja wa watu hawa ambao wanaona kazi pekee haitawawezesha kufikia yale mafanikio makubwa waliyopanga kufikia.
Pamoja na ajira kutokuweza kukufikiahsa katika malengo yako makubwa, pamoja na changamoto nyingi zilizopo kwenye ajira, bado ni muhimu wewe kuendelea kuwepo kwneye ajira hiyo kwa muda kabla hujaiacha na kuingia moja kwa moja kwenye ujasiriamali. Hapa nitakupa sababu kumi kwa nini nakuambia hivi.
Kabla hatujaangalia sababu hizi kumi kwanza tuangalie upotoshwaji ambao umekuwa unafanywa kwa wengi. Watu wengi wamekuwa wakiaminishwa kwamba, kama unataka kuw amjasiriamali mwenye mafanikio, basi unahitaji kuchukua mazingira hatari(rsk taker). Kama upo kwenye ajira basi uachane na ajira hiyo na kuingia kwenye ujasiriamali ambapo utaweka nguvu zako zote na kuweza kupata kipato kinachoendana na juhudi zako. Maelezo haya ni ya kweli ila hayamalizii kipande muhimu sana cha maelezo hayo ambacho ni biashara zinazoanzishwa na watu ambao hawana uzoefu wowote wa biashara, kati ya kumi, nane zinakufa ndani ya mwaka mmoja mpaka miwili. Na biashara zinazoanzishwa na watu ambao walishawahi kufanya tena biashara, sita kati ya kumi zinakufa kati ya mwaka mmoja mpaka miwili.
Kuingia kwneye biashara ambayo watu nane kati ya kumi watashindwa, ni hatari kubwa sana kwa mtu yeyote, kwa sababu hii ni sawa na kuwa na uhakika kwamba unakwenda kushindwa kwenye biashara hiyo.
Nimekuwa nikishauri watu wanaoingia kwenye biashara na ujasiriamali kwa muda sasa lakini sijawahi kumwambia mtu aache kazi haraka ili aweze kuweka nguvu zake kwenye ujasiriamali. Nina sababu nyingi kwa nini sifanyi hivyo, na hapa nitakushirikisha sababu kumi.
1. Unahitaji kuendelea kuwa na kipato cha uhakika. Japokuwa kazi haina uhakika sana kwa sasa, lakini angalau kwa sasa kuna kipato ambacho unakipata kwenye ajira yako. Hiki kitakuvusha nyakazi ambazo ni ngumu, hasa pale ambapo utaanza ujasiriamali ukiwa bado kwenye ajira yako.
2. Kuna nafasi nyingi za kuweza kuanza ujasiriamali hata bado ukiwa kwenye ajira yako. Tumia nafasi hizi na anza kidogo kidogo, jifunze kenye kila hatua unayoshindwa au kukosea, endelea kukuza biashara yako na ikifikia hatua ukaona sasa hapa inaweza kukupatia kipato cha kutosha kuendesha maisha yako ndio unaweza kuacha kazi.
3. Kutoa fedha kwenye biashara changa ni kuiua. Katika miezi angalau sita ya kwanza ya biashara yoyote ndio kipindi ambacho biashara yoyote inakazana kukua. Sasa kama utaondoa fedha kwenye biashara hii kwa sababu yoyote ile, unakuwa umeandika adhabu ya kifo kwneye biashara yako. Unahitaji kuendelea kuwa na kipato kingine unachotegemea tofauti na biashara hiyo, hivyo kama umeajiriwa, hiki ndio kipato chenyewe.
4. Kukuza mtandao wako wa kibiashara. Unapokuwa kwneye kazi ni rahisi sana kukuza mtandao wako wa kibiashara. Unaweza kutengeneza wateja wengi wa huduma au bidhaa zako kupitia kazi unayofanya hivyo inakupa nafasi nzuri ya kuweza kukuza biashara yako.
5. Kufaidi huduma nyingine muhimu. Kuna huduma muhimu ambazo utaweza kuzifaidi kama utakuwa kwenye kazi. Kupitia kazi yako unaweza kuwa unapata huduma ya bima ya afya kwako na kwa familia yako. Hii inakusaidia kuokoa fedha nyingi ambazo ungezitumia kwenye huduma za afya. Japokuwa unaweza kujiunga na mfuko wa bima ya afya kama mtu binafsi, bado itakugharimu kiasi kikubwa kuliko aliyeko kwneye ajira.
