Huu ndio ule wakati ambapo wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu wanamaliza masomo yao. Ni wakati wa furaha sana kwenye maisha yao kwa sababu kitu walichokuwa wanakifanyia kazi kwa miaka mitatu, minne au mitano kimefika ukingoni.

 
Wanafunzi wengi wanamaliza wakiwa na matumaini makubwa sana ya kwenda kuanza maisha yao ya kazi na kujitegemea zaidi. Lakini mambo yanayoendelea huku mtaani ni tofauti kabisa na matarajio ya wanafunzi. Hali halisi ni tofauti na maandalizi ambayo mwanafunzi huyu anayo.
Ni vyema leo ukajifunza mambo kumi muhimu ambayo yatakuwezesha kuwa na maisha bora, mambo haya hukuwahi kujifunza chuoni hivyo jifunze na yafanyie kazi. Pia mtumie mhitimu mwingine makala hii ili na yeye apate kujifunza na kufanyia kazi mambo haya na maisha yake yapate kuwa bora.
Yafuatayo ni mambo kumi ambayo kila mhitimu wa elimu ya juu mwaka huu 2015 anatakiwa kuyajua.
1. Hakuna kazi.
Soma kwa bidii, faulu vizuri na utapata kazi nzuri na kuwa na maisha mazuri. Hivi ndivyo ulivyokuwa unaimbiwa kila siku kwenye maisha yako ya elimu. Kwa bahati mbaya sana waliokuwa wanakuimbia hivi yaani walimu wako walipata kazi kwa mtindo huo. Ila kwa sasa, mambo yamebadilika sana. Waliosoma ni wengi lakini nafasi za ajira ni chache sana. Ni sawa na kusema hakuna kazi.
Kwa hiyo kama hakuna kazi ndio elimu yako haina maana tena? Hapana, hapa ndipo unapoweza kuitumia akili yako vizuri na kuweza kufikiria njia nyingine za kutengeneza kipato na kuendesha maisha yako.
2. Kazi zipo kwa walioko tofauti.
Nafasi ya kawaida ya kazi ni kwamba inatangazwa na watu mnaomba. Kila mwombaji anatuma wasifu wake na wasahili wanachambua kwenye wasifu ule. Hii ilikuwa nzuri sana enzi zile ambapo wenye elimu ya juu walikuwa wachache, ila wakati huu ambapo kila mtu ana elimu ya juu, kupata kazi kwa njia hiyo ni vigumu sana, kama tulivyoona hapo juu.
Ila kwa wale ambao wako tofauti, wale ambao wana kitu cha ziada wanaweza kuonesha, hawa bado wana nafasi kubwa za kupata kazi. Wale ambao wana kitu cha ziada tofauti na wasifu ulioandikwa kwenye karatasi, wana nafasi kubwa ya kupata kazi na kutengeneza kipato kizuri.
Sasa utawezaje kuonesha kile cha ziada ulichonacho? Kuna fursa nyingi sana, anza na kazi za kujitolea, anza na kazi nyingine zinazoendana na kile ulichosomea na kazi hizi ziwe za kuinufaisha jamii inayokuzunguka, anzisha blog(kama unataka kujifunza jinsi ya kufanya hivyo bonyeza hapa) na andika mambo yanayohusiana na kile ulichosomea, kwa ajili ya kuelimisha umma. Yapo mambo mengi sana unayoweza kuyafanya na ukajiweka tofauti na wale ambao wanasubiri nafasi za kazi zitangazwe na wapeleke maombi yao.
3. Kusoma ndio kumeanza rasmi.
Warren bufet, tajiri namba mbili duniani, aliulizwa na mhitimu wa chuo, afanye nini ili afikie mafanikio kwenye maisha? Warren alichukua karatasi na kumwambia soma karatasi kama hizi 500 kila siku. Najua wanafunzi wengi mlikuwa mnasubiria siku ya kumaliza ifike ili uachane na mambo ya kusoma. Uanze kupata muda wa kupumzika, kufuatilia vitu unavyopenda na kadhalika.
Ukweli ni kwamba sasa kusoma ndi kwanza kumeanza. Na uzuri ni kwamba sasa hivi unasoma vitu ambavyo unapenda kusoma na sio ambavyo unalazimika kusoma kwa sababu unatakiwa kujibu mtihani. Soma sana, soma kila siku. Na sio kusoma magazeti, bali kusoma vitabu ambavyo vitakuongezea maarifa na kukuhamasisha pia.
Sio lazima usome kurasa 500 kama alivyosema Warren, ila mimi nakuambia wewe uanze kusoma vitabu viwili kwa wiki, na unahitaji kama masaa mawili tu kwa kila siku ili uweze kumaliza kusoma vitabu hivyo.
Kama uko tayari kusoma vitabu viwili na unajituma, sio mtu wa sababu, karibu kwenye kundi letu la kujisomea vitabu, linaitwa TANZANIA VORACIOUS READERS. Hapo tunafanya biashara moja tu, kusoma vitabu, ukishindwa kutimiza hilo unaondolewa, hakuna hadithi wala sababu nyingine. Kama utaweza tuma email kwenye makirita@kisimachamaarifa.co.tz na nitakupa maelekezo.
4. Kazi sio usalama.
Najua wengi mmekuwa mnadanganyana kwamba ni bora kupata kazi serikalini kwa sababu hii itakuwa salama. Mnaambiana ni bora upate kazi maana ina security, mmekuwa mnadanganyana kwa muda mrefu. Sasa ukweli ni kwamba kazi sio usalama hasa kwa kipindi hiki. Kama unafikiri nakutishia, kitu ambacho wengi mtafikiri, tafuta watu watatu ambao wanafanya kazi kwenye kazi utakayokuwa umepata wewe au unayotafuta, watu hawa wawe wamekaa kwenye kazi hiyo kwa zaidi ya miaka kumi kisha fanya nao mazungumzo. Waombe wakushirikishe mambo yote waliyopitia kwenye kazi hiyo. Utabaki mdomo wazi, kama watakuambia kwa njia ya kirafiki.
