Habari za leo rafiki na mpenzi msomaji wa mtandao huu wa AMKA MTANZANIA. Ni matumaini yetu ya kuwa umzima wa afya na unaendelea vyema na majukumu yako kila siku. Nasi kwa furaha kubwa tunapenda kukuribisha katika siku nyingine ambayo unapata nafasi ya kuwa nasi na kuweza kujifunza mambo muhimu ya kuweza kubadili maisha yako na kuwa bora zaidi.
Leo katika makala yetu tutaangalia mambo ambayo mara nyingi tukiyafanya huwa ni lazima tufupishe maisha yetu kwa namna moja au nyingine hata kama hatujui. Hii yote huwa inatokana na aina ya maisha ambayo huwa tumechagua kuishi ambayo aina hiyo ya maisha huwa ni hatari sana kwa afya zetu na maisha kwa ujumla, hali ambayo hupelekea tukijikuta tukipoteza maisha yetu moja kwa moja.
Tatizo ambalo huwa tunalo wengi wetu ni kuishi maisha ya kujisahau sana na kufanya vitu ambavyo ni hatari sana nakudhani kuwa hatutaweza kufa ama tutaishi milele. Na mara nyingi kwa wengi huwa wanaanza kushtuka mambo yanapokuwa yameshakuwa magumu au afya zao zimekuwa mbovu kabisa. Je, unajua ni mambo gani yanayoweza kufanya maisha yako yakawa mafupi?
1. Kutokujali afya yako.
Watu wengi huwa wanaishi maisha ya kutokujali afya zao. Huwa nimaisha ambayo huwa wanajihusisha nayo pasipo kujali athari za mambo hayo kwa baadae inaweza ikawa ni nini. Yapo mambo ambayo ukiyafanya afya yako inakuwa ipo hatarini moja kwa moja hata hujasomea udaktri nni rahisi kwako kuweza kuyajua.
Tuchukulie kwa mfano kama wewe unakula vyakula hovyo na vibovu ambavo havifai, ni lazima afya yako itakuwa ipo hatarini sana. Lakini siyo hivyo tu unaweza ukawa pia mvuta sigara au unakunywa pombe sana bila utaratibu, mambo kama hayo ni rahisi sana kwako kuweza kukuharibia afya yako na kukufanya maisha yako kuwa hatarini. Hivyo ni muhimu sana kuepukana na mambo hayo ili kuweza kulinda afya zetu na maisha yetu kwa ujumla.
2. Kuishi wewe kama wewe.
Hakuna kitu hatari katika maisha yako kama kuweza kuamua kuishi wewe kama wewe. Hili ni jambo la hatari sana kwako na kwa namna yoyote ili linaweza kuhatarisha afya yako. Kwa kawaida binadamu ameumbwa ili kuweza kuwa na mahusiano na wengine. Sasa wapo watu ambao wamekata mirija ya mahusiano na wengine kwa sehemu kubwa.
Watu hawa kutokana na kutokujihusisha kwao na watu wengine hujikuta ni watu ambao maisha yao yanakuwa magumu na yanakuwa yapo hatarini. Hii huweza kutokea kwa sababu muda mwingi hujikuta mawazo yao mengi ni hasi kutokana na kujitenga na hivyo hujikuta ni watu wa kuwa na msongo wa kimawazo zaidi hali ambayo huwa ni rahisi kwa kuweza kupotezamaisha yao.
3. Kukaa chini kwa muda mrefu.
Hili ni jambo dogo tu sana, na unaweza ukalichukulia kwa urahisi, lakini kwa mujibu wa wataalamu wa afya hili pia ni jambo mojawapo ambalo tukiliendekeza sana linaweza kutuharibia afya zetu. Inashauriwa kuwa siyo vizuri sana kukaa chini kwa muda mrefu bila ya kusimama. Hiyo inaweza ikatuletea na kutusababishia magonjwa kadhaa kama vile magonjwa ya moyo, kisukari au kansa  .
Ili kuweza kulinda afya zetu nakuwa bora zaidi tunalazimika kutokukaa sana chini kwa muda mrefu. Ikitokea hivyo tukawa na kazi za kukaa chini muda mrefu, ni vizuri ukalazamika wewe mwenyewe kujaribu kutenga muda wa kusimama angalau kidogo ili kufanya mzunguko wa damu ukaendelea vizuri. Vinginevyo itapelekea kwetu sisi kuwa hatarini kiafya.
4. Kuangalia TV kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya wanadai  kuwa kuangalia TV kwamuda mrefu tena ukiwa karibu nayo inapelekea moja kwa moja kuua baadhi ya seli ndani ya miili yetu. Kwa wanaume pia kwa mujibu wa tafiti ambazo zimefanyika huweza pia kupunguza uwezekano wa kuzalisha mbegu za kiume kwa asilimia kubwa.  
Kikubwa cha kuzingatia hapa ni utambue kuwa kuangalia TV kwa muda mrefu sana kwa namna moja au nyingine kuna mdhara yake ambayo unaweza hata usiyaone kwa urahisi. Unaweza ukawa hujui lakini huo ndiyo ukweli. Unachotakiwa kufanya ni kuwa makini kuangalia kwa kiasi na siyo kupitiliza mpaka kutwa nzima.
5. Kutokupata usingizi wa kutosha.
Kukosa usingizi mara kwa mara katika maisha yako ni moja tatizo ambalo linaiweka afya yako hatarini moja kwa moja. Kwa kawaida binadamu anatakiwa alale saa 8 kwa siku. Unapokosa kulala saa hizo kinachokutokea kwanza inakuwa siyo rahisi kwako kuweza kuwa na kumbukumbu nzuri na za kutosha.
Lakini si hivyo tu, pia hukupelekea wewe kuweza kupata magonjwa kama vile ya kisukari, kansa na pia kuna wakati huweza kusababisha vifo vya mapema kwa wale wote ambao wanakosa usingizi wa kutosha. Kwa hiyo utaona kuwa kama muda mwingi unakuwa unakosa usingizi, utambue kuwa ni muhimu sana kwa afya yako na maisha yako kwa ujumla.
Ikumbukwe pia katika misha yetu kitu cha kwanza na muhimu ambacho tunakihitaji sana ni ubora wa afya zetu. Tunapokuwa na afya njema tunakuwa tunauwezo wote wa kufikia mafanikio tunayotaka. Bila afya nzuri na bora sahau kabisa kuwa na mafanikio. Hivyo ni muhimu kulinda afya zetu ili kufanikiwa zaidi. Kwa kifupi, hayo ndiyo mambo yanayoweza kuhatarisha afya yako.
Tunakitakia mafanikio mema katika kuboresha na kulinda afya yako zaidi.
Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika zaidi.
Ni wako rafiki katika  afya na mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048 035,