6. Kazi inaweza kukupa uzoefu wa biashara. Kuna baadhi ya biashara unazoweza kuanzisha ambazo zinaendana na kazi unayofanya sasa. Kwa kuwepo ndani ya kazi ile unajifunza mambo yote muhimu ya kuzingatia ili na wewe uweze kukuza biashara yako. Pia unawajua vizuri wateja ambao wanaweza kuja kuwa wateja wako pia na mambo mengine ya ndani ambayo yatakuwezesha kuendesha biashara yako vizuri.
7. Kazi itakupa changamoto zitakazokuwezesha kufanikiwa kwenye biashara. Kama kazi uliyonayo imekuchosha kwa sababu unahitaji kuamka mapema sana na kutekeleza majukumu mengi, shukuru sana maana hiko ndio utakuwa unafanya kila siku kwneye biashara yako. Kama una mawazo wkamba ukishakuw amjasiriamali utaamua ni mud agani uamke, ni muda gani ufanye kazi na muda gani upumzike, utashindwa haraka sana. Ujasiriamali una changamoto nyingi, ukiziweza changamoto za kwenye ajira utaweza changamoto za ujasiriamali.
8. Chanzo kizuri cha mtaji. Kuwepo kazini unakuwa kwemye nafasi nzuri ya kuapata mtaji wa kuanzia na hata wa kukuzia biashara yako. Unaweza kutumi akiba zako kuanza na ukishaona biashara imekaa vizuri unaweza kutumia nafasi yako ya kazi kuomba mkopo ambao utauzungusha zaidi kwenye biashara yako. Kuwepo kweye kazi kutakupa kipaumbele kwenye kupata fedha za mtaji.
9. Kuweza kwenda vizuri na watu. Ujasiriamali sio vita ya mtu mmoja, ni vita inayokuhitaji wewe uweze kushirikiana na makundi mbalimbali ya watu. Kuna wateja, wafanyakazi, washirika, washindani, wawekezaji, taasisi z akifedha na kadhalika. Unahitaji kuw ana uzoefu mzuri wa kufanya kazi na watu mbalimbali ili uweze kuenda na watu hawa vizuri. Kuna wakati unawez akuingia kwenye mgogoro na baadhi ya makundi ya watu, hivyo unahitaji kuw ana mbinu za kuwez akutatua migogoro, mbinu za ushawishi na mengine mengi yanayohusisha watu.
10. Kukufanya uwe mtu wa kujali majukumu yako zaidi ya starehe au mapumziko. Kama wewe ni mwajiriwa na wakati huo huo una baishara yako pembeni, ni dhahiri maisha yako hayatakuwa sawa na ya waajiriwa wengine. Wakati wenzako wamepumzika baada ya kazi wewe utakuwa unafuatilia biashara zako, wakati wenzako wanafurahia mapumziko ya mwisho wa wiki, wewe unayatumia kukuza biashara yako. Wakati wenzako wanafurahia sikukuuza katikati ya wiki ili walale, wewe unazifurahia ili uweze kufanya kazi kwenye biashara yako zaidi. Yote haya yanakufanya wewe uwe mtu wa majukumu na hivyo utakapoingia kwenye biashara moja kwa moja utakuwa umejijengea tabia ya kufanya zaidi ya wengine.
Kama unataka kufanikiw akwneye ujasiriamali na bado upo kwenye ajira, huna haja ya kufanya maamuzi ya haraka halafu ujikute kwenye matatizo. Endelea kufanyia biashara yako kazi wakati bado upo kwenye kazi yako, utahitaji kuweka juhudi za ziada sana ili biashara yako iweze kufikia hatua ambayo inajiendesha vizuri.
Lakini pia usitumie sababu hii kufia wkenye ajira kwa sababu tu hutaki kuchukua maamuzi ya haraka, fanyia kazi biashara yako na baada ya muda ingia moja kwa moja.
Kama huna kazi na unataka kuingia kwenye biashara, usisubiri upate kazi, anza mara moja na utajiweka kwenye nafasi nzuri ya kufikia mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.
TUPO PAMOJA