5. Watu wengi watakudanganya kuhusu kipato chao.
Utakutana na vijana wenzako wanaofanya kazi benki na watakuambia wanalipwa vizuri sana. Usiwasikilize wala usiwaamini, sio kweli. Utawapigia simu wenzako watakuambia wamepata kazi sehemu fulani na wanalipwa vizuri. Utajisikia vibaya na kujiona wewe ndio una kisirani. Sio kweli, asilimia 90 ya watu watakaokuambia kuhusu vipato vyao, watakudanganya. Sijui ni kwa nini, lakini ndio watu wanafanya hivyo, nafikiri hakuna mtu anayependa kuonekana ni mpotezaji(loser)
Mwaka 2011 mwishoni nilikutana na rafiki yangu ambaye alikuwa amemaliza chuo mwaka huo. Katika maongezi akaniambia amepata kazi kwenye kampuni fulani na alikuwa analipwa vizuri na mshahara alinitajia. Mwaka 2012 nilimwona akitafuta tena kazi, nilipomwuliza vipi kule ndio ilibidi anipe ukweli wenyewe. Mshahara ulikuwa kidogo na waliahidiwa utaongezwa, ila hajaona dalili hizo.
6. Hakuna kazi ambayo sio ya saizi yako.
Wewe kuwa na diploma au digrii hakukufanyi kuwa tofauti sana na wananchi wengine wa kawaida. Hakuna kazi ambayo sio saizi yako. Kwa kifupi usichague kazi na kazi yoyote utakayoipata, onesha juhudi kubwa sana, onesha uwezo wako mkubwa na onesha kile cha kipekee ulichonacho. Na hata kama hutapata kazi, angalia ni kitu gani unachoweza kufanya, usishinde tu ndani kuangalia tv, na picha za wenzako instagram ambazo zitakuumiza moyo.
7. Mitandao ya kijamii, kuwa makini nayo.
Hivi vidude vinakula muda sana. Ukitaka kuanza kufuatilia maisha ya watu kupitia mitandao ya kijamii unaweza kujiona wewe ndio hujielewi kabisa. Unaweza kuona wenzako wanabadili nguo nzuri, wanakula kwenye migahawa mizuri, wapo kwenye klabu nzuri na mengine mengi. Haya yote ni uongo na wala yasikusumbue, hivi vitu unavyoviona kwenye mitandao hii ni vile ambavyo watu wanafanya kwa mara chache sana. Lakini ile picha halisi ya maisha yao huwezi kuiona kwa picha wanazoweka kwenye mitandao ya kijamii.
8. Mitandao ya kijamii… sehemu ya pili.
Mitandao ya kijamii ni kama uwakilishi wako kwenye mtandao. Watu wakitaka kukujua vizuri wataandika jina lako google, yaani watakugoogle, na google huwa haifichi, italeta kila kitu ambacho umewahi kuandika kwenye mtandao. Pia italeta kila picha ambayo umewahi kuweka kwenye mtandao. Sasa kama cv yako umeandika hard working, discplined and determined na huku kwenye instagram au facebook wewe ni team bata batani unajichanganya mwenyewe.
Siku hizi hata wanaofanya usaili wa kazi watakutafuta kwanza google. Mtiririko wa vitu unavyoweka kwenye mtandao unatosha kueleza wewe ni mtu wa aina gani. Sio lazima uweke kila kitu kwenye mitandao ya kijamii, hakikisha chochote unachoweka ni kitu ambacho ungependa kisomwe siku ya mazishi yako, kama sio achana nacho.
9. Kuwa mwaminifu, kuwa mwadilifu.
Najua hivi ni vitu vigumu sana kuelewa kwa sasa, hasa pale ambapo umekulia na kusomea kwenye mfumo ambao unaendekeza vitendo ambavyo sio vya uaminifu au uadilifu. Mfumo ambao u akuambia ukipata kazi tra au bandarini ndio umetoka. Au ukipata kazi ya utrafic mambo yako yamekuwa vizuri. Achana na mambo hayo, kuwa mwaminifu usiibe kitu cha mtu, usidhulumu mtu na timiza kile unachoahidi.
Jiheshimu na kuwa na misingi yako mwenyewe ambayo utaisimamia. Haya ni maisha yako usiishi kwa kuigiza wengine. Hakikisha chochote unachofanya au kusema unaweza kukisimamia na kujivunia kwa kitu hiko.
10. Soma makala hizi, ni muhimu sana.
Kuna vitu vingi sana ambavyo unatakiwa kuvijua ila pia tulishavijadili kwenye makala nyingine. Tumekuwa tunaandika makala hizi za ushauri kwa wahitimu tangu mwaka 2013. Hivyo hapa nimekuchagulia makala chache ambazo ni muhimu sana kuzisoma, tafadhali sana zisome.
1. KABLA HUJAANZA KUZUNGUKA NA BAHASHA SOMA HAPA.
2. Mabadiliko; Yalikuwepo, Yapo Na Yataendelea Kuwepo.
3. Soma makala hizi za ushauri kwa wahitimu wa elimu ya juu.
Nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya mafanikio ambayo umeianza rasmi. Hakuna kinachoshindikana kama kweli utaamua. Karibu sana na endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku. Kwa lolote niandikie kwenye email makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.
Makirita Amani.