Kama ingekuwa rahisi, basi hakuna ambaye asingetaka.
Siku moja mtu tapeli aliulizwa ni mtu gani rahisi kumtapeli? Bila ya kusita alijibu kwamba mtu rahisi kumtapeli ni mtu ambaye sio mwaminifu. Mtu yeyote ambaye anaamini kuna njia rahisi ya kupata chochote anachotaka ndio huwa anaishia kutapeliwa.
Kwa mfano mtu anaambiwa leta fedha zako, zinakaa kwetu kwa siku kadhaa halafu utarudishiwa mara tano ya fedha ulizotupatia. Kama wewe sio mwaminifu, kama wewe unaikiri kuna njia rahisi, unajiingiza kwenye mtego na watu wanakutapeli.
Tunaona kila siku na kama umewahi kutapeliwa utakubaliana na mimi kwamba ulikuwa na tamaa. Au ulifikiria kuna njia rahisi ya kupata chochote ambacho unataka kupata.
Hakuna njia rahisi, hakuna njia ya mkato.
Dunia hii imekuwepo kwa miaka bilini kadhaa, katika kipindi chote hiki binadamu wamekuwa wakitumia juhudi na maarifa kuweza kuendesha maisha yao. Kama kungekuwa na njia rahisi, hakuna mtu ambaye angependa kuumia. Binadamu sisi ni viumbe wavivu sana, kila mtu angekimbilia njia hiyo na wala hakuna ambaye asingeifahamu.
Watu wote makini wanajua hakuna njia rahisi, hakuna njia ya mkato na hivyo wanaanza mapema kabisa kujitengeneza. Watu wasiokuwa makini hawajui hili na hivyo huendeshwa na tamaa na hatimaye kujikuta wanatapeliwa kila siku.
Ngoja nikupe siri moja ya kuepuka kutapeliwa au kupoteza fedha zako au muda wako. Ukishaanza kuhisi kwamba kitu unachoambiwa sio kweli, wala usihoji, kimbia haraka sana maana uko sahihi, sio kweli. Mtu akikuambia njoo nikuoneshe njia ya mkato ya kupata fedha, kimbia haraka sana kumkwepa, maana ukimsikiliza tu anakupoteza.
Sio rahisi na hakuna njia ya mkato.
TAMKO LA LEO;
Najua sio rahisi kupata kile ambacho nakitafuta, najua hakuna njia ya mkato ya kunifikisha pale ninapotaka kufika. Hivyo sitapoteza muda wangu kwenye mambo ya aina hii. Nitaendelea kuweka juhudi na maarifa kwenye hiki ninachofanya. Najua hapa ndipo mafanikio yangu yalipo.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.
