Najua unapenda kufanikiwa, najua juhudi zote unazoweka ni ili maisha yako yawe bora zaidi kuliko yalivyokuwa jana. Najua kwamba unasoma haka kwa sababu utaondoka na maarifa ambayo yatakuwezesha kuwa bora zaidi. Na ninakuahidi kwamba utaondoka na maarifa hayo. Kama hutayapata utaniwia radhi kwa kupoteza muda wako, ila nakuahidi haitachukua muda mrefu.

kuishi nyuma

Kwanza kabisa kama ambavyo nimekuwa nasema kila siku, mafanikio yanatabirika. Vitu unavyofanya leo ndio vinakufanya ufikie mafanikio au vinavyokuzuia wewe kufikia mafanikio. Hivyo kama unataka kujua miaka kumi ijayo utakuwa wapi, angalia ni vitu gani unafanya kila siku.

Leo nataka nikukumbushe eneo moja ambalo unapenda kukaa sana, sio kukaa kama kukaa bali huwa unapenda kupeleka mawazo yako kwenye eneo hili, huwa unapenda kuweka akili yako kwenye eneo hilo. Na vibaya zaidi ni kwamba hakuna mtu aliyewahi kufanikiwa kwa kuweka akili yake na mawazo yake kwenye eneo hilo. Hivyo na wewe ni muda wa kuacha kupoteza muda wako kwenye eneo hilo.

Eneo ninalozungumzia hapa ni mambo yaliyopita. Hakuna mtu yeyote amewahi kufanikiwa kwa kufikiria mambo yaliyopita, sasa nashangaa kwa nini wewe unafanya hivi. Unapoteza muda wako na kujipa sababu ambazo hata hazina maana.

Huu sio wakati wa kutumia kauli hizi;

Yaani kama mimi ningepata elimu, leo ungekuta nipo mbali sana…..

Kama ningejua mambo haya tangu nikiwa kijana, maisha yangu yangekuwa bora sana….

Wazazi wangu hawakutaka kunisikiliza, wao walinilazimisha nifanye wanachotaka, ona sasa wameharibu maisha yangu….

Kama ningekua sijaoa/olewa na mtu msumbufu, maisha yangu yangekuwa bora sana….

Hizi ni chache sana kati ya kauli nyingi ambazo umekuwa unazitumia kuishi kwenye kipindi cha nyuma.

Sasa nisikilize kwa makini sana, si unataka kufikia mafanikio? Acha mara moja kutumia kauli hizi. Hazina maana tena, hata kama uliteswa, ulidhulumiwa, ulifanywa nini, havina maana tena. Chenye maana ni nini unafanya leo ili kesho yako iwe bora. Ndio kama upo hai basi kilichotokea nyuma hakina maana tena, jifunze na songa mbele.

Mambo mazuri yapo mbele kwa mbele, kuangalia nyuma ni kupoteza muda.

SOMA; Usiwasamehe wazazi wako, waelewe.

TAMKO LA LEO;

Kuangalia nyuma kila mara hakuna faida yoyote kwangu. Nimegundua kwamba hakuna mtu aliyewahi kufanikiwa kwa kuangalia na kufikiria yaliyopita. Mambo yote mazuri yako mbele. Na uzuri wa mambo hayo nitaupata kama nitafanya mambo mazuri leo. naamua leo na kila siku kufanya mambo mazuri, kwa kufanya hivi kila siku najua nitakutana na mafanikio katika njia hii.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.