Kama kuna njia rahisi kabisa ya kuipoteza siku yako ni kuianza bila ya kufanya kitu hiki kimoja ambacho ni muhimu sana kwako na kwa maisha yako. Ni kitu ambacho kitakuwezesha wewe kufika kule unakotaka wakati wengine wanaendelea kuhangaika na maisha na wasijue wanaenda wapi.

PANGA SIKU
TAFADHALI SANA USIIANZE SIKU YAKO KABLA HUJAIMALIZA KWENYE KARATASI.

Kabla sijakuambia kitu hiki muhimu naomba nitoe angalizo, mwaka juzi nimewahi kuandika makala kama hii nikieleza kitu muhimu cha kufanya kila siku asubuhi. Msomaji mmoja baada ya kusoma aliniandikia email akisema, mimi nilijua unawaambia watu wakiamka asubuhi kitu cha kwanza kufanya wasali, ila wewe unawaambia wasome(katika makala hiyo nilikuwa naongelea umuhimu wa kusoma kila siku). Nilimjibu kwa kifupi kwamba kusali hilo sio swala la kusubiri uambiwe, kila mtu ana imani yake na ni vyema kufuata taratibu ambazo zinaendana na imani uliyonayo. Hivyo fanya utaratibu wako wa kiimani kila unapoamka, na sitegemei kuulizwa tena swali kama hilo.

Sawa, sasa turudi kwenye mada hii ya leo.

Kuna jinsi ambavyo ukiianza siku unajua kabisa unakwenda kuipoteza na kuna jinsi ambavyo ukiianza siku yako unajua utakwenda kufanya mambo mazuri. Tunachotaka mimi na wewe ni kuianza siku tukijua tunakwenda kukamilisha mambo mazuri ili tuweze kuboresha maisha yetu.

Sasa kama hiki ndio unachotaka kweli, usianze siku yako bila ya kuipangilia. Hiki ni kitu muhimu sana kiasi kwamba naweza kukuambia kama hujapangilia siku yako ni bora ukaiahirisha, au uache vitu vingine vyote ulivyokuwa unafikiria kufanya na uanze kuipanga siku kwanza.

Hakuna kitu muhimu kama kuipangilia siku yako, kwa sababu kwa dunia tunayoishi ambayo ina kelele za kila aina, kama hujaipangilia siku umeamua kuipoteza.

Na kuipangilia siku ninakosema sio kufikiria tu leo au kesho nitafanya hiki na hiki na hiki, hapana huko sio kupanga, ni kufikiria tu. Na akili yako ikizidiwa mawazo hutaweza kukumbuka uliyofikiria muda uliopita.

Hivyo ili kuipangilia siku yako kuwa na kijitabu unachoandika mipango yako ya kila siku, kila wiki na kila mwezi. Kwenye kitabu hiki andika ni vitu gani unataka kufanya kwenye siku husika, kuanzia kwenye maisha yako binafsi na kwenye kazi au biashara yako. Jinsi unavyoandika vitu hivyo viandike kwa mfuatano kuanzia kile ambacho ni muhimu zaidi kuenda kile ambacho sio muhimu.

Unapoianza siku unafuata ile orodha yako, na usiende jambo la pili kabla hujamaliza la kwanza. Na ili uone uzuri wa hili, ukishamaliza jambo weka alama kubwa ya vema mbele ya orodha yako. Utajisikia vizuri sana na utajiona mshindi.

Lakini kama utaianza siku yako bila ya kuipangilia na bila ya kuwa na orodha ya vitu utakavyofanya, ni rahisi kuchukuliwa na mambo yanayoendelea na pia rahisi kuahirisha baadhi ya mambo. Pia utajikuta unakimbilia kufanya mambo ambayo ni rahisi na sio muhimu wakati una mambo magumu na muhimu yanayokusubiri.

Kwa kuwa na orodha ya vitu unavyofanya, na kuweka vema kwenye vile ulivyokamilisha inakujengea hisia kwamba wewe ni mkamilishaji mzuri wa mipango yako na utaendelea kuwa unafanya hivyo ili usijiangushe.

Anza leo kuipangilia siku yako, na kila siku jioni kabla hujalala, pitia mipango yako ya siku husika, ona utekelezaji wako kisha weka mipango ya siku inayofuata. Hivyo hivyo unaweza kuipangilia wiki yako kabla hujaianza na hata kupangilia mwezi wako kabla hujauanza.

Maisha ni mipango, kama huweki na kufuata mipango yako, unapoteza maisha yako mwenyewe.

TAMKO LA LEO;

Najua nimekuwa napoteza maisha yangu kwa sababu nayaendesha bila ya mipango. Kuanzia sasa sitaianza siku kabla ya kuorodhesha mambo ambayo napanga kuyafanya. Nitaiendesha siku yangu kwa kufuata mipango yangu na sio kurukia kila kitu kinachoendelea.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.